Habari za Punde

MIGOMBA MABINGWA SIRRO CUP 2018 KIBITI.

Na Jeshi la Polisi
Timu ya Migomba kutoka Wilayani Rufiji mkoani Pwani wametawazwa kuwa mabingwa wa kombe la Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro (Sirro Cup 2018 Kibiti) baada ya kuichapa timu ya Mjawa ya Wilayani Kibiti kwa mikwaju ya penati 12-11 katika fainali iliyopigwa katika uwanja wa Samora Kibiti.

Mchezo huo ulikuwa mkali kwa dakika zote tisini ambapo kila timu ilijitahidi kutafuta nafasi lakini mpaka dakika tisini zinakamilika hakuna timu iliyoweza kuona nyavu za timu pinzani na hivyo kuamuriwa kupigwa kwa mikwaju hiyo iliyopelekea Migomba kuibuka mabingwa.

Kutokana na ushindi huo Migomba walikabidhiwa kombe, pesa taslimu shilingi milioni moja na seti moja ya jezi huku Mjawa wakipata fedha taslimu laki tano na seti moja ya jezi wakati mshindi wa tatu timu ya Mipeko alipata fedha taslimu laki tatu na seti moja ya jezi.

Akizungumza baada ya kuwakabidhi zawadi mabingwa hao, Mkuu wa Mkoa wa Pwani amemuomba IGP Simon Sirro kuendelea kuandaa kombe hilo kwa kuwa limesaidia kuinua vipaji vya vijana wa Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji na kuimarisha usalama kupitia michezo.

“Bila usalama tusingekuwepo leo hii hapa, hivyo nawaasa kuendelea kutoa taarifa za uhalifu ili zifanyiwe kazi kwa maana bila usalama hii burudani tusingeiona hapa na namuomba IGP mwakani tena afanye hivi hivi” Alisema Ndikilo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Kitengo cha Michezo ndani ya Jeshi la Polisi Kamishna 
Msaidizi wa Polisi (ACP) Philip Kalangi alisema jumla ya timu 52 kutoka Wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji zilishiriki michezo hiyo iliyobeba kauli mbiu ya Kibiti Salama, Jamii Salama ikiwa na lengo la kuwakutanisha wakazi wa maeneo hayo kupitia michezo na kupiga vita uhalifu.

Kalangi alisema Programu hiyo ya michezo inafanywa pia katika mikoa mbalimbali kupitia kwa Wakuu wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya na ni endelevu ili kusaidia ushirikishwaji wa jamii katika mapambano dhidi ya uhalifu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.