RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed
Shein ameongoza futari maalum iliyoandaliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ)
na kupongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Benki hiyo katika kufikia
malengo iliyojiwekea.
Hafla hiyo ya futari
ilifanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Verde Mtoni Mjini Zanzibar ambayo ilihudhuriwa
na viongozi wa dini na Serikali, wateja na wanahisa wa Benki ya Watu wa
Zanzibar (PBZ) pamoja na wananchi mbali mbali.
Akizungumza kwa niaba
ya Rais wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohamed Mahmoud
alisema kuwa kujumuika kwa pamoja katika futari ni jambo jema na kutumia fursa
hiyo kutoa shukurani kwa niaba ya waalikwa waliohudhuria katika futari hiyo
adhimu.
Aidha, alieleza kuwa
kufutari kwa pamoja ni sehemu ya utamaduni wa Wazanzibari wa kufutari kwa
pamoja katika mwezi wa Ramadhani ambapo hapo zamani kwa mjini na mashamba
kulikuwa na utamaduni huo ambao ulisaidia kuiweka jamii pamoja sambamba na kuwasaidia wale waliokosa futari
na wale ambao hawakuwa na sehemu ya kufutari.
Hivyo, aliiomba Benki
ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Taasisi nyengine kuendelea na utamaduni huo ambao
unakumbusha mambo ambayo yalikuwa yakifanywa hapo siku za nyuma ya kufutari kwa
pamoja na kuweza kujenga uhusiano mwema na udugu.
Alieleza kuwa Rais Dk.
Shein amefurahi kwa futari hiyo iliyoandaliwa na Benki ya (PBZ) pamoja na waalikwa
wengine wote waliohudhuria katika futari hiyo.
Mapema Mkurugenzi
Mwendeshaji Juma Ameir alieleza mafanikio yaliopatikana kutoka Benki hiyo na
kusisitiza haja ya kuiimarisha Benki ya Kiislamu na kutumia fursa zilizopo kwa
ajili ya kuendeleza miradi mbali mbali kwa wananchi na Serikali.
Alieleza kuwa kwa
kipindi hichi hasa katika kuelekea uchumi wa viwanda Benki ya Kiislamu inaweza
kusaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo la uchumi huo ikiwa ni pamoja na
kufanya mashirikiano na kueleza kuwa Benki hiyo milango yake iko wazi.
Alieleza kuwa mtaji wa
Benki umeongezeka kutoka Bilioni 57 hadi kufikia Bilioni 71 ambapo faida kabla
ya kodi imeongezeka kutoka Bilioni 18.7 hadi 21.8 ambapo faida baada ya kodi
imefikia Bilioni 13.1 ikilinganishwa na mwaka 2016.
Nae Mjumbe wa Bodi ya
Sheria ya Benki ya Kiislamu Abdalla Twalib akitoa shukurani kwa niaba ya
wafanyakazi na uongozi wa (PBZ) kwa waalikwa wote waliohudhuria katika futari
hiyo akiwemo Rais wa Zanzibar Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment