HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR,
MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI WAKATI WA KUTOA
HOJA YA KUAKHIRISHA MKUTANO WA KUMI WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI ULIOJADILI
BAJETI YA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KWA MWAKA FEDHA 2018/2019 -
TAREHE 29 JUNI, 2018
Mheshimiwa Spika,
kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwenye wingi wa
rehma, Muumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake kwa kutujaalia uhai na afya njema na
kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Baraza la Tisa ulioanza tarehe 09 Mei, 2018.
Ninafuraha kuona kwamba shughuli zote zilizopangwa katika ratiba ya
Mkutano huu zimekamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa wa kupigiwa mfano.
Mheshimiwa Spika, Kwa
mara nyengine tena tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuiweka nchi yetu
katika hali ya amani, utulivu, umoja, upendo na mshikamano mkubwa miongoni mwa
wananchi wetu. Hali hii imetuwezesha sisi viongozi na wananchi kutekeleza
majukumu yetu ya kiuchumi na kijamii kwa ufanisi jambo ambalo limechangia kuimarisha
uchumi na ustawi wa nchi yetu. Hivyo, sote hatuna budi kuhakikisha kuwa
tunaisimamia, tunailinda na kuidumisha hali hii kwa mustakbali wa nchi yetu na
wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, kwa umuhimu na uzito wa kipekee napenda kumpongeza kwa dhati Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed
Shein, kwa miongozo yake mbali mbali ya busara na hekima anayoitoa kwetu
inayotuwezesha kusimamia vyema majukumu tunayopangiwa ya kuiendesha Serikali
yetu. Kwa hakika, Dkt. Ali Mohamed Shein
ni dira yetu ya matumaini katika kujenga uchumi imara ambao unaoimarika kila
mwaka na kuleta tija kwa wananchi ambao unatokana na usimamizi na utekelezaji
bora wa Ilani yetu ya CCM ya mwaka 2015 - 2020. Mafanikio haya tumeyapata kutokana
na nia yake thabiti kwa wananchi wake.
Nampongeza sana Rais wetu kwa juhudi zake na kuona mbali katika kuiletea
nchi yetu maendeleo endelevu.
Mheshimiwa Spika, vile vile, napenda kutoa pongezi zangu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa namna anavyosimamia
utekelezaji wa majukumu yake ya kuiongoza nchi yetu. Aidha, nampongeza kwa
dhati namna anavyokisimamia na kukiongoza Chama chetu cha Mapinduzi na Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote
ni mashuhuda wa jinsi alivyoweza kurudisha nidhamu ya utendaji kazi, kuondoa
ubadhirifu wa mali za umma na kuwezesha wananchi wa Tanzania kufaidika kwa
pamoja na rasilimali za nchi na kupata huduma za kijamii ipasavyo. Hongera Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukushukuru na kukupongeza wewe Mheshimiwa
Spika pamoja na Naibu wako, Mhe. Mgeni Hassan Juma, Wenyeviti wa Baraza, Katibu
wa Baraza na Watendaji wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kuliendesha Baraza
letu kwa umahiri na ufanisi mkubwa. Mmefanya kazi kubwa katika kipindi hiki cha
Baraza la Bajeti ambalo lilikuwa na mambo mengi. Naamini busara zako pamoja na
viongozi wenzako zimechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha mkutano huu ambao
leo tunafikia tamati.
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kuwashukuru
Waheshimiwa Wajumbe wenzangu wa Baraza la Wawakilishi kwa kutumia haki yao ya
Kikatiba na Kidemokrasia kwa kuchangia na kuuliza maswali mbali mbali ambayo
Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri wamejitahidi kuyapatia ufafanuzi wa
kina. Nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri kwa kazi
mlioifanya ya kuwaelewesha Waheshimiwa Wajumbe na wananchi wetu kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Kumi wa
Baraza la Tisa tulijadili na kupitisha Bajeti ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Waheshimiwa Wajumbe
walipata nafasi ya kuzichangia kwa umahiri, uweledi na uwazi bajeti zote za
Kisekta na kuzipitisha. Kadhalika, kwa umoja wetu tuliweza kuipitisha
Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/2019, jambo ambalo litaiwezesha Serikali
yetu kutekeleza mipango yake ya kimaendeleo iliyojipangia kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa ombi langu kwa
Waheshimiwa Wajumbe wenzangu pale mtakapogundua kuwa mipango tuliyoipanga
katika Baraza letu hili Tukufu haiendi kama tulivyokubaliana naomba msisite
kuishauri Serikali hata kabla ya muda wa kikao cha Baraza hakijafikia kwani
kuna vikao vyetu halali ambavyo vina uwezo wa kuufanyia kazi ushauri huo.
Mheshimiwa Spika, Mkutano huu pia umejadili Miswada Miwili (2) na kuipitisha kuwa
Sheria. Miswada yenyewe ni:-
(i)
Mswada wa
Sheria ya Matumizi (Appropriation Bill); na
(ii)
Mswada wa
Sheria ya Fedha (Finance Bill).
Hata hivyo Miswada
ifuatayo imesomwa kwa mara ya kwanza:-
(i)
Mswada wa
Sheria ya Wakala wa Uchapaji;
(ii)
Mswada wa
Sheria ya Usimamizi wa Mahkama;
(iii)
Mswada wa
Sheria ya kuanzisha Ofisi ya Ukaguzi wa Elimu Zanzibar.
Aidha, katika Mkutano huu jumla ya maswali ya msingi 279 na maswali ya nyongeza
....... yaliulizwa na kupatiwa ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri.
Kuna maswali mengine yaliyoahidiwa kujibiwa kwa maandishi kutokana na sababu
mbali mbali. Napenda kuwathibitishia Waheshimiwa Wajumbe kuwa maswali yote ya nyongeza
ambayo yameahidiwa kujibiwa kwa maandishi, majibu yake yatafikishwa kwenu kwa
muda muafaka.
Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama Zanzibar ni ya kuridhisha. Upatikanaji wa maji umefikia asilimia 62 ya
mahitaji ya wananchi. Bado kuna asilimia 38 ya wananchi wetu ambao wanaendelea
kusumbuka na huduma ya maji safi na salama, hali hii inatokana na kuongezeka
kwa idadi ya watu, uchakavu wa miundombinu ya maji na kuongezeka kwa shughuli
za kiuchumi na kijamii mijini na vijijini kunakopelekea kutokuwepo kwa uwiano
kati ya maji yanayozalishwa na mahitaji halisi. Ili kukabiliana na tatizo hilo,
Serikali kupitia Mamlaka ya Maji (ZAWA) inaendelea kutekeleza miradi 7 ya maji
chini ya Programu Kuu mbili ya Uhuishaji na Upanuzi wa Shughuli za Maji Mijini
na Programu ya Usambazaji Maji Vijijini.
Programu hizo zina lengo la ujenzi wa matangi, ujenzi wa majengo ya
mitambo ya kutibu maji, uchimbaji na uendelezaji wa visima, ulazaji wa mabomba
mapya, kudhibiti upotevu wa maji pamoja na ukarabati wa miundombinu ya maji.
Juhudi hizi zinafanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na
wananchi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa wananchi wanaopata huduma ya maji kuchangia huduma
hii ili Serikali ipate nguvu ya kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wengine
wenye upungufu wa maji katika maeneo yao.
Sambamba na juhudi hizo, Serikali inaendelea kuwapatia maji wananchi
wake wenye ukosefu wa huduma hii kupitia magari maalum ili kuwaondolea usumbufu
wa kutafuta huduma ya maji safi na salama masafa marefu. Ninawaomba wananchi
waendelee kuwa wastahamilivu kwa wale wanaopata usumbufu wa maji kwani Serikali
inaendelea na juhudi za kulipatia ufumbuzi suala hilo. Sambamba na hilo,
napenda kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa ZAWA, Ndugu Mussa Ramadhan Haji kwa
juhudi yake ya kuwapatia maji safi na salama kwa kiwango kikubwa katika muda
mfupi baada ya uteuzi wake. Ni matumaini
yangu kwamba utaziendeleza juhudi zake hizo.
Mheshimiwa Spika, suala la uuzaji wa ardhi bila ya kufuata
sheria limekuwa likiibuwa mizozo mingi katika nchi yetu. Kwa bahati mbaya
uuzaji huu wa ardhi umekuwa ukichangiwa na baadhi ya watendaji wa Wizara ya
Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati na baadhi ya Masheha wetu. Jambo hili
halikubaliki na wale wote wanaojishughulisha na vitendo hivi watachukuliwa
hatua za kisheria. Natoa agizo kwa Wakuu
wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwafuatilia Masheha wanaoendeleza tamaa zao za
kuuza maeneo ya ardhi bila ya kufuata sheria, hatua kali zichukuliwe licha ya
kuachishwa Usheha.
Ni vyema wananchi
wakaelewa kuwa mara tu baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari,
1964, ardhi yote imewekwa chini ya mamlaka ya Serikali, hivyo ardhi ni mali ya
Serikali na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
ndie msimamizi mkuu. Kwa hivyo kuuza mali ya Serikali bila ya idhini yake
tafsiri yake ni wizi wa mali ya umma. Natoa wito kwa wananchi wote kujiepusha
na tabia ya kuuza ardhi kwani jambo hili ni kosa kisheria. Hivyo, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na
Nishati ndio yenye mamlaka ya kuuza ardhi kisheria kwa idhini ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na sio
mtu au Taasisi nyengine yoyote nchini.
Mheshimiwa Spika, katika msimu uliopita wa mvua za Masika zilizoambatana na upepo
mkali, Zanzibar kama sehemu nyengine za Afrika Mashariki ilikumbwa na mvua
kubwa zilizosababisha athari mbali mbali ikiwa pamoja na vifo vya watoto wanne
(4), uharibifu mkubwa wa miundombinu hasa barabara na makaazi ya watu. Katika
kuwafariji wananchi wake, Serikali imetoa ubani kwa wafiwa na kuwasaidia baadhi
ya wananchi waliopatwa na maafa kwa kuwapa msaada wa chakula pamoja na baadhi
ya vifaa vya ujenzi. Aidha, Serikali
inaendelea na juhudi za kurekebisha athari zilizotokea hasa za ukarabati wa
barabara katika maeneo mbali mbali nchini.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukuwa fursa hii kutoa pole kwa wananchi wote waliopatwa na
maafa katika maeneo mbali mbali ya visiwa vyetu Unguja na
Pemba. Hata hivyo, kwa mara nyengine tena Serikali inaendelea kutoa wito kwa wananchi
kujihadhari na majanga kwa kuepuka ujenzi holela pia kutokujenga katika maeneo
hatarishi yakiwemo mabonde na njia asili za maji pamoja na kuepuka kulaza
mabati katika nyumba zetu ili kupunguza maafa yanayosababishwa na mvua na upepo
hapa visiwani kwetu. Nawapongeza
wananchi kwa juhudi za awali walizozichukua za kuzibua mashimo na kujenga
mitaro ili kuepuka mkusanyiko wa maji na kuweza kupita kirahisi. Hongereni sana wananchi kwa juhudi
mlizozichukua.
Mheshimiwa Spika, kama
tunavyojua kwamba vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto
unaendelea kuwa kero kubwa katika jamii yetu. Ili kukabiliana na vitendo hivyo,
Serikali imeandaa Mpango kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Vitendo vya Ukatili na
Udhalilishaji wa Wanawake na Watoto.
Mpango huu maalum wa miaka 5 (2017 - 2022) ambao utaongeza juhudi za
kupambana na kadhia hii. Sambamba na mpango huo, Serikali imezifanyia
marekebisho baadhi ya Sheria zinazohusiana na udhalilishaji na ukatili wa
wanawake na watoto ikiwemo Sheria ya
Makosa ya Jinai Nam. 6 ya mwaka 2018 na
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya Nam. 7 ya mwaka 2018, ili
kuhakikisha kuwa watendaji wa makosa hayo wanapata adhabu inayostahiki ili
kupunguza na kuyaondoa kabisa matendo hayo mabaya yanayotia aibu nchi yetu,
pamoja na kutoa haki kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji. Sheria hizo
tayari zimeshasainiwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi ambazo zinatoa adhabu kali pamoja na kuondoa dhamana kwa watuhumiwa
wa vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.
Mheshimiwa Spika, Sheria hizo zimeziongezea nguvu Mahkama za Wilaya na Mikoa za kuweza
kutoa adhabu kali zaidi kwa waliotiwa hatiani. Waheshimiwa Wajumbe wenzangu,
Taasisi zinazohusika, wazee, walezi na wananchi wote, napenda kuchukuwa fursa
hii kutoa wito kwenu tuendelee kushirikiana kwa hali na mali katika kupambana
na kadhia hii. Aidha, nawanasihi wazee
wenzangu kuwa linapotokea tukio la udhalilishaji katika familia zetu tuache
tabia ya kumaliza masuala haya kienyeji na kuondoa muhali ili Sheria iweze
kuchukua mkondo wake, vyenginevyo ni kudhoofisha juhudi za Serikali katika
kupambana na vitendo hivyo. Imani yangu
kuwa tukishirikiana kwa pamoja suala la udhalilishaji litabakia kuwa historia,
wananchi watakuwa na amani na vizazi vyetu vitajengeka kitabia na kuwa na
maadili mema. Naomba tushirikiane kwani “Umoja ni Nguvu na Umoja ni Ushindi”.
Napenda kuwakukumbusha wananchi maneno aliyosema Mheshimiwa Rais
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wakati akilihutubia Baraza la Eid
El Fitri tarehe 15 Juni, 2018, alisema:
“Napenda kuwaasa wazazi na walezi
kwamba linapotokezea kosa la udhalilishaji ambalo limefanywa na mtu wa familia,
hatupaswi kabisa kulitolea hukumu au kulimaliza kifamilia. Tunapoamua kuyamaliza matatizo haya kifamilia
au kuchelea kutoa ushahidi sahihi katika vyombo vya sheria, inakuwa ni sawa na
kudhoofisha jitihada za Serikali na kuyaendeleza maovu.” Hivyo, nawasisitiza wananchi kuwa mtu yeyote
ambae atamkingia kifua mdhalilishaji na yeye atachukuliwa kuwa ni mdhalilishaji
na hatua kali dhidi yake zitachukuliwa.
Mheshimiwa Spika, katika
kupambana na usafirishaji, uingizaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya
Zanzibar, Serikali kupitia Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Kudhibiti Dawa za
Kulevya inaendelea na kazi ya kusimamia na kuratibu mapambano dhidi ya dawa
hizo. Pia, Tume inaratibu utekelezaji wa
Sheria ya Dawa za Kulevya Zanzibar. Katika utekelezaji wake imefanya mafunzo
kwa Mahakimu wa Mikoa na Wilaya za Mahkama za Zanzibar, Jeshi la Polisi,
Waendesha Mashtaka, na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi
juu ya Sheria ya Dawa za Kulevya ili waweze kuielewa na kuitekeleza ipasavyo
Sheria hiyo. Aidha, Tume inaendelea kutoa elimu ya kinga dhidi ya matumizi ya
dawa za kulevya kwa lengo la kuwaokoa vijana wetu na matumizi ya dawa
hizi. Vile vile, Tume inaendelea na
utekelezaji wa Mpango wa tiba na marekebisho ya tabia kwa waathirika wa matumzi
ya dawa za kulevya kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali na jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, Tume kwa kushirikiana na wadau wa udhibiti wa dawa za
kulevya imeandaa mkakati wa kuhakikisha kuwa kesi zote za dawa za kulevya
zinawasilishwa Mahkamani haraka ili kuhakikisha kwamba kesi hizo zinapata
ufumbuzi wa haraka na kuepusha kuharibiwa kwa ushahidi. Pia, Tume imeshaanza kazi ya uangamizaji wa
dawa za kulevya pamoja na kuyafanyia kazi maeneo makorofi ya dawa za kulevya kwa
kuliwezesha Jeshi la Polisi kushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za
Mikoa dhidi ya mapambano na kurudisha heshima ya nchi yetu. Hata hivyo, juhudi za pamoja bado
zinahitajika. Naiomba jamii isichoke tuendelee kutoa taaluma kwa vijana wetu
juu ya athari za dawa hizo ili kuwaokoa vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya
Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka
ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi (ZAECA) inaendelea na kazi ya kuelimisha
jamii juu ya athari za rushwa na uhujumu uchumi nchini. Mamlaka imetoa elimu
kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara pamoja na Skuli tofauti za Unguja na
Pemba, vipindi vya Redio na Televisheni pamoja na machapisho mbali mbali. Vile vile, Mamlaka imefanikiwa kufunga
mitambo kwa ajili ya programu ya kupiga simu namba ya bure ambayo ni 113.
Madhumuni ya huduma hii ni kurahisisha kutoa taarifa ya vitendo vya rushwa na
uhujumu Uchumi. Tayari mafanikio ya utumiaji programu ya kupiga simu yameanza
kuonekana kwani wananchi wengi wamepata ari na utayari wa kuripoti matukio ya
rushwa na uhujumu wa uchumi. Napenda kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuitumia
namba hii kuyaripoti matukio ya vitendo vya rushwa ili hatua za haraka ziweze
kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Kuzuia
Rushwa na Uhujumu Uchumi imezindua Mkakati Jumuishi wa Kitaifa wa Kuzuia Rushwa
na Uhujumu wa Uchumi. Lengo la Mkakati
huu ni kuishirikisha jamii katika mapambano dhidi ya rushwa. Sambamba na mkakati huo, Mamlaka inaendelea
kufanya kazi ya udhibiti wa vitendo vya Rushwa na uhujumu wa uchumi katika
Taasisi na Idara mbalimbali za Serikali. Udhibiti huo umepelekea Mamlaka kuokoa
jumla ya Shilingi 169,028,120/=.
Lengo la udhibiti huo ni kuweza kuzuia upotevu wa mapato ya Serikali na
kupunguza vitendo vya Rushwa katika utoaji wa huduma kwa wananchi bila ya
pingamizi zozote, na bila ubaguzi wa aina yoyote.
Mheshimiwa Spika, hali ya usalama barabarani nchini ni tishio
kwa jamii kutokana na uendeshaji ovyo wa vyombo vya moto. Vijana wajulikanao
kama T1 bado hawajadhibitiwa ipasavyo. Kadhalika alama za usalama barabarani
bado hazijafuatwa na madereva walio wengi. Mambo yote haya yanachangia kwa
kiasi kikubwa kutokea kwa ajali za mara kwa mara katika barabara zetu, jambo
ambalo hupelekea kuwasababishia wananchi kupata ulemavu au vifo. Kutokana na hali hiyo, Serikali hairidhishwi
hata kidogo na hali ya usalama barabarani.
Mheshimiwa Spika, naliagiza Jeshi la Polisi na Idara
zinazohusika na vyombo vya moto kushughulikia ipasavyo usalama wa barabarani
kwa kufanya kazi zao kwa uadilifu ili kuokoa maisha ya wananchi wetu na vyombo
vyao. Hivyo, madereva wote wahakikishe kuwa wanafuata sheria za usalama
barabarani na kupunguza mwendo kasi katika maeneo ya makaazi ya watu yakiwemo
skuli na hospitali ili watu wetu watembee barabarani wakiwa katika hali ya
amani. Inasisitizwa pia waendesha vyombo
vya moto vya magurudumu mawili wafuate sheria ya kuvaa kofia ngumu ili kuokoa
maisha yao pindipo wakipata ajali.
Kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria.
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa
kuwa kila ifikapo tarehe 05 Juni ya kila mwaka huwa tunaadhimisha Siku ya
Mazingira Duniani. Kwa mwaka huu wa 2018,
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni “Pambana
na Uchafuzi wa Mazingira kwa kukabiliana na takataka za Plastiki” (Beat Plastic Pollution). Katika kuadhimisha siku hii, Ofisi yangu kwa
kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali zimeanzisha Kampeni Maalum
ya Usafi na Utunzaji wa Mazingira katika Skuli za Msingi na Sekondari kwa
Unguja na Pemba. Lengo kuu la kuanzisha
kampeni hiyo ni kujenga utamaduni wa kutunza na kuhifadhi mazingira miongoni
mwa watoto wetu tangu wakiwa wadogo kwani kama wasemavyo wahenga, ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’ na ‘udongo upate ulimaji‘.
Mheshimiwa Spika, napenda
kuzipongeza Taasisi zote za Serikali
na za watu binafsi pamoja na wananchi wote walioshiriki katika shughuli mbali
mbali za uhifadhi wa mazingira kwa kufanya usafi na upandaji wa miti ikiwemo miche ya mikarafuu, matunda na viungo ambayo jumla ya miche 3,910,401 ilipandwa kwa Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa misitu,
jumla ya hekta 116 za mashamba na hifadhi za Serikali zimepandwa miti katika
msimu huu. Misitu ya jamii hekta 383, mashimo ya mchanga hekta 6 na kando mwa
bahari hekta 56. Haya ni mafanikio
makubwa katika kuhifadhi mazingira yetu.
Hata hivyo, natoa wito kwa wananchi tuitunze miti hii iliyopandwa ili
ikuwe na kuleta manufaa kwetu na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa
Spika, hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula nchini
imeendelea kuimarika katika msimu wa 2017/2018. Uzalishaji wa chakula kwa
ujumla umefikia tani 357,932 ukilinganisha na mahitaji ya tani 583,651 ya
chakula kwa sasa. Kutokana na uzalishaji
huo, hivi sasa Zanzibar inajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 61
ukilinganisha na asilimia 42 iliyorekodiwa kwa mwaka 2016. Mafanikio haya yanatokana na kuwepo kwa hali
nzuri ya hewa iliyopelekea uzalishaji kuwa mzuri na kuimarika kwa mazao ya
mpunga, muhogo, ndizi, viazi vitamu, mahindi, mboga na matunda. Kadhalika,
Serikali inajitahidi kutoa ruzuku kwa wakulima kwa kushirikiana na Taasisi
zisizo za Kiserikali katika kuunga mkono juhudi za kuongeza uzalishaji kwa
kutoa taaluma ya kilimo cha kisasa na matumizi bora ya teknolojia ambayo
yamechangia kwa kiwango kikubwa upatikanaji wa chakula cha kutosha nchini.
Mheshimiwa Spika, wakati
wa uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali,
Waheshimiwa Wajumbe wameonyesha kutokuridhishwa kwao na kiwango cha ujenzi wa
skuli za Serikali zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa nchini. Serikali kwa
upande wake imeridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya kuchunguza suala hili. Naomba
kuisisitiza Kamati hiyo kufanya kazi zake kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kwa
maslahi ya nchi yetu. Pia, Serikali
inaahidi kuifanyia kazi taarifa itakayowasilishwa na Kamati hiyo kwa
kuwachukulia hatua za kisheria watu wote watakaobainika au watakaohusika na
ubadhirifu au kadhia hiyo ya ujenzi huo wa kiwango cha chini ambao umeipotezea
fedha nyingi Serikali yetu na kuhujumu uchumi wetu.
Mheshimiwa Spika, uchumi wa Zanzibar unaendelea kuimarika na kukua siku hadi siku, hali
hii inatokana na ukusanyaji mzuri wa mapato na kuzuia uvujaji wa mianya ya
mapato hayo, kama yalivyokwisha elezewa kwa ufasaha na undani na Mheshimiwa
Waziri wa Fedha na Mipango.
Mafanikio haya yameiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake kwa
uhakika kama ilivyojipangia. Naamini kwamba, Bajeti ya mwaka 2018/2019 ambayo
tumeipitisha hivi punde na kwa uongozi imara na mahiri wa Rais wetu Mheshimiwa
Dkt. Ali Mohamed Shein tutaitekeleza kwa asilimia mia moja na kuleta manufaa
kwa wananchi wa nchi yetu. Nia ya
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuondoa utegemezi katika Bajeti yetu. Mengi yameelezwa na Mheshimiwa Waziri wa
Fedha na Mipango wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti kwa mwaka wa fedha wa
2018/2019.
Mheshimiwa Spika, kwa mara nyengine tena napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha
kukamilisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu kwa ufanisi mkubwa tukiwa
katika hali ya amani, utulivu, upendo na mshikamano mkubwa. Pongezi hizo pia ziwafikie watendaji wote wa
Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na Katibu wa Baraza, Ndugu Raya Issa
Msellem. Vile vile, nawapongeza
Wakalimani wetu wa lugha ya alama ambao wamewawezesha Waheshimiwa Wawakilishi
na wananchi wenye ulemavu wa kusikia kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea
ndani ya Baraza lako Tukufu. Hali
kadhalika, navishukuru vyombo vyote vya habari vilivyoshiriki kikamilifu katika
mkutano huu kwa kuwapatia wananchi taarifa juu ya mwenendo mzima wa majadiliano
ya Wajumbe yaliyokuwa yakiendelea hapa Barazani.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia niwatakie Waheshimiwa Wawakilishi kila la kheri na
mafanikio mema katika kuwatumikia wananchi wao Majimboni mwao na utekelezaji wa
ahadi zao na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 kwa vitendo. Pia, nachukua
nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukamilisha vyema funga ya
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ambapo Mtume wetu Muhammad (SAW) alisema “mwanzo wa mwezi wa Ramadhani ni Rehma,
katikati yake ni Msamaha na mwisho wake ni Kuachwa Huru na moto”, imani na
mafunzo hayo yalipelekea kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitri kwa salama, amani na utulivu mkubwa. Pia, tuliyojifunza katika mwezi huo Mtukufu
wa Ramadhan tuendelee kuyatekeleza. Huku
tukimuomba Mwenyezi Mungu atuongoze katika njia iliyonyooka, njia ya wale
walioneemeshwa sio ya wale waliokasirikiwa au ya wale walioghadhibikiwa na pia
kuiendeleza amani na utulivu wa nchi yetu.
Aidha, ninawatakia Waheshimiwa Wajumbe wote safari njema na mrudi salama
Majimboni mwenu na hasa wale Wajumbe wenzetu wanaokwenda Pemba.
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja
kwamba, Baraza lako Tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 19 Septemba, 2018 saa 3.00 barabara za
asubuhi Mwenyezi Mungu akitujaalia.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment