Habari za Punde

Vijana watakiwa kuchangamkia Fursa, wasizisubiri hadi ziwafuate

   Waziri wa Vijana,Utamaduni.Sanaa na Michezo Balozi Ali Abeid Karume amewataka Vijana kuchangamikia fursa mbali mbali zinazotolewa katika mawizara na sio kusubiri fursa hizo ziwafuate walipo.
   Amesema tayari ameziagiza Taasisi za Wizara kutoa kipaumbele maalum kwa vijana ili waweze kupata fursa zinazopatikana kwa vijana ikiwa ni pamoja na Michezo,Utamaduni na Sanaa.
   Akizungumza na Baraza la Watendaji la Vijana Taifa huko katika Ukumbi la Sanaa,Sensa na Filamu Mwanakwerekwe amesema iwapo Vijana hawatochangamkia fursa hizo lengo la Serikali la kuanzisha Baraza la Vijana halitoweza kufikiwa.
    Amewataka Vijana hao kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kudumisha umoja na mshikamano, Amani na utulivu, kuachana vitendo vya ukatili, kuepukana na utumiaji wa Dawa za kulevya na Ukimwi na Udhalilishaji wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto.
    Hata hivyo Balozi Karume ameilipongeza Baraza la Vijana kutokana na kazi kubwa wanayoifanya ya kuongoza Mabaraza ya Vijana ngazi ya Wialaya na Shehia hasa ukichukulia kuwa suala la kuwaongoza Vijana linataka moyo , ari, utulivu na Busara na kuwataka  kuzidisha juhudi za kiutendaji ili waweze kujipatia kipato na Taifa kwa ujumla.
   Ameeleza kuwa kuanzishwa kwa Baraza la Vijana Zanzibar ni juhudi kubwa iliofanywa na Serikali kuhakikisha kinapatikana chombo kitakachowaunganisha Vijana wote bila kujali itikadi zao za Kisiasa,Kiutamaduni na Kijamii.
    Mbali na hayo amesema Baraza la Vijana Zanzibar ni jukwaa la kuwaunganisha Vijana na Serikali katika masuala ya maeneleo ya Vijana na kuweza kufikia kwa vitendo azma ya ushirikishwaji kamili wa Vijana katika vyombo vya maamuzi hapa nchini.
     Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Zanzibar Khamis Rashid Kheir amesema lengo la kuweka kikao hicho ni kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mpango wa Vijana kwa mwaka 2018/2019 na kuweza kubaini kwa kiasi gani malengo waliojipangia yameweza kutekeleza sambamba na mipango ambayo itaweza kutumika kwa mwaka 2018-2019.
    Amefafanua kuwa matatizo makubwa yanayowakabili ni kutokuwepo kwa mfumo nzuri wa Uongozi katika ngazi za shehia na kupelekea kutopatikana kwa ufanisi nzuri wa kiutendaji hivyo wamejipanga kuhuisha Mabaraza ya Vijana ngazi ya Shehia ili kuweza kuanzisha miradi ya maendeleo na kuweza kujipatia kipato wao na familia zao.
     Miongoni mwa mambo yaliojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na Taarifa ya utekelezaji wa Baraza la Vijana Zanzibar mwaka mmoja 2017-2018, Mpango kazi wa Baraza la Vijana Zanzibar kwa mwaka 2018-2019 na uimarishaji wa Babaraza ya vijana Shehia na Wilaya.
        Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.