Habari za Punde

KUSITISHA MPANGO WA KUTOA MIKOPO KWA WANAFUNZI WA STASHAHADA (DIPLOMA)

Jumapili, Juni 3, 2018
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuutaarifu umma kuwa imesitisha mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaosoma stashahada (Diploma) kuanzia mwaka wa masomo 2018/2019 kama ilivyotangaza awali.

Itakumbukwa kuwa tarehe 10 Mei mwaka huu, HESLB ilitoa mwongozo unaosimamia utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019. Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, unaeleza kuwa HESLB itaanza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na kuwa mwongozo kuhusu utaratibu wa kuomba mikopo hiyo ya wanafunzi wa stashahada ungetolewa baadae.

Hatua hii imechukuliwa ili kuhakikisha kuwa kiasi chote cha TZS 427.5 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi kwa mwaka 2018/2019 zinaelekezwa kwa wanafunzi wenye mikopo hivi sasa na waombaji wapya wahitaji ambao wana sifa za kujiunga na kozi za shahada tu ambao ndiyo walengwa wakuu.

Hivyo basi, tunatoa wito kwa wanafuzi wote wenye sifa za kujiunga na masomo ya shahada katika taasisi za elimu ya juu na ambao ni wahitaji wa mikopo kuhakikisha wanasoma kwa makini mwongozo wa utoaji mikopo na kuuzingatia. Mwongozo unapatikana katika tovuti ya HESLB ambayo ni www.heslb.go.tz

Kwa takwimu za mwaka 2017/2018, takribani maombi 10,027 ya mikopo yaliyowasilishwa Bodi ya Mikopo yalikuwa na upungufu kama vile kutosainiwa, kutokuwa na viambatanisho sahihi n.k.

HESLB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji na pia kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.

Taarifa hii pia inapatikana katika tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).

Imetolewa na:

Abdul-Razaq Badru
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.