Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Saleh Omar Kabi alipowasili katika viwanja vya Skuli ya Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba kuhudhuria hafla ya Iftar ilioandaliwa na Rais wa Zanzibar kwa Wananchi wa Mkoa huo.
WANANCHI wa Mkanyageni, Mkoa wa Kusini Pemba wameeleza
kuridhika kwao na uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Alhaj Dk.Ali Mohamed Shein kutokana na kuwajali wananchi hatua ambayo
imeipelekea Zanzibar kuendelea kupata
neema.
Hafla hiyo ya futari iliandaliwa
na Alhaj Dk. Shein kwa ajili ya wananchi wa Mkanyageni ilifanyika katika viwanja
vya skuli ya Mkanyageni, Mkoa wa Kusini Pemba ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali
mbali wa dini, vyama vya siasa, Serikali pamoja na wananchi wa Mkanyageni na
vijiji vya jirani.
Mke wa Rais wa
Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nae aliungana pamoja na akiwa mama wenzake wa
Mkanyageni katika futari hiyo pamoja na viongozi wanawake wa Kitaifa na
wananchi wengine.
Akitoa neno la
shukurani kwa niaba ya wananchi wa Mkanyageni, Maalim Abdalla Yussuf Ali
alieleza kuwa uongozi wa Rais Dk. Shein umeonesha dhahiri kuwajali wananchi wa
Zanzibar hatua ambayo imejenga mustakbali mwema katika kuimarisha maendeleo
endelevu hapa nchini.
Maalim Abdalla
alieleza kuwa Wananchi wa Mkanyageni wanakila sababu ya kujivunia uongozi wa
Rais Dk. Shein kutokana na imani kubwa anayowaonesha wananchi wa Zanzibar hatua
ambayo imeipelekea Zanzibar kuendelea kupata neema za Mwenyezi Mungu.
Wananachi hao
walieleza kuwa kuridhika kwao si kwa futari tu aliyowaandalia ambao ni
utamaduni aliouweka muda mrefu bali wameridhika na mambo mengi ya maendeleo
anayoyafanya Rais Dk. Shein katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo
kila mmoja anayaona.
Aidha, wananchi hao
walitumia fursa hiyo kumpongeza na kumshukuru Alhaj Dk. Shein kwa kuwaalika
kwenye futari hiyo na kuweza kukaa nae pamoja huku wakitumia fursa hiyo kumuombea
dua kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kuwa na hekima na busara katika uongozi
wake.
Pamoja na hayo,
wananchi hao walieleza kuwa uongozi wa Rais Dk. Shein umekuwa ukisisitiza umoja
na mshikamano jambo ambalo na wao kwa upande wao wamekuwa wakilipa kipaumbele
kwa kutambua umuhimu wake.
Nae Mkuu wa Mkoa Kusini
Pemba Hemed Suleiman Abdalla akitoa neno la shukurani kwa wananchi hao kwa
niaba ya Rais Dk. Shein aliwashukuru na kuwapongeza kwa kukubali muwaliko huo
na kushiriki pamoja katika futari hiyo maalum aliyowaandalia.
Alitumia fursa hiyo
kueleza fadhila za kufutarisha na kusisitiza haja ya kuendelea kumcha
MwenyeziMungu hasa katika kipindi hichi cha mwezi Mtukufu wa Ramadhani..
Aidha, alieleza haja
ya kuendelea kushikamana na kushirikiana na kupendana kwani wananchi wote wa
Zanzibar ni wamoja na kila mmoja amekuwa akimtegemea mwenzake na kusisitiza
kuwa umoja huo walioonesha katika futari hiyo ni vyema wakauendeleza pia,
katika shughuli nyengine za maendeleo.
Sambamba na hayo,
katika neno hilo la shukurani lililotolewa kwa niaba ya Rais Dk. Shein na Mkuu
wa Mkoa huo lilieleza kuwa Alhaj Dk. Shein yuko tayari wakati wote kushirikiana
na wananchi kwa kutambua kuwa ushirikiano ndio njia pekee ya kuimarisha maendeleo
na kuleta umoja miongoni mwa wananchi.
Pia, kiongozi huyo alilieleza
haja kwa wananchi kuendelea kuliombea Taifa ili lizidi kupata neema, baraka na
kuimarisha amani na utulivu uliopo.
Alhaj Dk. Shein amemaliza
ziara yake Kisiwani Pemba iliyoanza
Jumanne Juni 5 mwaka huu ambapo alianza kwa kuwafutarisha wananchi wa Mkoa wa
Kaskazini Pemba huko katika viwanja vya Ikulu ndogo Micheweni na siku ya tarehe
6 aliwafutarisha wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika Ikulu ndogo ya Chake
Chake na anatarajiwa kuanza ziara kama hiyo katika Mikoa ya kisiwani cha Unguja.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment