Habari za Punde

Hotuba ya Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, Wakati wa Uvunaji wa Mpunga Kwa Msimu wa Mwaka 2018. Katika Bonge la Kibokwa.



Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi Zanzibar Mhe. Rashid Ali Juma, akizungumza wakati wa zoezi la Ufunaji wa Mpunga kwa mwaka 2018, katika Bonde la Kibokwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Kwa namna ya kipekee napenda kuwashukuru washirika wetu wa  maendeleleo kwa jitihada wanazozichukua kuunga mkono juhudi za serikali ya Mapinduzi Zanzibar za kuwaletea wananchi maendeleo.  Mradi wa kuongeza uzalishaji wa mpunga Expanded Rice Productivity Project (ERPP) ambao umepata ufadhili wa Benki ya Dunia, ni mfano kati ya miradi mingi ambayo washirika wa maendeleo wanatuunga mkono.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachukua juhudi mbali mbali katika kuona ya kwamba kilimo cha Mpunga kuimarika nchini na mavuno ya mpunga na tija inaongezeka kwa kuongeza bajeti ya serikali kupitia wizara ya kilimo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo, zana za kilimo, dawa za magugu, kuwapatia viwanda vya kusarifia zao la mpunga kwa kutoa daraja zenye ubora mbali mbali.  Kwa kipindi cha miaka 7 (2011/2018) Serikali imekua imetoa kipaumbele na kuongeza maradufu bajeti ya Wizara ya Kilimo ili kukidhi kiwango cha mahitaji ya pembejeo hizi muhimu.

  
Waziri wa Kilimo,Maliasili, Mifugo na Maliasili akizindua uvunaji wa mpunga kwa mwaka 2018 kwenye Bonde la Kibokwa.

Katika msimu huu wa mwaka 2018 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewekeza Tsh. 4,574,665,000 kwa ajili ya kununua pembejeo za kilimo cha mpunga na ununuzi wa matrekta mapya.  Wizara imenunua tani 1,800 za mbolea (tani 900 ya kupandia na 900 ya kukuzia) tani 350 za mbegu na lita 23,400 za dawa ya kuulia magugu na kusambazwa kwa wakulima kwa njia ya ruzuku.  Aidha, kupitia mradi wa kuongeza uzalishaji wa zao la Mpunga (ERPP), jumla tani 459 za mbolea ya kupandia (tani 153) na kukuzia (tani 306) na tani 15 za mbegu zimenunuliwa.  Kati ya tani 459 tani 358 (tani 153 ya kupandia na 205 ya kukuzia) zimeshasambazwa kwa wakulima. Wizara pia imepokea tani 15 za mbegu.  Mbegu na mbolea ya kupandia zimeanza kusambazwa kwa wakulima.


 Viongozi mbali mbali wa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar walioshiriki kwenye uzinduzi wa uvunaji wa Mpunga mwaka 2018 uliozinduliwa 01/02/2018.

Jumla ya matrekta 20 mapya yamenunuliwa pamoja na matrekta 10 tumepata msaada kutoka serikali ya Libya na kuyafanyia matengenezo matrekta 23 makongwe.  Mashine kubwa 5 za kuvunia mpunga zimekarabatiwa na hivi sasa jumla ya mashine 7 zinaouwezo na kufanya kazi ya kuvuna (5 Unguja 2 Pemba).  Mradi wa ZANRICE unaofadhiliwa na GIZ umenunua mashine ndogo mbili 2 ambazo zinztumika katika kazi za uvunaji wa mpunga msimu huu hasa katika maeneo ya umwagiliaji maji uwezo wa kuvuna na kupembua mpunga ekari moja kwa saa zilizogharimu milioni 38.

Nimefarijika sana kwa matokeo mazuri ya ongezeko la mavuno ya mpunga mwaka jana (2017) ya tani 39.683 ikilinganishwa na wastani wa uzalishaji wa tani 20,603.5 kwa miaka mitano 2012 hadi 2016 ikiwa ni ongezeko la tani 19,079.15.  mavuno haya takriban yamekidhi nusu ya mahitaji yetu kwa mwaka ya tani 80,000 za mchele.  Matarajio yetu ni kwamba mavuno yataongezeka katika msimu huu wa mwaka 2018 kufikia wastani wa tani 45,000.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi akikabidhi mashine ya kuvunia mpunga kwa bibi wa Cheju Rukia Wahabi baada ya kumaliza zoezi la uvunaji.

Napenda niwahakikishie kwamba serikali yetu itaendelelea kuweka mazingira mazuri ya uzalishaji kwa kukupatieni pembejeo za uzalishaji kwa wakati na kiwango kinachotosheleza na kuimarisha miundombinu ya umwagiliajimaji Unguja na Pemba.

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Maliasili Mifugo na Uvuvi imo katika mchakato wa kuongeza eneo lililojengwa miundombinu ya umwagiliaji hekta 1,524 kupitia mradi wenye thamani ya dola za kimarekani 58 milioni kwa Unguja na Pemba kupitia mkopo wa EXIM Bank ya Korea kwa lengo la kukifanya kukifanya kilimo chetu kuwa si cha kutegemea mvua ili wakulima wengi zaidi waweze kufaidika na fursa ya kuongeza uzalishaji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.  Vile vile, Serikali itajenga hekta 193 za miundombinu ya umwagiliaji kupitia mradi wa ERPP kwa lengo la uzalishaji wa mbegu ya mpunga hapa hapa nchini.

Kwa vile wakulima mmethibitisha kwamba matumizi ya teknolojia ya shadidi huongeza uzalishaji na tija wa zao la mpunga, hupunguza matumizi ya mbegu pamoja na maji, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi pamoja na watendaji wake wataongeza juhudi katika kusambaza taaluma hii kwa wakulima wengi zaidi kwa kuwa karibu zaidi wakulima ili kuwapatia ushauri wa kitaalamu ikiwa ni pamoja na jinsi ya kupambana na wadudu waharibifu na maradhi.


Badhi ya Mawaziri wa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mkuu wa mkoa Kaskazini wakiwa pamoja na wafanyakazi wa Mradi wa ERPP wakiwa katika picha ya pamoja.

Katika kutekeleza agizo hili Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi itahakikisha kwamba wataalamu wote wa kilimo watatumia muda mwingi wa kazi kutembelea wakulima kujua matatizo yao na kuwapa ushauri unaostahili badala ya kutumia muda mwingi wakiwa maofisini.  Aidha wataalamu wa kilimo na wenyewe wanatakiwa kuwa ni wakulima kwa uanzisha mashamba yao ambayo pia yangetumika kama mashamba ya mfano.

Nimeshuhudia mafanikio wanayoweza kupatikana kupitia kilimo shadidi ukilinganisha na kilimo cha tulichokizowea.  Hivyo niwaombe wakulima wote waliopo katika mabonde yenye miundombinu ya umwagiliaji maji watumie teknolojia ya SHADIDI ili kuweza kuongeza uzalishaji na hatimae tuweze kufikia lengo la Serikali la kujitosheleza kwa mchele angalau kwa kutoka asilimia 39.7 ya sasa  hadi asilimia 60 ifikapo mwaka 2020.

Kwa mara nyegine napenda niwahakikishieni wadau wote wa sekta ya Kilimo kwamba serikali itaendelea kuweka mazingira ya uzalishaji ili kutoa fursa kwa wakulima na wawekezaji pamoja na wataalamu wa kilimo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.  Pia napenda kusisitiza mashirikiano ya karibu baina ya wakulima wataalamu na viongozi ni muhimu sana ili tufanikiwe katika kufikia azma ya serikali ya kuongeza uzalishaji wa mpunga katika maeneo yote ya Unguja na Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.