Habari za Punde

Mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Aongoza Wake Wa Viongozi Kuchangia Watoto Wenye Matatizo ya Moyo Tanzania.


Na.OWM. 
MKE wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa amewaongoza wake wa viongozi kuchangia sh. milioni nne kwa ajili ya watoto wawili wanaohitaji kufanyiwa upasuaji wa moyo.

“Kwa umoja wetu, na kwa kuguswa na uhitaji wa watoto wenye matatizo ya moyo, tuliamua tuchange fedha na zimefikia shilingi milioni nne ili tuweze kusaidia kuchangia gharama za matibabu kwa ajili ya watoto wawili,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Julai 27, 2018) wakati akizungumza na baadhi ya wazazi na watumishi waTaasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili mara baada ya kuwatembelea watoto wengine waliofanyiwa upasuaji wiki hii.

Mama Majaliwa ambaye aliongozana na wake wengine wa viongozi wakiongozwa na Mwenyekiti wa New Millenium Group, Mama Mbonimpaye Mpango, alikabidhi hundi kwa wazazi wa watoto wawili ambao ni Angela Francis (2) na Sabina Mnyango (4).

Watoto hao ni miongoni mwa watoto tisa wenye umri wa miezi mitatu hadi miaka 17 ambao walipangiwa kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na madaktari bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Chain of Hope la Uingereza. Matibabu hayo yalianza Julai 23, mwaka huu na yanatarajiwa kukamilishwa leo.

Mama Majaliwa aliwashukuru madaktari na wauguzi wa JKCI kwa uamuzi wao wa kuwafanyia matibabu watoto hao hapa nchini kwani kwa kufanya hivyo wameokoa fedha za Serikali ambazo zingetumika kumtibu kila mtoto kama wangeamua kupelekwa nje ya nchi kwa matibabu.

Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali ya awamu ya tano kwa jinsi wanavyoendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwenye sekta ya afya hasa kwa mama na mtoto.

Amesema gharama ya matibabu ya mgonjwa mmoja anapopelekwa nje ya nchi kwa siku 14, inakaribia wastani wa sh. milioni 30. “Kwa kuamua kufanya upasuaji huu hapa nchini, mmeongeza faraja kwa watoto wetu; mmewawezesha ndugu na wanafamilia kuwa karibu zaidi na mgonjwa wao tofauti na hali ambavyo ingekuwa kama upasuaji huo ungefanyika nje ya nchi,” amesema.

Mama Majaliwa amesema inakuwa vigumu kwa mzazi kutambua mtoto yupi amezaliwa na tatizo la kwenye moyo pindi tu anapozaliwa. “Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba katika kila watoto 100 wanaozaliwa, mtoto mmoja huwa anazaliwa akiwa na tatizo kwenye moyo wake,” amesema.

Mapema, akitoa taarifa fupi kuhusu taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohamed Janabi alisema wagonjwa wote waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na watoto sita wameruhusiwa kutoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kuendelea na matibabu.

Hii ni mara ya tatu kwa matibabu ya moyo kwa watoto kufanyika tangu Januari mwaka huu. Mara ya kwanza madaktari wa JKCI walishirikiana na wenzao kutoka Uingereza; mara ya pili ulifanyika upasuaji wa moyo bila kufungua kifua ambapo wa Save a Child’s Heart (SACH) kutoka Israel na Berlin Heart Centre ya Ujerumani walishiriki na mara ya tatu walishirikiana na taasisi ya Open Heart International (OHI) ya Australia.

Akitoa shukrani kwa niaba ya wazazi wa watoto hao, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto, Dk. Nice Majani aliwashukuru akinamama hao kwa uamuzi wao wa  kuwasaidia watoto wasio na uwezo wa kuchangia matibabu hayo.

“Tunawashukuru sana kwa msaada wenu kwa sababu kuna wazazi wengine wanashindwa kupata kama hizi kwa sababu ya gharama kubwa za matibabu. Wako Wazazi wanakabiliwa na changamoto za kulea watoto wenye matatizo ya moyo, hawawezi kufanya kazi kama watu wengine kwa sababu ya uhitaji mkubwa wa huduma kwa watoto wao,” alisema.

Alisema hapa Tanzania kuna watoto wapatao 750 ambao wako nje wakisubiri kupatiwa matibabu kama hayo lakini hawawezi kulazwa wote kwa sababu hakuna nafasi ya kutosha. “Tunatamani kujua ni wapi tutapata mtu wa kutusadia kujenga hilo jengo ili tuweze kuwahudumia watoto wengi zaidi,” alisema.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 27, 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.