Habari za Punde

MOI Yawajengea uwezo Wataalamu wa Kubeba Wagonjwa

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface akimkabidhi sare ya mmoja wa Wahitimu wa Mafunzo ya Wataalam wa kubeba Wagonjwa "Patient Transporter" Tunu Salum akipokea sare maalum inayowatambulisha Wataalam hao wa kubebea wagonjwa na kusafirisha 
 Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MOI bwana Fidelis Minja akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya kubeba na kusafirisha wagonjwa ambayo yamehituimishwa leo MOI.
Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface (Aliyeketi katikati) na viongozi wengine waandamizi wa MOI pamoja na kiongozi wa chama cha kuweka na kukopa cha wauguzi (TANA Capt Adam Laeyna) wakiwa katika picha ya pamoja na wahitimu wa mafunzo ya kusafirisha na kubeba wagonjwa. 


Patrick Mvungi- MOI
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa MOI Dkt Respicious Boniface amefunga mafunzo ya wataalamu wa kubeba wagonjwa ‘Patient transporters’ .
Mafunzo hayo yajulikanayo kama ‘Basic life support ‘ yamefanyika kwa miezi 6 na wataalamu 12 wamehitimu ambapo lengo ni kuwapa mbinu za kuwasafirisha na kuwabeba wagonjwa kwenda na kutoka maeneno mbalimbali kwa kuzingatia misingi ya usalama wa mgonjwa.
Dkt. Respicious Boniface amesema kwamba Taasisi ya MOI imewajengea uwezo wataalamu hawa kwa lengo la kuhakikisha wagonjwa wanasafirishwa kwa kuzingatia misingi na maadili ya afya na kuhakikisha wagonjwa wanakua kwenye mkono salama katika kipindi chote wanaposafirishwa kutoka eneo moja kwenda eneo jingine.
“Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa mgongo, nyonga ,magoti au anapata shida kupumua namna yake ya kumsafirisha na kumbeba lazima iwe ya  kisayansi na inahitaji umakini mkubwa lasivyo mgonjwa anaweza kupata tatizo jingine au kufariki, naamini mtatekeleza jukumu hili  kwa umakini mkubwa kama walivyojifunza” alisema Dkt Boniface
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi MOI Bwana Fidelis Minja amesema wataalamu hawa wtajulikana kama patient transporters ambao pamoja na mbinu nyingine wana utaalamu wa kumsaidia mgonjwa endapo atapata shida yoyote pindi atakapo kuwa kwenye mchakato wa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine.
“Hali ya mgonjwa inaweza kubadilika muda wowote akiwa kwenye mchakato wa kuhamishwa au kupelekwa eneo lolote la hospitali, kwamfano mgonjwa anatolewa wodini kwenda kwenye kipimo kama MRI na njiani akapata ‘cardiac arrest’ wataalamu hawa wanaweza kupatia huduma ya msingi kabla hajafika kwenye chumba cha dharura na hivyo kuokoa Maisha yake” alisema bwana Minja.
Aidha, Mkurugenzi wa tiba MOI Dkt Samuel Swai amesema uwepo wa wataalamu hawa utasaidia wagonjwa kuwa salama kabla ya kufika kwenye eneo husika au kwa daktari. Aliongeza kwamba hospitali nyingi zina changamoto ya ubebaji wa wagonjwa kwa namna inayofaa na wakati mwingine wagonjwa wanapata matatizo kwakubebwa katika namna isiyosalama.
Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha kuweka na kukopa cha wauguzi Tanzania (TANA SUCOSS) Capt Adam Francis Leyna ameipongeza taasisi ya MOI kwa jitihada kubwa za kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuahidi kuendelea kufadhili mafunzo mengine yenye tija kwa wauguzi wa MOI na kwa taifa.

Taasisi ya MOI imekua ikiendesha mafunzo kwa wataalamu wake kwa lengo la kuhakikisha watanzania wanapata huduma bora kwa kuzingatia msingi ya usalama wa mgonjwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.