Habari za Punde

Msekwa, Makinda, Kificho Kuwanoa Wabunge Viongozi wa Bunge

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akifungua mafunzo ya Siku Tatu ya Kamati ya Uongozi,Makamu Wenyeviti wa Kamati na Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Bunge, mafunzo hayo yanafanyika katika Ofisi za Bunge Tunguu Zanzibar. wa kwanza Spika Mstaaf wa Tanzania Mhe. Pius Msekwa na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zuberi Ali Maulid na kushoto Spika Mstaaf wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Pandu Ameir Kificho. 


Na.Mwinyimvua Nzuki.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Yustin Ndugai amewataka wabunge wa bunge hilo kutumia kikamilifu mafunzo wanayopatiwa ili waimarishe utendaji wa chombo hicho.
Amesema bunge kama taasisi inayosimamia utendaji wa seriklia na utungaji wa sheria imekuwa ikitoa mafunzo kwa wabunge mara kwa mara yanayolenga kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Akifungua semina ya Kamati uongozi wa bunge katika ofisi ndogo za bunge hilo Tunguu mkoa wa Kusini Unguja, Ndugai alisema bunge lina wajibu wa kuwaendeleza wabunge na watendaji wa chombo mara kwa mara ili kukifanya kuwa uimara.
Alisema ili kuimarisha utendaji wa bunge na wabunge, ofisi yake imeamua kuitisha mafunzo hayo na mengine yatakayofanyika ndani na nje ya nchi ambayo anaamini yatawaimarisha na kuwataka washiriki wa semina hiyo kutumia kuikamilifu uzoefu wa watoa mada walioteuliwa.
“Hii ni nafasi muhimu kwa kila mshiriki hivyo tutumie nafasi ya kuwa na viongozi wastaafu na wataalamu wengine waliopangwa kuwasilisha mada katika semina hii ili kujifunza namna bora ya kuendesha bunge na Kamati zetu”, alisema Spika Ndugai.
Aidha Spika Ndugai aliwataka viongozi wa Kamati na wabunge wa Zanzibar kuitumia ofisi hiyo kikamilifu katika shughuli zao za kibunge na kusisitiza kuwa ujenzi wa ofisi hiyo ulilenga kuimarisha muungano wa Tanzania.
Akiwakaribisha wajumbe wa semina hiyo ambao ni wenyeviti na makamo wenyeviti wa Kamati za kudumu za bunge, Wenyeviti wa tume ya uajiri ya bunge na wajumbe wa Kamati ya uongozi wa bunge, Spika wa baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid aliupongeza uongozi wa bunge na Kamati ya maandalizi kwa kuchagua watoa mada wenye weledi na uwelewa mpana katika uendeshaji wa mabunge nchini.
Alisema hatua hiyo itawasadia wajumbe kuchota sehemu ya uzoefu wa viongozi hao ambao wamelitumikia bunge la Tanzania, baraza la wawakilishi, serikali na vyombo mbali mbali vya kimataifa.
“Uamuzi wenu kuwaleta mama makinda (anna semamba), mzee Kificho (Pandu Ameir) na mzee Pius Msekwa ni wa kupongezwa kwani naamini katika muda huu wa siku mbili tutaendelea kujifunza mambo mengi ambayo yatasaidia uendeshaji wa bunge kama taasisi muhimu kwa maslahi ya jamii”, alisema Maulid.
Akizungumzia mafunzo hayo makamo mwenyekiti wa Kamati ya ustawi wa jamii inayoshughulikia ukimwi na dawa za kulevya dk. Jasmine tisekwa bunga alisema ubora wa mada zilizopangwa katika semina hiyo utasaidia kukuza uelewa wa wabunge kuhusiana na mambo mbali mbali yanayohusiana na kazi zao.
“Katika siku hizi tutajifunza kuhusu maadili, itifaki na mgongano wa maslahi katika uongozi wa umma mabo ambayo ndiyo changamoto kubwa sio katika uongozi wa bunge lakini hata katika maisha yetu ya kaweaida”, alisema Dk. Jasmine ambae ni mbunge wa viti maalum anaewakilisha vyuo vikuu.
Aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa mafunzo kama hayo mara kwa mara, semina hiyo imekuwa ya kipekee kutokana na aina ya wawasilishaji wa mada ambao anaamini watasaidia kubadilisha mitazamo ya viongozi wa Kamati na wabunge kwa ujumla.
Nae Mbunge wa Uzini Zanzibar Salum Rehani Mwinyi alipongeza uongozi wa bunge kuandaa semina hiyo na nyengine amabazo zimekuwa zikiwasaidia viongozi wa Kamati na wabunge kuelewa mambo mbali mbali yanayohusiana na sekta wanazozisimamia.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuwajengea uwezo, pia inatoa nafasi ya kutanua uelewa juu ya mambo mbali hasa kutokana na mabadiliko yanayotokea katika uendeshaji wa bunge na utekelezaji wa mipango ya serikali.
“Kwa muda mrefu tumekuwa na seminakama hizi lakini hii imekuwa ya kipekee kwani inatukumbusha juu ya umuhimu wa maadili, utawala bora, itifaki na diplomasia pamoja na njia za kuepukana na mgongano wa kimaslahi katika utendaji wetu kama viongozi wa umma ambao tuna wajibu kwa wananchi wetu, vyama vyetu na bunge kwa wakati mmoja”, alifafanua Rehani.
Mapema akitoa taarifa ya semina hiyo katibu wa bunge stepen kigaigai aleleza kuwa semina hiyo inatokana na ombi la wajumbe vwa Kamati za kudumu za bunge walilolitoa baada ya uchaguzi wa Kamati hizo mwezi Machi mwaka huu imelenga kuwawezesha wajumbe wa kutambua wajibu na majukumu yao katika utekelezaji wa kazi zao.
Semina hiyo ya siku mbili imehudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Naibu Spika wa bunge hilo Dk. Tulia Akson huku Maspika wastaafu wa bunge na Baraza la Wawakilishi Pius Msekwa, Anna Makinda na Pandu Ameir Kificho wakipangiwa kutoa mada ya uzoefu katika uongozi wa bunge na Kamati za bunge na elimu ya maadili, uongozi na utawala bora na viongozi itakayowasilishwa na mama Makinda kwa niaba ya Uongozi Institute.
Mada nyengine zitakazowasilishwa katika semina hiyo ni mgongano wa maslahi unavyoweza kuathiri maadili ya viongozi wa umma na wabunge itakayowasilishwa na Katibu wa sekretarieti ya maadili ya umma Waziri Kipacha, nafasi ya viongozi wa bunge na wenyeviti wa Kamati za bunge katika ulinzi na usalama wan chi itakayotolewa na Mluli Mahendeka na elimu kuhusu masuala ya diplomasia, itifaki na tabia kwa wabunge na viongozi itakayotolewa na mwalimu mstaafu katika chuo cha Diplomasia Luke Chilambo.
Pamoja na semina hiyo washiriki wa semina hiyo pia watapata nafasi ya kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein na kufanya ziara katika maeneo mbali mbali ya kihistoria ya mji wa Zanzibar ikiwa ni sehemu ya kuhimiza utalii wa ndani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.