Habari za Punde

UJUMBE wa Benki ya Exim ya Indonesia ukiwa pamoja na Kampuni ya ujenzi ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Indonesia umewasili leo Zanzibar kwa ziara ya siku tatu ikiwa ni matokeo ya ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoifanya hivi karibuni


Kiongozi wa Ujumbe wa Eximbank ya Indonesia  pamoja na Kampuni ya Ujenzi,Mkurugenzi Mkuu wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Indonesia Nd,Daniel T.S.Simanjuntak (wa pili kushoto) akibadilishana mawazo na Kaimu Mkurugenzi Mambo ya Nje Ofisi ya Zanzibar Balozi Mohamed Haji Hamza,(kushoto) wakiwepo na katibu wa Rais wa Zanzibar Nd,Haroub Shaibu Mussa,(kulia) Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa,Fedha na Uchumi Mhe.Mohamed Ramia Abdiwawa (wa pili kulia) na Raksa Permana Ibrahim Afisa Ubalozi Indinesia Dar es Salaam,ujumbe huo  ulipowasili   katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume leo,kufuatia ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein  nchini Indonesia kwa mualiko wa Makamo wa Rais wa Nchi hiyo Mohammed Jusuf Kalla hivi karibuni,  [Picha na Ikulu.] 11/08/2018.  

UJUMBE wa Benki ya Exim ya Indonesia ukiwa pamoja na Kampuni ya ujenzi ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Indonesia umewasili leo Zanzibar kwa ziara ya siku tatu ikiwa ni matokeo ya ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliyoifanya hivi karibuni nchini humo.

Ujumbe huo wa watu 7 umewasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa Kanda ya Afrika Daniel Simanjuntak.

Akizungumza mara baada ya mapokezi ya wageni hao Mshauri wa Rais Masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, Fedha na Uchumi Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa alisema kuwa ujio huo ni matokeo ya ziara ya Rais Dk. Shein ambapo katika ziara hiyo makubaliano mbali mbali yalifanyika na tayari baadhi ya makubaliano hayo yanaanza kutekelezwa kupitia ujumbe huo uliofika leo ambao utaangalia maeneo yaliyojadiliwa.

Rais Dk. Shein katika ziara yake hiyo aliyoifanya katika Jamhuri ya Indonesia hivi karibuni ambapo alikutana na viongozi mbali mbali wa nchi hiyo alikwemo mwenyeji wake Makamo wa Rais wa Muhammad Jusuf Kalla na viongozi wengine wa serikali pamoja na wale wa  Kampuni za serikali na zile za binafsi.

Balozi Ramia alieleza kuwa ujumbe huo ni miongoni mwa watendaji kutoka katika baadhi ya sekta ambazo zilipata fursa ya kuzungumza na kufanya makubaliano wakati wa ziara hiyo ambao wanahusika zaidi na masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa, sekta ya ujenzi na miundombinu pamoja na Benki ya EXIM ya nchini humo.

Aliongeza kuwa miongoni mwa shughuli ambazo watazifanya wakiwa hapa Zanzibar ni pamoja na kukutana na baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali wakiwemo uongozi wa WEizara ya Fedha, Miundombinu pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi (ZIPA).

Aidha, Balozi Ramia alieleza kuwa ujumbe huo pia utapata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali wakiwa hapa nchini ikiwa ni pamoja na kutembelea eneo la Kisakasaka, Mji mpya wa Fumba, eneo linalotarajiwa kujengwa Ukumbi wa Kimataifa pamoja na eneo linalotarajiwa kujengwa nyumba za bei nafuu.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mambo ya Ushirikiano wa Kimataifa Kanda ya Afrika Daniel Simanjuntak alieleza kuwa ujio wao una azma ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati ya Zanzibar na Indonesia.

Pamoja na hayo, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa hatua hiyo pia, itaimarisha sekta za maendeleo kwa ajili ya kukuza uchumi na kusisitiza kuwa Indonesia iko tayari kushirikiana na Zanzibar katika kuhakikisha yale yote yaliyozungumzwa na kukubaliwa yanatekelezwa kwa vitendo.

Alisisitiza kuwa ziara ya Dk. Shein nchini humo imezidi kukuza uhusiano na viongozi wa nchi hiyo pamoja na kujenga mashirikiano na taasisi mbali mbali za maendeleo zikiwemo sekta za serikali na sekta binafsi ikiwemo benki ya Exi ambapo ambapo katika ziara hiyo Dk. Shein alikutana nao na kufanya nao mazungumzo.

Katika ziara ya Rais Dk. Shein ambayo aliianza Agosti 1 na kumaliza Agosti 5 mwaka huu  aliianza kwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Makamo wa Rais wa nchi hiyo Muhammad Jusuf Kalla pamoja na viongozi wengine mbali mbali wa ngazi za juu wa Serikali na sekta binafsi wa nchi hiyo.

Rais Dk. Shein akiwa nchini Indonesia alikutana na Wafanyabiashara na Wenyeviwanda kupitia Jumuiya yao ya Wafanyabiashara na Wenyeviwanda wa nchi hiyo huko mjini Jakarta, alitembelea Kampuni ya Uvuvi pamoja na Hospitali ya Harapan Kita iliyopo mjini Jakarta.

Akiwa katika kisiwa cha Bali atapata fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha Udayana,  Chuo cha Utalii kiliopo mjini Bali pamoja na kukutana na uongozi wa kiwanda cha mafuta ya nazi katika ofisi zao zilizopo katika mji wa Bali pamoja na kutembelea maeneo ya utamaduni na kutembelea kiwanda cha kusarifu mwani.

Pia, Dk. Shein katika ziara yake hiyo nchini Indonesia alipata fursa ya kutembelea kisiwa cha Bali ambacho ni maarufu kwa utalii duniani na kufanya mazungumzo ya pamoja na viongozi wakuu wa kisiwa hicho.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.