Habari za Punde

Waziri Dkt Kigwangalla 'Fiti' Kurejea Nyumbani ,Kikwete Amtembelea Tena

Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla kitengo cha mifupa MOI anapopatiwa matibabu alipomtembelea kwa mara nyingine jana.
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Hamisi Kigwangalla kitengo cha mifupa MOI anapopatiwa matibabu alipomtembelea kwa mara nyingine jana.
 Picha zote na Andrew Chale, 


Na Andrew Chale, Dar
Rais Mstaafu wa awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano 
wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amemtembelea na 
kumjulia hali Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hamisi 
Kigwangalla aliyelazwa katika wodi maalum kitengo cha 
Taasisi ya mifupa MOI,  hospitali ya Taifa Muhimbili jijini 
Dar es Salaam kwa mara nyingine tena.

Hii inakuwa ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Dk 
Kigwangalla ambapo awali alimtembelea Agosti 8,2018 
alipokuwa amelazwa Wodi ya Mwaisela akipatiwa Matibabu 
ya awali na juzi Agosti 15,2018 katika wodi ya Taasisi ya 
Mifupa MOI.

Akiwa hospitaini hapo mapema jana, Kikwete ameweza 
kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo mbalimbali 
huku akimtakia unafuu  aendelee na majukumu yake ya kila 
siku na akimpongeza kwa shughuli zake anazozifanya katika 
kuinua sekta ya Utalii pamoja na kulinda rasilimali za 
Maliasili.

“Nikutakie kheri. Nashukuru kwa kukuta unaendelea vizuri 
sasa na nilikuja ukiwa upo unaongea ukiwa umelala 
kitandani na kwa sasa nimekuja tena umeweza kuimarika na 
hata kutembea na kukaa kama hivi hongera sana” alieleza 
Kikwete wakati akimjulia hali Waziri Kigwangalla wodini 
hapo.

Tayari jopo la Madaktari bingwa wa MOI wamebainisha 
kuwa Dkt. Kigwangalla kwa sasa anaendelea vizuri na muda 
wowote anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani ambapo kwa 
sasa sehemu zilizobakia ni mkono wake wa kushoto ambao 
kila siku unaendelea kuimarika.

Hata hivyo, Dkt. Kigwangalla amemweleza Kikwete kuwa 
kwa sasa hali yake inaendelea kuwa vizuri na muda wowote 
anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani  huku akiendelea na 
mazoezi kidogokidogo.

Aidha, jioni ya jana Dkt. Kigwangalla ameweza kufanya 
mazoezi ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa moja 
kuanzia kwenye viunga vya Hospitali hiyo na kuzunguka 
maeneo yanayozunguka Muhimbili na baadae kupanda kwa 
kutumia ngazi katika jengo anapopatiwa matibabu kwa 
miguu mpaka gorofa ya sita. 

Waziri Dkt. Kigwangalla alipata ajali ya gari mnamo Agosti 
4, 2018 huko Manyara akiwa katika ziara ya kikazi ambapo 
katika ajali hiyo iliyokuwa na watu 6, Afisa Habari wa Wizara 
hiyo Hamza Temba alifariki dunia huku watano 
wakijeruhiwa akiwemo yeye anaendelea na matibabu 
Hospitalini hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.