Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Manispa ya Guilin China.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif akimpongeza Mkulima maarufu wa mazao ya Chenza maarufu kwa jina la Konco Bibi Lai Yumei alipomtembea  shambani kwake kuangalia taaluma anayotumia katika kilimo hicho. Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Serikali ya Manispaa ya Guilin katika Jimbo la Guangxi Nchini China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha kwa pamoja masuala yaliyomo ndani ya  Sekta za Utalii, Kilimo na Mazingira kwa nia ya kustawisha Uchumi wa Wananchi wa pande hizo mbili.


Kauli hiyo imetolewa na Naibu Meya wa Manispaa ya Guilin Bibi Wei Fengyun kwenye Hoteli ya Kimataifa ya Shangrila Spa wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Ujumbe wake walipofanya ziara ya Siku mbili kwenye Manispaa hiyo kuangalia miradi ya maendeleo ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo.

Bibi Wei Fengyun alisema Mji wa Guilin umeteuliwa rasmi na Serikali ya China kuwa miongoni mwa Miji iliyopewa fursa ya kuimarisha Sekta ya Utalii kutokana na mazingira ya rasilmali zilizomo ambazo zinaweza pia zikatumiwa katika kusaidia maendeleo ya Tanzania.

Alisema upo uwekezano wa kuandaliwa kwa safari za anga za moja kwa moja kati ya Guilin na Tanzania zinazoweza kusafirisha Watalii na hata Wafanyabiashara lengo likiwa kujikita katika Sekta ya Utalii inayoonekana kuchukuwa nafasi kubwa katika Uchumi wa Dunia.

Naibu Meya huyo wa Manispaa ya Guilin alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba China na Afrika zina mtandao wa pamoja katika kushirikiana kwenye masuala mengi ya Kiuchumi na Maendeleo kupitia Mpango wake wa kusaidia Bara hilo.

Akitoa shukrani zake kwa Uongozi wa Manispaa ya Guilin kwa kutoa mualiko wa ziara yake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar na Tanzania ziko tayari kusaini Mkataba wa ushirikiano kati yake na  Manispaa hiyo ya Guilin.

Balozi Seif  alisema Wananchi na Viongozi wa Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla wana nafasi ya kujifunza mambo mbali mbali ya Kitaalamu yaliyofikiwa na Manispaa ya Guilin katika mipango yake ya kujiletea Maendeleo ya haraka.

Alieleza kwamba Tanzania imejizatiti kuendeleza uhusiano wake wa Kihistoria na Jamuhuri ya Watu wa China kutokana na Mataifa hayo Mawili  kufanya kazi pamoja hasa katika nyanja za Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Ujumbe wake alitembelea sehemu mbali mbali za Kihistoria pamoja na Sekta ya Utalii ambapo walipata nafasi ya kufanya safari ndani ya Mto Maarufu wa  Lijiang kwa boti maalum.

Boti hizo za Serikali zilizokodishwa kwa Makampuni Binafsi hutoa huduma kwa wageni na watalii mbali mbali zaidi kutoka Marekani, Japani, Korea na wenyeji China, takwimu zikionyesha watalii milioni 8,000,000 wenyeji na milioni 6,000,000 hutembezwa kwenye Mto huo  kwa Mwaka.

Ziara ya Balozi Seif  pia ilielekea kwenye Shamba la Matunda ya Chenza maarufu kwa jina la Konco linalomilikiwa na Bibi Lai Yumei ambae piani  Mkuu wa Chama cha Kikoministi cha China katika Manispaa ya Guilin. 

Zaidi ya Tani 700 kwa Mwaka za Matunda hayo huzalishwa na kutengenezwa  bidhaa za asali, achari pamoja na juisi yakilimwa katika mfumo wa mwagiliaji maji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.