Habari za Punde

Risala ya Maadhimisho ya 16 ya Waganga wa Asili Barani Afrika Yalioadhimishwa 31/8/2018 Katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Zanzibar.

Mwakilishi wa Waganga wa Tiba Asili Zanzibar akisoma Risala ya Jumuiya yao Wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Tiba Asilia Barani Afrika. Mheshimiwa Mgeni Rasmi: Waziri Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar na Ujumbe ulioongozananao, Mhe: Waziri wa Afya na Utibabu Zanzibar, Mhe: Naibu Waziri wa Afya na Utibabu Zanzibar Mhe: Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Muwakilishi wa Shirika la Afya W.H.O, M/kiti wa Baraza la Tiba asili na Tiba mbadala Zanzibar na wajumbe wa Baraza lako,  Itifaki imezingatiwa, Viongozi wa Waganga wa asili na Waganga wa asili mliohudhuria, wapendwa waalikwa wote Mabibi na Mabwana Asalamualeikum. (TAIRENI WAGANGA )
Awali ya yote tumshukuru Mola muumba wa Ulimwengu na vilivyomo ndani yake kwa kutuwezesha kufika hapa tukiwa wazima wa afya, pia tunamuoba Mola wetu awape afuweni wale wote walishindwa kufika leo hii kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo za maradhi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi tunapenda kukupa shukrani za pekee kwa kuwacha shughuli zako za kibinafsi na Kiserikali, kuja kujiunga nasi katika hafla hii ya madhimisho ya waganga wa asili hongora sana  Mama yetu mpendwa.
Pia sijawasahau Wanakamati ya maandalizi na wale wote waliochangia kwa njia moja au nyengine katika kufanikisha maadhimisho yetu haya ya leo pia karibuni sana Waganga wenzetu mliotoka Nchi Rafiki za Afrika Mashariki mnastahili pongezi za dhati kwa ujasiri wenu mlituonesha kufika visiwani kwetu na huu ndio udugu halisi utakaotufanya tufike tuwendako katika kuziingiza dawa zetu za asili ndani ya  mfumo wa kisasa, kiuweledi na kiufanisi zaidi.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi chimbuko la maadhimisho haya ni vikao vilivyotokana na Shirika la Afya Ulimwenguni W.H.O kutowa azimio kuwa Nchi za Kiafrika ziwezeshwe kuimarisha dawa zao za asili ili kujipunguzia mzigo mkubwa wa kununuwa madawa ya kisasa ambayo yanahitaji fedha nyingi za kigeni, na ndipo ilipopangwa siku hii ya waganga wa asili Barani Afrika tokea Mwaka 2003 na hapa Zanzibar tunaziadhimisha mfululizo tokea Mwaka huo hadi leo, baadhi ya mafanikio tuliyoyapata ni kama yafuatayo :-
1.     Mashirikiano makubwa kati ya waganga wenyewe, baina ya Nchi moja na nyengine na hatimae tumeweza kuunda Umoja wa waganga wa asili wa Afrika Mashariki na kila ifikapo siku kama hii ya maadhimisho ya waganga  ndipo tunapofanya tathmini ya kujuwa mafanikio, changamoto na matatizo tunayopambananayo.

2.     Pia tunamashirikiano ya karibu baina ya waganga wa asili na madaktari wa Hospitali kwa kutupatiya Semina, Mafunzo na kubadilishana ujuzi kati yetu hivyo basi imepelekea kupeyana rufaa baina yetu, na yale magonjwa yaliyo nje ya uwezo wetu waganga wa asili kuyapeleka Hospitalini na wao madaktari wa Hospitali yale magonjwa wanayoyaona yanastahili kwenda kwa waganga wa asili wanatuleteya hivyo kuanza kuondoka kwa lile Daraja linalotugawa baina ya waganga na madaktari wa Hospitali.
            Sasa napenda kuvitaja Vitengo vya Hospitali ambavyo  tunashirikianavyo :-

·        Kitengo cha chakula dawa na vipodozi kinatufanyia  uchunguzi wa dawa zetu kama hazina maradhara na nisalama kwa kula binaadamu, pia kutuelimisha namna ya utayarishaji bora wa madawa pamoja na kuzifanya ziuzike Kitaifa na Kimataifa.

·        Kitengo cha macho kuna ugonjwa unaitwa mtoto wa jicho hospitalini wanaweza sana kwa kumfanyia mgojwa upasuaji na kuona kama mwanzo hivyo tunakutana kwa semina za kuongeza na ujuzi wa kimatibabu baina yetu.


·        Kitengo cha malaria kinatupatia semina za mara kwa mara na kutuelimisha kuwa inapofikia homa ya mgonjwa kuwa juu inatubidi kumuwahisha hospitalini kwani inaweza kumpanda kichwani na kuonekana kama mgonjwa wa akili lakini hospitalini anapatiwa shindano ya kutuliza malaria.

·        Kitengo cha presha na sukari haya ni magonjwa endelevu ambayo bila ya kuwa na vipimo vya Kihospitali huwezi kumpatia dawa mgonjwa vile vile  inatubidi kutowa rufaa pale tunapoona dawa zetu hazijampatia nafuu mgonjwa na vipimo bado vinaonyesha ugojwa uko juu sana au umeshuka  sana kiasi ambacho utamleteya madhara mgonjwa, hospitalini tunajuwa wambinu za hali ya juu na vifaa vya kimagharibi ambavyo vinakubalika ulimwenguni kote.

Isitoshe kumeandaliwa mradi wa matibabu ya pamoja baina ya waganga wa asili na kitengo cha presha na sukari hivyo kwa kuanziya klinik za tiba asili 20 na viringe 5 vimepatiwa vifaa vya kupima presha na sukari pia kutakiwa kutowa ripoti ya kila miezi 3 - 6 na ya mwaka kwa lengo la kupunguza athari zinazojitokeza kwa wagonjwa wa sukari na presha kwani lengo kuu la mradi huu ni kuwapatia mafunzo na vifaa waganga wote waliosajiliwa na wanaojisshughulisha  kutibu magonjwa ya presha na sukari.

Pia kutokana na magonjwa yenyewe yalivyo yanapelekea baadhi ya wagonjwa kupata kiharusi hivyo kundi hili la watibabu wa asili limepatiwa fursa ya kwenda kujifunza kwa vitendo katika idara ya viungo hospitali ya Mnazimmoja kwa minajili yakutumia mbinu zote mbili za kiasili na kisayansi

Mhe: Mgeni Rasmi kwaruhusa yako napenda kuwasimamisha mama Tanjya na mama Karolina ili uwaone hawa ndio wafadhili wetu wa mradi huu wa presha na sukari hongereni sana kwa mchango wenu wa hali na mali.

·        Kitengo cha T/B, Ukoma na Ukimwi haya ni magonjwa thakili sana kwani ni magonjwa yanayoambukiza  hivyo inatulazimu mashirikiano ya karibu kabisa na madaktari katika kuyatibu kwake.

·        Kitengo cha Mental mashirikiano yetu ni ya karibu sana pale tunapoona ugojwa wa akili hautabiriki hivyo mgonjwa anaweza akaanzia upande mmoja wa matibabu na kumalizia upande wa pili wa matibabu kwani lengo letu ni moja tu kumpatia uzima mgonjwa pia kumeadaliwa mradi wa ugonjwa wa sonona ambao kwa sasa unaratibiwa Wilaya ya Kusini Unguja na Kaskazini A Unguja hivyo waganga wa asili wanaoishi maeneo hayo wamepatiwa semina maalumu za kuutambuwa ugonjwa huo wa sonona na

jinsi ya kuutibu na pale inapoonekana hali ya mgonjwa inazidi watowe rufaa katika vituo vya Afya vilivyoteuliwa kutibu magonjwa hayo ndai ya Wilaya zao na fomu za rufaa wamepatiwa.

Na sisi waganga wa asili tunatowa pongezi kwa madaktari wa Hosptali ya akili na Wafadhili wao kwa kutowa wazo na  kuona iko haja ya waganga wa asili kupatiwa Wodi ya kuwatibu wagonjwa wa akili ndani ya Hospitali ya Mental kwa kweli ni suala la kupigiwa mfano na kuviomba vitengo vyengine kuiga mfano wao.

·        Kitengo cha mama na watoto tuna wakunga wa asili ambao wanauzowefu mkubwa wa kuleya mimba kwa mjamzito mpaka kuzalisha, kutibu watoto lakini bado kunahitajika vipimo vya kisayansi na mbinu mbadala za madaktari wetu mahiri wa kihospitali hivyo lazima mashirikiano kati yao yawepo kwa kiwango kikubwa sana na kuwafanya wakunga wetu wa asili kufaya kazi zao kwa kujiamini zaidi.

·        Kitengo cha Benki ya damu,  hichi ndio moyo wa matibabu kwani mgonjwa anapopungukiwa na damu au kuzidiwa na damu inatulazimu kuupata mchango wao kikamilifu na ndio maana na sisi waganga wa asili tunaishajiisha jamii kujijengea utamaduni wa kuchangia damu na ukichangia unakuwa mwanachama na kupatiwa kadi abayo ni rahisi kwa mgojwa wako kupatiwa damu mara moja pindi inapohitajika.

3.     Vile vile Jamii imekuwa na uwelewa wa kuziamini na kutumia dawa za asili hivyo kuwezesha kufunguliwa Kliniki za dawa za asili na Kliniki za tiba mbadala ambazo kwa sasa zinaendeshwa na rafiki zetu wenye asili ya Eshia kama Wachina na Wakorea kwani Kliniki hizi zinahitaji elimu ya Kisayansi zaidi Kliniki hizi zinauwezo wa kutumia hata vifaa vya Kimagharibi katika kuendesha matibabu yake.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi kama tujuavyo kila penye mafanikio kama haya tuliyoyataja hapo juu huwa hapaachi changamoto na matatizo, kati ya matatizo tuliyonayo ni kama yafuatayo ;-
1.     Tunawaomba waganga wenzetu ambao hawajajisajili na Baraza la Tiba Asili wafanye hivyo kwani kutatuwezesha kupata maendeleo ambayo yalikuwa ndio ndoto zetu za siku nyingi.

2.     Madawa tunayoyafanya tunaomba yapatiwe maabara ya utafiti ambayo itaweza kutowa tathmini ya magonjwa yanayotibiwa na dawa hizo na viwango vya matumizi yake na sio sasa hivi tunapata majibu ya kuwa salama tu kwa mtumizi ya binaadam  huo ni uchunguzi tu na sio utafiti.

3.     Upande wa Madaktari wa Hospitali bado kuna Madaktari ambao wanauwelewa mdogo wa haya mashirikiano yetu kwa kuona wanashiriana na waganga ambao hawana elimu kama waliyonayo wao lakini wajuwe kuitwa kwao Madaktari wa kisasa, kulianzia madaktari wa zamani nao ni waganga wa asili na utaalamu wao huu wa zamani ndio ulioimarishwa hatua kwa hatua mpaka ukafikia hapa tunapouona hivi sasa na wao kuitwa madaktari wa kisasa na kadiri miaka inavyosonga mbele hata ujuzi wao wa hivi sasa utakuwa wa zamani kama wanavyoudharau utaalamu wa waganga wa asili hivi sasa tunaomba tuondokane na dhana hizo potofu tushirikiane baina ya waganga wa asili na madaktari wa hospitalini kwa lengo la kutowa matibabu yaliyo bora ndani ya  jamii.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi: Waziri wa Biashara Viwanda na Masoko Zanzibar tunakujuwa umahiri wako wa kazi ulionao lakini tunaleta ombi letu kwako utufikishie salamu zetu kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa kunahitajika Bajeti maalum ya Mwaka ujao wa Fedha ili tutafutiwe Chuo cha Utafiti ambacho kitaweza kufanya utafiti wa madawa yetu bila kwenda Nchi jirani.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi: sasa kwa ruhusa yako napenda kuitaja kauli mbiu ya Mwaka huu 2018 kama ifuatavyo :-
UTENGENEZAJI WA KIENYEJI WA BIDHAA ZA TIBA ASILI KATKA KANDA YA AFRIKA,
Kama inavyosomeka kauli mbiu yenyewe kuwa ni UTENGENEZAJI wa madawa ya asili yaliyo bora kwani ni ukweli usiopingika kuwa Bara letu la Afrika limebarikiwa miti ya dawa ya kutosha ukilinganisha na Mabara mengine hivyo kama tutajipanga vizuri basi tutatengeneza Masoko makubwa ya bidhaa zitokanazo na mimeya ya asili na kujipatia kipato cha mtu moja moja na Taifa kwa ujumla lakini haya yote yatafanikiwa kama tutaunganisha ujuzi wetu, vitendea kazi na mitaji ya kuongeza thamani madawa yetu ya asili.
Tunamuomba Mola wetu aturejeshe majumbani  kwetu  salama usalimini.
Mungu ibariki Afrika
Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Zanzibar
Asanteni kwa kunisikiliza                      
Mtayarishaji
HAJI JUMA MSANIF
KATIBU MKUU JUTIJAZA
ZANZIBAR

MWISHO


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.