Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akifungua semina ya siku moja iliyowahusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), akuzungumza wakati akiahirisha semina ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Jijini Dodoma.
Mshauri wa Masuala ya Kisheria katika mradi wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) kutoka Benki ya Dunia, Philip Kelly akiwasilisha mada katika semina ya siku moja ya PPP, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Kangi Lugola (Mb) (kulia) akiwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi -CCM (2015) wakati aliposhiriki semina ya Siku moja iliyohusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb).
Baadhi ya Washiriki wa Semina ya siku moja iliyohusisha Mawaziri, Naibu Mawaziri na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na Taasisi zake, wakifuatilia mada kuhusu Ubia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), iliyofanyika katika ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye Walemavu, Mhe. Jenista Mhagama (Mb), (kushoto) akisoma makabrasha kuhusu Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Jijini Dodoma. kushoto kwake ni Naibu Waziri Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Mhandisi Stella Manyaya (Mb) na anayefuatiwa ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga.
Mshauri wa Masuala ya Kisheria katika mradi wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) Bw. Philip Kelly (katikati) akifafanua jambo wakati wa semina ya siku moja ya PPP, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma. Kushoto ni Mtaalamu wa Masuala ya PPP, Bw. Craig Sugden na kulia ni Bw. Abhijit Bhaumik, wote watatu wanatoka Benki ya Dunia.
Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kuahirishwa kwa Semina ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, yaliyohusisha Mawaziri na Manaibu waziri, Jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini-WFM)
Na. Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Serikali ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuanzisha
na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa ubia kati
ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ambapo miradi zaidi ya
11 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji lengo likiwa
ni kufanikisha azma ya kuwa na uchumi wa viwanda.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Idara ya Ubia Sekta ya
Umma na Binafsi (PPP), Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt.
John Mboya wakati akiwasilisha mada ya utekelezaji wa
dhana ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika miradi ya
maendeleo nchini kwenye semina iliyowashirikisha
mawaziri, naibu mawaziri na baadhi ya watendaji wa serikali
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango
jijini Dodoma.
Akiwasilisha mada hiyo, Dkt. John Mboya amesisitiza
umuhimu wa kuwepo kwa umakini mkubwa katika uandaaji
na utekelezaji wa dhana hiyo ya ubia Sekta ya Umma na
Binafsi kwa kuzingatia sheria, sera, miongozo, kanuni na
taratibu mbalimbali zilizopo.
Aidha alizitaka taasisi na wadau wa utekelezaji kuwa tayari
kujifunza kutoka katika nchi zilizoendelea kupitia dhana hii
ya ushirikikishwaji wa sekta binafsi katika kuchochea ukuaji
wa viwanda na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Dkt. Mboya aliitaja baadhi ya miradi iliyoko katika hatua
mbalimbali ya utekelezwaji kwa Ubia kati ya Sekta ya Umma
na Binafsi kuwa ni mradi wa mabasi yaendayo haraka
(DART), Ujenzi wa Viwanda vya dawa, mradi wa VETA
utakaohusisha ujenzi wa vyuo 10 ambavyo vinatarajiwa
kutoa ujuzi mbalimbali kwa wanafunzi wapatao 90,000 ili
kukidhi mahitaji ya wataalamu watakao saidia kufanikisha
uchumi wa viwanda.
"MIradi Mingine ni Ujenzi wa Bandari ya Mwambani,
barabara ya Dar es salaam hadi Chalinze, Ujenzi wa Reli
kwenye miradi ya Mchuchuma hadi Mbambabay mikoa ya
Kusini ya Lindi na Mtwara, Ujenzi wa Reli kuanzia Tanga,
Arusha hadi Musoma, na mradi wa umeme wa Chuo Kikuu
cha Dodoma.
Akijibu swali la Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa, Josesph Kakunda, aliyetaka kujua
kuhusu kuondolewa kwa sheria ya utekelezwaji wa miradi
kwa Ushirikishwaji wa Pamoja kati ya serikali na sekta
binafsi (Joint Venture) ambayo haikufanikiwa kama
ilivyokusudiwa hapo awali, Dkt. Mboya alisema kuwa sheria
hiyo haijaondolewa bali miradi hiyo itatekelezwa kupitia
sheria ya Kampuni.
Akichangia katika mjadala wa semina hiyo, Naibu Waziri wa
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya,
alisema ni vema wakati wa kuchagua miradi wahusika wawe
makini ili kuepuka kuanzisha miradi inayofanana na ambayo
inaweza kuwa chanzo cha kufa kwa miradi iliyotangulia.
"Ninashauri kuwepo kwa fursa ya ushirikishwaji katika
miradi midogo ambayo ina manufaa kwa wananchi ikiwemo
ya ujenzi wa nyumba za waalimu" Alisema Mhandisi
Manyanya
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, alizitaka
taasisi ambazo zinatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi
zielezee umma wa watanzania mafanikio yaliyopatikana ili
kuhamasisha wadau wengine kufuata nyayo hizo
huku akitolea mfano Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini
(TPDC) ambalo nalo liko katika utekelezaji wa dhana hiyo.
Mwenyekiti wa semina hiyo Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, alisema kuwa Serikali
imepeleka Muswada Bungeni unaohusu PPP, ambao
ukipitishwa na Bunge linalotarajiwa kuanza Septemba 4,
2018, utekelezaji wa ubia huo utakwenda kwa kasi zaidi ili
kuiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kukuza uchumi na
kuleta maendeleo ya wananchi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sera, Bunge , Kazi,Vijana, Ajira na Walemavu, Jenister
Mhagama, akiahirisha mafunzo hayo, aliwataka wadau wa
semina hiyo kuendelea kukutana na kuelimishana hadi hapo
marekebisho ya sheria hiyo ya Ubia Sekta ya Umma na
Binafsi (PPP) yatakapofanyika.
"Utekelezwaji wa dhana hii ya Ubia Sekta ya Umma na
Binafsi ndio njia rahisi itakayosaidia kukamilisha miradi
mingi ambayo imeainishwa katika ilani ya uchaguzi ya
Chama Cha Mapainduzi (CCM) na kwenye Mpango wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, bila ushirikiano huu
na sekta binafsi hatuwezi kufikia uchumi wa viwanda kwa
kasi inayotakiwa’’ Alisema Waziri Mhagama.
Semina hiyo ya siku moja imeendeshwa na wataalamu wa
masuala ya Ubia Sekta ya Umma na Binafsi kutoka Benki ya
Dunia, ambapo Jumapili, kamati tatu za Bunge zitapatiwa
elimu na kujengewa uwezo kuhusu dhana hiyo ya PPP.
No comments:
Post a Comment