STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE OF THE
PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 01.10.2018

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amemtumia salamu za rambirambi
Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Joko Widodo kufuatia tetemeko la ardhi lililoambatana
na tsunami lililotokea katika kisiwa cha Sulawesi Ijumaa ya Septemba 28, 2018
na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.
Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar pamoja na wananchi wake,Rais Dk. Shein alituma salamu hizo za rambi
rambi kwa serikali, familia pamoja na ndugu, jamaa na marafiki wa Jamhuri ya Indonesia
kufuatia tukio hilo kubwa la kusikitisha lililosababisha vifo vya watu wapatao
832 na majeruhi kadhaa.
Kufuatia tukio hilo la tetemeko la ardhi
lililoambatana na tsunami ambapo limetokea kwenye kisiwa cha Sulawesi katika
Jamhuri ya Indonesia, Rais Dk. Shein amemtumia salamu hizo za rambirambi Rais Widodo
wa Indonesia na kumtaka kuwa na subira katika kipindi hichi kigumu cha msiba.
Aidha, salamu hizo za rambirambi
alizozituma Rais Dk. Shein alimuomba MwenyeziMungu awape moyo wa subira ndugu,
jamaa, marafiki na wanafamilia wote wa Marehemu pamoja na wananchi wa Indonesia
katika tukio hilo la kuhuzunisha.
Salamu hizo zilipongeza na kuunga mkono
juhudi kubwa zilizochukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Indonesia katika hatua
zote zilizozichukua na timu za uokozi sambamba na kuiweka katika mazingira
mazuri jamii iliyoathirika.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alimuomba Mwenyezi
Mungu kuzilaza roho za marehemu mahala pema peponi pamoja na kumuomba
MwenyeziMungu awajaalie majeruhi wote kupona kwa haraka. Amin.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu awajaalie wale
wote waliopata majeraha kupona kwa haraka…..…na tunapongeza juhudi za uokozi
jinsi zilivyochukuliwa” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo liyotolewa na Rais Dk.
Shein.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment