Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Afanya Ziara ya Kushtukiza Bandari ya Malindu Zanzibar. Na Kutoa Agizo Kupunguzwa Kwa Makontena Katika Bandari Hiyo Kutoa Nafasi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi, akitembelea Bandari Kuu ya Zanzibar malindi wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika bandari hiyo akiongozana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Abdalla Juma wakiwa katika eneo la kuhifadhia Makontena katika bandari hiyo. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Ndg. Abdallah Juma baada ya kutembelea bandari hiyo ilioko malindi Zanzibar na akiuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari kuyaondoa Makontena Matupu Bandarini ya kuyahifadhi katika eneo la mbele ya Hoteli ya Bwawani ili kupunguza mrundikano wa Makontena katika eneo hilo.Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Shirika la Bandari Zanzibar kuyaondosha mara moja Makontena yote yaliyopo katika maeneo ya Bandari ambayo hayana bidhaa ili kuondoa vurumai liliopo katika eneo hilo.
Alisema hatua hiyo mbali ya kuondoa msongamano katika eneo hilo muhimu lakini pia itasaidia kuchukuwa hadhari mapema kabla ya kusubiri kutokea athari inayoweza kusababishwa na uzito wa Makontena yanayoteremshwa katika Bandari hiyo.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Agizo hilo wakati alipofanya ziara ya ghafla Bandarini Malindi mapema asubuhi kuangalia mazingira halisi ya utendaji kazi pamoja na kuona mrundikano wa Makontena ambayo kama haikuchukuliwa hatua za dharura yanaweza kuleta athari hapo baadae.
Alisema katika jitihada za kuwaona Watendaji wa Shirika hilo wanawajibika ipasavyo ni vyema kwa Uongozi wa Shirika kuchukuwa hatua za kuwatoza kodi za ziada Wafanyakazi wote watakaochelewa kutoa Makontena yao Bandarini kwa mujibu wa Taratibu zilizowekwa.
Balozi Seif  aliushauri Uongozi wa Shirika hilo kulitumia eneo la pembezoni mwa Hoteli ya Bwawani ambalo kipindi cha nyuma walikuwa wakilitumia kuweka Makontena kwa vile ujenzi wa eneo kaka masuala ya Uwekezaji bado haujakamilika Kisheria.
Alisema mrundikano wa idadi kubwa ya Makontena kupindukia uwezo wa eneo hilo unaweza kuleta athari kubwa ya kudidimia au kukatika kwa Bandari hiyo iliyojengwa kwa gharama kubwa mno na Serikali Kuu.
Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah alisema Bandari hiyo hupokea Makontena elfu 5,000 yanayoingia kila Mwezi ambapo uwezo wa Bandari ni Makontena elfu 4,180.
Alisema hivi sasa yapo Makontena 2,302 Bandarini kati ya hayo 185 matupu yakiwemo yale ya ziada 400 yanayopaswa kuhamishwa ndani ya eneo hilo la Bandari.
Mkurugenzi Abdullah alimueleza Balozi Seif  kwamba wapo baadhi ya Wafanyabiashara waliokuwa na tabia ya kuifanya bandari kama sehemu ya kuweka Makontena yao lakini mpango huo hivi sasa umetafutiwa dawa kwa mujibu wa utaratibu wa Bandari.
Alisema watendaji wa Shirika hilo kupitia Mkuu wa Operesheni wanajiandaa kuitumia fursa ya kuyahifadhi Makontena matupu katika eneo liliopo mbele ya Hoteli ya Bwawani ili kutekeleza agizo hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.