Habari za Punde

Mbwana Samatta: Sababu ya mshambuliaji wa Tanzania kung’ang’aniwa na klabu za West Ham, Everton na Burnley England

Samatta akicheza dhidi ya Sho Sasaki wa Sanfrecce Hiroshima ya Japan Desemba 13, 2015
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania Mbwana Ally Samatta anang'ang'aniwa na klabu tatu za England, taarifa za vyombo vya habari nchini Uingereza zinasema.
Tetesi zinasema nyota huyo anatafutwa na West Ham United, Everton na Burnley.
Samatta, 25, maarufu kwa Watanzania kama Samagoal ameng'aa sana akichezea klabu ya KRC Genk nchini Ubelgiji.
Amefungia klabu hiyo mabao 11 katika mechi 16 ambazo amewachezea msimu huu, nusu ya mabao hayo akiyafunga barani Ulaya.
Taarifa za kumhusisha Samatta na klabu ya Everton zimetoka kwa mtandao wa hitc.com, mmoja wa mitandao ambayo imeibukia kuwa maarufu kwa taarifa za wachezaji na kuhama kwao.
Samatta, mwenye kimo cha futi 5 inchi 11, amefunga mabao sita katika ligi ndogo ya klabu barani Ulaya, Europa League, na ni hapo ameanza kuonekana na klabu za England.
Mnamo 23 Agosti 2018 Samatta, alifunga 'hat-trick' dhidi ya Brøndby IF katika Europa League kwenye mechi ambayo walishinda 5-2.
Everton wametatizika kumpata mshambuliaji wa kutegemewa tangu nyota wao Romelu Lukaku alipowaacha na kuhamia Manchester United kwa £75 mwaka 2017.
Wamekumbwa na ukame wa mabao msimu huu na zaidi wamesaidiwa na mawinga au viungo wa kati badala ya washambuliaji wao ambao wameonekana butu.
Ndio maana si ajabu wanavutiwa na mchezaji ambaye ameibuka stadi wa kutikisa nyavu.
Walijaribu kujaza pengo kwa kumchukua mchezaji wao wa zamani Wayne Rooney lakini mshambuliaji huyo hakuvuma sana na mwishowe alihamia Marekani.
Mshambuliaji wao wa sasa Oumar Niasse, kwa mujibu wa msn.com anatarajiwa kuihama klabu hiyo ya Merseyside, na inaarifiwa meneja wao Marco Silva anatafuta mchezaji wa kujaza nafasi hiyo.
Cenk Tosun alikuwa amenunuliwa na klabu hiyo Januari lakini baada alianza vibaya kisha akaimarika kabla ya kudidimia tena. Mturuki huyo amewafungia bao moja pekee msimu huu. Alikuwa kwenye benchi mechi yao dhidi ya Leicester City Jumamosi.
Klabu nyingine za Ligi Kuu ya England - West Ham United, Burnley na Brighton - pia zinadaiwa kumfuatilia kwa karibu mchezaji huyo kutoka Afrika Mashariki.
Gazeti la Daily Mirror Jumamosi liliripoti kwamba West Ham wanamfuatilia mchezaji huyo ingawa walisema Everton wanaonekana kuwa na uzito zaidi wa kumtafuta ikizingatiwa kwamba Niasse anatarajiwa kuuzwa Januari.
Everton tayari wana uhusiano na Afrika Mashariki kupitia mdhamini wao SportPesa, na waliibuka kuwa klabu ya kwanza ya Ligi Kuu ya England kuchezea Afrika Mashariki walipocheza dhidi ya mabingwa wa ligi ya Kenya Gor Mahia katika Kombe la SportPesa Super Cup mwaka jana.
Watakuwa pia klabu ya kwanza ya England kuwa mwenyeji wa klabu ya soka ya Afrika Mashariki watakapowakaribisha nyumbani Gor Mahia uwanjani Goodison Park mwezi ujao.
Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016 ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.
Amesalia na miezi 20 hivi kabla ya mkataba wake kumalizika.Samatta alihamia Ubelgiji mwaka mmoja baada yake kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Mwafrika aliyekuwa anacheza ligi za barani Afrika mwaka 2015.
Alishinda vikombe sita vikuu akiwa na TP Mazembe ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kuondoka.
Kufikia Machi mwaka huu, alikuwa ameichezea timu ya taifa ya tanzania mechi 44 na kuwafungia mabao 16 tangu alipowachezea mara ya kwanza mwaka 2011.
Samatta aliichezea Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mnamo mwaka wa 2011.
Ingawa Mtanzania huyo amevuma sana msimu huu, ambapo alifunga mabao manane katika mechi 11 za kwanza, msimu uliopita hakufanya vyema sana. Alifunga mabao saba katika mashindano yote akichezea klabu yake msimu wa 2017/18.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.