Habari za Punde

Mhe. Balozi Seif Ali Iddi Atangaza Kutogombea Tena Nafasi ya Uwakilishi Jimbo la Mahonda Mwaka 2020.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pia ni Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Mhe.Balozi Seif Ali Iddi akitangaza rasmi kutogomea tena nafasi hiyo ifikapo mwaka 2020 alipokuwa akiyazindua Madarasa ya Chuo cha Ujasiri Amali ya Wadi ya Mahonda kwenye Tawi la CCM Kitope “B”.
Baadhi ya Wana CCM na Wananchi wa Wadi ya Mahonda wakimsikiliza Balozi Seif hayupo picha alipokuwa akiyazindua Madarasa ya Chuo cha Ujasiri Amali cha Wadi ya Mahonda.
Baadhi ya Wanafunzi wa Madarasa ya Ushoni, Piko na Kupamba Maharusi wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyotokea kwenye uzinduzi wa Madarasa yao hapo Tawi la CCM Kitope “B”.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif akimpongeza Kijana msoma Utenzi wakati wa hafla ya uzinduzi wa Madarasa ya Vijana ya Ujasiri Amali.
Balozi Seif  akirdhika na mafunzo yanayotolewa katika moja ya Darasa la Ushoni la Chuo cha Ujasiri Amali cha Wadi ya Mahonda baada ya kuyazindua Mafunzo ya Madarasa hayo.
Balozi Seif akiwasisitiza Wanafunzi wa Darasa la Ushoni kuwa makini katika mafunzo yao yatakayokuja wasaidia katika harakati zao za kujitafutia maisha hapo baadae.Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.
Mwakilishi wa Jimbo la Mahonda Balozi Seif Ali Iddi ametangaza rasmi kutogombea tena nafasi hiyo ya Uwakilishi ifikapo Mwaka 2020 na kuwapa fursa Wananchi wa Jimbo hilo kuanza kutakafari mapema Mtu atakayestahiki kushikilia kijiti hicho.
Hata hivyo Balozi Seif alionya kwamba wakati yeye anaendelea kuwatumikia Wananchi waliomchagua katika kipindi kilichobakia cha Miaka Miwili Chama Cha Mapinduzi hakitosita kumchukulia hatua za Nidhamu Mtu au Mwanachama ye yote atakayeamua kuanza kufanya kampeni kabla ya wakati.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Kauli hiyo wakati akizindua rasmi Madarasa ya Vijana ya Chuo cha Ujasiri Amali kilichoanzishwa na Uongozi wa Wadi ya Mahonda hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi Kitope “B” Wilaya ya Kaskazi “B” Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alisema wakati umefika kwa yeye kupumzika baada ya kulitumikia Taifa katika nyadhifa mbali mbali akizitaja baadhi kuwa ni pamoja na Ualimu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania alipotumia muda wake mkubwa na baadae kumalizia katika ulingo wa kisiasa.
“ Nimeamua kutamka hili kwenye Mkutano huu halali unaokubalika kwa mujibu wa Taratibu zetu tulizojiwekea. Nashukuru kwamba umekusanya Wawakilishi wa makundi yote ikiwemo Kina Mama, Wazee, Vijana, Viongozi wa Ngazi za Shina, Jimbo, Wilaya na Mkoa na Serikali kuanzia Shehia hadi Mkoa”. Alisema Balozi Seif.
Balozi Seif  aliwahakikishia Wananchi wa Jimbo la Mahonda kwamba yeye pamoja na Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Bahati Abeid Nassir wataendelea kushirikiana na Uongozi wa Jimbo hilo katika kuona changamoto zinazowakabili Wananchi katika maeneo yao zinapatia ufumbuzi wa kudumu.
“ Nimefanya kazi kubwa ya kuwatumikia Wananchi katika nafasi mbali mbali. Kwa sasa nahitaji kupumzika salama. Si vyema wala uungwana kusubiri kuja kupigwa marungu”. Alisema Balozi Seif.
Alisema katika kipindi hichi kilichobakia akiwa Mwakilishi amesisitiza kuendelea kulishughulikia tatizo la huduma za maji safi na salama ili ifikapo Mwaka 2020 Wananchi wa Jimbo hilo wawe tayari wameridhika na kazi waliyomtuma.
Mwakilishi huyo wa Jimbo la Mahonda ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimshukuru na kumpongeza Katibu wa Wadi ya Mahonda Nd. Juma Kassim kwa ubunifu wake wa kuanzisha Darasa la Vijana la kujifunza mbinu za Ujasiri Amali utakaowapa muelekeo wa kujiajiri wenyewe hapo baadae na kuacha mawazo finyu ya kuendelea kuwa tegemezi kwa Wazee pamoja na Serikali.
Balozi Seif alisema kitendo cha Katibu huyo wa Wadi ya Mahonda cha Kuuza gari yake binafsi na kuamua kununua vifaa na zana za kuanzisha Darasa hilo ni cha Kizalendo na kishujaa kinachopaswa kuungwa mkono na kuigwa na Viongozi wa Wadi nyengine hapa Nchini.
Alisema ubunifu wa miradi ya Maendeleo kwenye shehia, Wadi na Jimbo ndio suluhisho pekee la kuibua kwa fursa za ajira Mitaani hasa ikizingatiwa kwamba hivi sasa Taifa linazalisha Wahitimu wa Vyuo Vikuu wapatao elfu 4,500 kwa kila Mwaka.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia ongezeko hilo la Vijana wasio na ajira ambalo haina uwezo wa kuliajiri kwa pamoja imeshajipanga kusaidia Kundi hilo kupitia mfumo wa Uwezeshaji Kiuchumi kwa kuwapatia mafunzo na nyenzo zitakazowajengea uwezo wa kujitegemea wenyewe.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mahonda Mheshimiwa Bahati Abeid Nassir alisema utaratibu wa Kamati zilizoanza kuundwa kwenye Wadi zilizomo ndani ya Jimbo hilo za kuwakusanya Vijana katika misingi ya kuwapatia Mafunzo ya ujasiri Amali umeanza kuleta matumaini.
Mh. Bahati alisema wakati umefika sasa kwa Uongozi wa Wadi ya Fujoni ukafikiria na kutafakari njia zitakazobuniwa kuibua Madarasa kama hayo ili Jimbo zima liwe tayari kuhimili vuguvugu la Ujasiri Amali utakaopunguza Vijana kukaa vijiweni kitendo ambacho hatimae kinasababisha Vijana hao kujitumbukiza katika matendo maovu.
Katika kuunga mkono jitihada za Uongozi wa Wadi ya Mahonda Mheshimiwa Bahati aliahidi kwamba kwa kushirikiana na Mwakilishi wa Jimbo hilo wanajipanga kuona namna gani wanaweza kuyaongezea nguvu ya Vifaa na Maposho ya Walimu madarasa hayo ili yafikie malengo yaliyokusudia.
Akisoma Risala Mmoja miongoni mwa Wanafunzi wa Madarasa hayo ya Wajasiri Amali Kijana Tatu Juma Khamis alisema Chuo hicho kimeanzishwa mnamo Tarehe 1 Agosti 2018 kikiwa na Wanafunzi 32 na Walimu Wanne.
Tatu Juma alisema uanzishwaji wa Madarasa hayo yatakayokuwa na Fani za Ufundi Ushoni, Kudarizi Mashuka, Piko pamoja na Kupamba Maharusi yatazingatia pia fani nyengine za ujasiri amali kadri hali itakavyoruhusu katika kipindi cha hapo baadae.
Alisema licha ya mafanikio makubwa yaliyoanza kujitokeza katika kipindi kifupi tokea kuanzishwa kwa mafunzo hayo lakini bado zipo baadhi ya changamoto zinazopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa mapema na Viongozi wa Jimbo hilo na hata wahisani wengine wa nje.
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na Usajili wa Chuo, upungufu wa vitendea kazi kama uhaba wa Vyarahani, Vitambaa, posho za Walimu pamoja na Choo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.