Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein, Azindua Mfumo wa Kuimarisha Usalama Katika Mji wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la  Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) alipokuwa akitoa hutuba yake katika sherehe za Uzinduzi wa Mradi wa mfumo wa uimarishaji wa usalama katika Mji wa  Zanzibar uliofanyika leo katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar,[Picha na Ikulu.] 3/10/2018.RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein  amesema kuwa katika kuhakikisha vitendo vyote vinavyohatarisha amani na usalama vinadhibitiwa ipasavyo Serikali imeaandaa mikakati ili wananchi na mali zao pamoja na wageni wanaoitembelea Zanzibar wakiwemo watalii wanakuwa salama.Dk. Shein aliyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Ulinzi wa Mji Salama, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Idrissa Abdulwakil, Kikwajuni Mjini Zanzibar ambapo kabla ya hapo alizindua Kituo cha Mfumo wa kuimarisha usalama kilicho Maisara.

Akiwa Maisara Rais Dk. Shein alipata maelezo juu ya uendeshaji wa kituo hicho pamoja na kupata maelezo juu ya ufanyaji kazi wa vifaa vya mradi huo zikiwemo gari maalum za kuangalia usalama, pikipiki pamoja na kupata maelezo ya matumizi ya ‘drone camera’.

Akitoa hotuba yake katika uzinduzi huo hapo katika ukumbi huo, Rais Dk. Shein alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba sifa njema ya Zanzibar kuwa ni sehemu salama yenye utulivu inabakia na inakuwa ya kudumu na inaendelea kuwa ni kichocheo cha kuongeza kasi ya maendeleo ya nchi katika nyanja zote.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimekuwa zikibuni mikakati mbali mbali na kuvitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kuwa nchi na watu wake wako salama.

Kwa hivyo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Serikali imeamua kuweka vifaa vya kisasa vya ulinzi kwa lengo lan kuimarisha hali ya usalama katika mji wa Zanzibar kwani vifaa hivyo vinauwezo mkubwa wa kuwabaini wahusika wa matukio mbali mbali kwa haraka na ufanisi mkubwa.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuvitumia vyema vifaa hivyo na wavitunze ili viweze kutumika kwa muda mrefu na wote wawe walinzi wa nchi yao huku akisisitiza kuwa amani, umoja na usalama hivi sasa utaimarika zaidi.

Dk. Shein alisema kuwa suala la kusimamia usalama wa wananchi popote walipo ni jukumu la msingi la Serikali ambapo wajibu huo umebainishwa wazi katika Ibara ya 9 Kifungu cha 7 (b) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kinacholeza kwamba.
“Usalama na hali nzuri kwa wananchi itakuwa ndiyo lengo kubwa la Serikali”, alinukuu Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein aliwatahadharisha wale wote wanaofanya magendo ya karafuu, sukari, mafuta na bidhaa nyengine hasa katika maeneo ya visiwa vidogo vidogo waache mara moja kwani mambo hivi sasa yamebadilishwa huku akisema kuwa mradi huo utaendelezwa katika awamu ya Pili kwa Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja na mikoa yote ya Pemba.

Alisema Serikali imeweka mazingatio ya kiulinzi katika kuhakikisha usalama wa Mji Mkongwe kutokana na umuhimu wa hadhi ya kuwa hazina ya Zanzibar na Urithi wa Kimataifa kama unavyotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).

Dk. Shein alieleza kuridhika kwake kuona kuwa utekelezaji wa Mradi huo unafanywa kwa pamoja baina ya wataalamu wa kigeni na wataalamu Wazalendo huku akisisitiza kuwa utaratibu huo unasaidia kuwaachia ujuzi wataalamu wazalendo ili waweze kuutumia katika kuuendeleza mradi huo hata baada ya kuondoka wataalamu wa kigeni.

“Kuna usemi katika lugha ya Kiengereza uanaosema “The ball is in your court”, yaani sasa mpira umo ndani ya kiwanja chenu, kwa hivyo ni jukumu la wataalamu wetu wajitume na wafanye kazi kwa bidii na maarifa, ili waweze kujenga uwezo na hatimae waweze kujitegemea kutokana na taaluma walioipata”,alisema Dk. Shein.

Aidha, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuuweka mji wa Zanzibar katika hali ya usafi na kueleza kuwa kutokana na uwepo wa mradi huo hivi sasa anamatumaini makubwa kuwa suala la usafi litaimarika kwani wale wote wanaokwenda kinyume na hali hiyo wataonekana.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuimarisha amani na usalama na kueleza kuwa hakuna mbadala wa amani na umoja kwani vitu hivyo vina gharama kubwa kuvipata pale vinapokosekana.” Zanzibar salama inawezekana”,alisisitiza Rais Dk. Shein.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Khair alisema kuwa mradi huo umekuja kwa lengo la kutekeleza matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na kutekeleza ahadi yake wakati alipokuwa akiinadi Ilani hiyo pale aliposema kuwa Wapiganaji wa vikosi vya SMZ watafanya kazi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa kuwaongezea vitendea kazi pamoja na kuimarisha maslahi yao.

Lengo la mradi huo ni kuimarisha usalama katika Mji wa Zanzibar pamoja na kuimarisha uchumi kwani bila ya mawasiliano na usalama hapatakuwa na uchumi mzuri “sasa mambo yatakuwa bambam”alisisitiza Waziri.

Alisema kuwa sasa kutapatikana taarifa zote na hakuna atakaedanganya hasa wale wakusanyaji mapato na kueleza kuwa Zanzibar inategemea biashara na utalii na moja lililoibuliwa na maabara ya utalii ni kuimarisha usalama.

Aliongeza kuwa sasa mji wa Zanzibar ni salama pamoja na kueleza kuwa Dk. Shein amewawezesha kuweza kukabiliana na matukio ya kihalifu na yale ya uokozi kwa kukabiliana nayo kisasa kutokana na vitendea kazi vya kisasa.

Alisema kuwa watendaji 56 wenye elimu ya Digirii wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kuendesha mradi huo ambao watakuwa wafanyakazi wa Idara ya Vikosi vya Ulinzi na usalama na hivi karibuni watapelekwa vijana maalum masomoni na kusema kuwa Kampuni ya “ROM Solution Ltd” wataukabidhi mradi huo kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mwaka 2020 lakini tayari hivi sasa kimeshaanza kufanya kazi.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Radhia Rashid Haroub alisema kuwa Serikali iliamua kuanzisha mradi huo wa kuimarisha mfumo wa usalama hapa Zanzibar katika mwezi April mwaka 2015 na kutilioana saini na Kampuni ya “ROM Solution Ltd”.

Kuimarisha ulinzi kufikia katika kiwango cha Kimataifa, katika maeneo ya uwanja wa ndege, bandarini, Mji Mkongwe na baadhi ya barabara kuu za kuingilia katika Mji wa Zanzibar uwanja wa ndege ikiwa ni pamoja na gari tatu katika  viwanja vya ndege, mbili Unguja na moja Pemba

Alisema kuwa jumla ya Kamera 56 zimefungwa katika eneo la uwanja wa ndege na bandarini kamera 42 katika eneo yanayozunguka Bandari, boti maalum kwa ajili ya ulinzi wa baharini nazo umeongezeka, kamera 682 zimewekwa katika Mji Mkongwe  na Kamera 96 zimewekwa katika barabara ambazo zinauwezo wa kubaini vyombo vya usafiri vinavyokeuka sheria, ambapo kwa ujumla Kamera 877 zimefungwa katika mradi huo.

Aliongeza kuwa ndege zisizo rubani “drones” tatu, pikipiki 20 maalum, redio seti 50, gari 15 kwa ajili ya mradi huo zimenunuliwa pamoja na vifaa vyenginevyo.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama katika Mkoa huo alitoa shukurani kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein kwa uamuzi wake wa kuanzisha mradi huo ambao una umuhimu mkubwa kwa usalama wa mji wa Zanzibar

Nae Mkuu wa Kampuni ya “ROM Solution Ltd” George Alexandru alieleza mafanikio ya mradi huo na jinsi hivi sasa Zanzibar ilivyokuwa imepiga hatua katika suala la usalama wa mji wake huku akieleza kuwa mji wa Zanzibar unaingia katika miongoni mwa miji salama duniani.

Viongozi mbali mbali walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar pamoja na viongozi wengine wa Serikali, vyama vya siasa, Mabalozi wadogo wanaofanya kazi Zanzibar pamoja na wananchi.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.