Habari za Punde

Semina ya Kuwajengea Uwezo Watendaji wa Afya Zanzibar Kuhusiana na Virusi Vya YA Ukimwi.

Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akifungua semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa afya katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Semina hiyo imefanyika Doubletree Hotel Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed akifungua semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa afya katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi. Semina hiyo imefanyika Doubletree Hotel Mjini Zanzibar.
Dkt. Farhat Khalid akiwasilisha mada ya hali ya maambukizi ya HIV Zanzibar pamoja na utoaji dawa za ART katika semina ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa afya iliyofanyika Doubletree Hotel Mjini Zanzibar.

Baadhi ya washiriki wa semina ya siku tatu yakuwajengea uwezo wafanyakazi wa afya katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi wakifuatilia mada mbalimbali zilizo wasilishwa.
Picha na Makame Mshenga.
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 19.11.2018
Imeelezwa kuwa kasi ya Wanaume kujitokeza kupima maambukizi ya UKIMWI ni ndogo ikilinganishwa na Wanawake hivyo kuna haja ya wao kubadilika ili kukabiliana na ongezeko la maradhi hayo nchini.
Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ameyasema hayo alipofungua  semina ya siku tatu ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa afya wanaotoa huduma kwa watoto wanaoishi na virusi vya Ukimwi huko Hotel ya Doubletree mjini Zanzibar.
Amesema watakapobaini hali ya maambukizi watakuwa na uwezo wa kujua namna gani ya kuishi wakiwa katika hali hiyo ya maambukizi.
Amesema kwa sasa hali ya maambukizi inaridhisha ambapo kwa ujumla Zanzibar ipo na asilimia 0.4 ya maambukizi ya Ukimwi.
Ameongeza kuwa kupungua huko kumetokana na namna Serikali inavyojitahidi katika kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na ongezeko la Bajeti ya Dawa kupitia Wizara ya Afya.
Hata hivyo ameongeza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha Wananchi wanakuwa na uwelewa wa kutosha juu ya maambukizi ya maradhi hayo na kukabiliana nayo.
“Pamoja na Serikali kufanya wajibu wake wa kutoa elimu na Dawa za matibabu wananchi inabidi tubadili tabia, njia nyingi za kupata maambukizi ni njia zinazoweza kuepukika ikiwemo kujiepusha na zinaa”Alisema Waziri Hamad
 Kwa upande wake Dkt. Farhat Khalid akiwasilisha mada ya hali ya maambukizi ya HIV Zanzibar amesema licha ya kupiga hatua katika kupambana na UKIMWI bado zipo changamoto ambazo zinarudisha nyuma juhudi zao.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni watu hasa wanaume kutokujitokeza kwa wingi kupima Virusi vya HIV jambo ambalo linapaswa kuepukwa.
“Utakuta Mwanamme anampeleka Mwenza wake kupima akijua kwamba kama hana maambukizi basi naye atakuwa hana..hii si sawa, au wengine wanashindwa kuja kuchukua Dawa za ARV na kukimbilia dawa za asili” alisema Dkt. Farhat
Hata hivyo alisema Wizara itaendelea kutekeleza wajibu wake ikiwa ni pamoja na utoaji dawa na elimu kwa Wananchi wote ili kuyaondoa maambukizi hayo.
Kwa upande wake Dkt. Aboubakar Magimbi anayefanya kazi katika Program ya kukabiliana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa watoto Tanzania, amesema kiujumla hali ya maambukizi imepungua kutoka asilimia 5 hadi 4.7 Tanzania bara.
Amesema hali hiyo pia inatokana na mipangilio mingi ya serikali ya kupambana na Ukimwi ikiwemo marekebisho ya Sera ili kukabiliana na Ukimwi.
Hata hivyo amesema yapo baadhi ya maeneo hali ya maambukizi si nzuri na hivyo juhudi zinatakiwa kuendelezwa ili kuepukana na Maradhi hayo nchini.
Semina hiyo ya siku tatu inawashirikisha Wadau wanaohusika na matibabu ya Watoto walioambukizwa HIV kutoka Zanzibar, Tanzania Bara, Msumbiji na Uganda ambapo pia Wakufunzi wanatoka katika nchi za Marekani, Uingereza, Itali na Afrika kusini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.