Habari za Punde

Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) lawatoa kifungoni wanamuziki Diamond Platnumz na Rayvany

Mamlaka nchini Tanzania zimewafungulia wasanii nyota wawili wa muziki Diamond Platnumz na Rayvany ambao walifungiwa kwa muda usiojulikana kwa kutumbuiza kibao kilichofungiwa.
Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) limetangaza jana kuwa wasanii hao ambao walifungiwa mwishoni mwa mwaka jana wapo huru kuendelea na kazi zao za sanaa. Uamuzi wa Basata ulifuatia kitendo cha wasanii hao kutumbuiza jukwaani kibao kilichopigwa marufuku na mamlaka cha Mwanza.
Kwa mujibu wa Basata, kibao cha Mwanza "kinaenda kinyume cha maadili na kuhamasisha ngono". Mwimbo huo ulifungiwa rasmi Novemba 12 lakini wasanii hao wakautumbuiza kwenye tamasha la Wasafi Festival Jijini Mwanza mwezi uliopita. Tamasha hilo pia lilipigwa marufuku.
Taarifa iliyotolewa Jumanne jioni na Basata imeeleza kuwa wawili hao wametolewa kifungoni baada ya "kupokea maombi kadhaa ya kukiri kosa na kuomba msamaha kutoka kwa wasanii tajwa na kampuni ya Wasafi Company Limited (WCB)."
Kwa mujibu wa taarifa iliyotiwa saini na Katibu Mtendaji wa Basata,Godfrey Mngereza, baada ya kupokea maombi hayo na kuzingatia jukumu la baraza hilo la "kusimamia, kuendeleza na kukuza kazi za wasaniina sekta ya sanaa nchini, Baraza limeamua kuwaruhusu wasanii tajwa kuendelea na shughuli za sanaa."

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.