Habari za Punde

Vituo vya Uzamiaji na Uokozi vyajengwa kukabili majanga baharini * KMKM yapatiwa boti za kisasa za Uokozi, vifaa vya uzamiaji * 'Drone' kutumika kuimarisha ulinzi baharini


Na.Abdi.Shamnah. Ikulu.Zanzibar.
Nidhahiri kuwa kwa miongo kadhaa ijayo, Wazanzibari wataendelea kukumbuka majanga makubwa yaliotikisa umma na kuibua huzuni na majonzi yasiofutika milele.
Itakumbukwa ilikuwa ni Julai 18, 2012 pale Meli ya Mv Skagit ilipozama katika mkondo wa bahari ya Zanzibar, ilipokuwa safarini ikitokea jijini Dar es Salaam kuelekea Zanzibar, ikiaminika kubeba zaidi ya abiria 200.
Tukio hilo lilijiri, ikiwa ni kipindi cha takriban miezi kumi tu, tangu pale mshtuko mkubwa ulipowakumba Wazanzibari baada ya tukio la kuzama kwa meli ya Mv. Spice Islander .
Wakati meli hiyo  ikipatwa na janga hilo ikitokea Unguja kuelekea kisiwani Pemba ilikuwa imebeba abiria zaidi ya 2,400.
Maswahibu hayo na mengine mengi yanayowakumba wananchi, hususan wale wanaotumia bahari katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo kuzama kwa vyombo vya uvuvi, imekuwa ni donda ndugu lisilopona na daima yamekuwa yakiziweka rehani roho na maisha ya Wazanzibari  kila kukicha.
Kuambatana na matukio hayo ya kuzama kwa vyombo mbali mbali baharini na kupoteza roho na mali za watu, kumekuwepo sababu kadhaa zinazohusishwa na majanga hayo, ikiwemo dhana za uzembe miongoni mwa watendaji, taasisi na wakati mwengine majanga ya kimaumbile (natural disaster).
Pamoja na hatua za haraka  zinazochukuliwa na Serikali kupitia Idara na taasisi zake katika kufanya uokozi, pale majanga hayo yanapojiri, bado kumekuwepo malalamiko ya kuwepo kasoro kadhaa za kiutendaji.
Kuchelewa kufika kwa wakati eneo la tukio, uwepo wa vifaa na zana duni za uokozi, mbinu za kale katika uokozi pamoja na mapungufu kadhaa yanayojitokeza, ni miongoni mwa chanagmoto zinazosababisha kupoteza mamaia ya  roho za wananchi.
Aidha,  huduma za mwanzo nazo zimekuwa zikipatikana katika hali ya kulegalega, huku zikiwa hazina uhakika wa kupatikana kwake kabla au baada ya wahanga kuokolewa.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, iliyo chini ya uongozi thabiti wa Rais Dk. Ali Mohamed, mwanamapinduzi  na muumini wa amani na usalama, imetathmin kwa kina matukio yanayoendelea kuikumba jamii kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi.
Hakika imejifunza kutokana na makosa. Baada ya tathmin ya kina imeona kuna umuhimu wa kujikinga kutokana na  maafa hayo na pale yanapotokea kwa bahati mbaya kutokana na majaaliwa ya Mungu, basi ni  vyema kuhakikisha hatua muafaka zinachukuliwa kukabiliana na majanga hayo.
Katika hatua hiyo imeona kuwepo umuhimu wa kuwa na vifaa bora na vya kisasa vya uokozi pamoja na wananchi wanaoendesha shughuli zao za kimaisha baharini kupatiwa mafunzo mbali mbali.
Hivi karibuni, Wazanzibari waliadhimisha miaka 55 ya Mapinduzi matukufu ya 1964, ambapo miongoni mwa miradi mikubwa na muhimu iliyozinduliwa na kupamba sherehe hizo, ilikuwa ni 'Ufunguzi wa mradi wa Vituo vya Uzamiaji na Uokozi Zanzibar', hafla iliyofanyika Mkoani Kisiwani Pemba.

Sherehe hii adhimu ilihitimishwa kwa mgeni rasmi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein kuzindua kituo hicho pamoja na Boti ya Uokozi (kwa niaba ya vituo vyengine Unguja na Pemba) .
Katika hafla hiyo, Dk. Shein alipata fursa ya kuzungumza na wananchi kuhusu hatua ya Serikali ya kutumia gharama kubwa katika kuimarisha  usalama  wa wananchi na mali zao, hususan wale wanaotumia bahari katika shughuli zao za kila siku .
Amesema Serikali imelazimika kubuni mradi mkubwa wa 'Zanzibar salama' kwa lengo la kuhakikisha maeneo ya bahari, nchi kavu  pamoja na angani yanakuwa salama muda wote.
Anasema uzinduzi wa vituo vya Uokozi na Uzamiaji, ni awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo, ikitanguliwa na ile ya uwekaji wa CCTV Camera katika maeneo mbali mbali ya Mji Mkongwe na maeneo mengine ya mji wa Zanzibar.
Dk.Shein amebainisha kuwa mradi huo unahusisha mambo mbali mbali, ikiwemo ujenzi wa vituo, vifaa vya mawasiliano, utoaji wa mafunzo kwa askari pamoja na wananchi.
Anasema hatua ya ujenzi wa vituo hivyo inakwenda sambamba na dhamira ya Mapinduzi matukufu ya 1964, pamoja na Ilani ya CCM ya 2015-2020 iliyoweka bayana kuhakikisha usalama wa Wazanzibari unaimarishwa maeneo yote.
Anasema, Serikali imelazimika kubuni mradi huo baada ya kuwepo matukio kadhaa baharini yaliosababisha maafa makubwa ya wananchi na upotevu mkubwa wa mali zao.
Anabainisha kuwa mradi huo ni mpango mbadala katika kukabiliana na majanga hayo, hivyo kuwahahakikishia wananchi usalama wa kutosha muda wote na mahala popote.
Dk. Shein alipongeza juhudi za Wizara ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ katika kusimamia ununuzi wa vifaa hivyo, akibainisha kuwa ni bora na vya kisasa vitakavyowahakikishia usalama wananchi  na wageni wanaouzuru hapa nchini.
Anaeleza kuwa pamoja na badhi ya watu kufanya matukio mbali mbali kwa lengo la kuhujumu uchumi wa Taifa, Zanzibar itaendelea kubaki salama muda wote, sambamba na kupata sifa kubwa duniani kote.
Anasema suala la usalama wa nchi, ni jambo lisilo na majadala kwa kuzingatia kuwa uchumi wa Taifa utaweza kuimarika tu pale panapokuwa na amani ya kutosha na kutoa fursa kwa wananchi kutekeleza shughuli zao za maendeleo bila vikwazo vyovyote.
Aidha, amesema Ustawi wa Uchumi wa Zanzibar, unaotegemea zaidi sekta ya Utalii, utakuwa endelevu  endapo tu usalama wa nchi utashamiri.
Akigusia utendaji kazi wa Idara maalum za SMZ, Dk. Shein anasema taasisi hizo zinafanyakazi kwa misingi ya sheria na Katiba ya Zanzibar.
Alisema kikosi cha KMKM kina uwezo mkubwa wa kiutendaji na ndio maana kimekuwa kikishiriki kikamilifu katika kukabiliana na matukio mbali mbali baharini, ikiwemo majanga, usalama wa taifa pamoja na uhalifu (magendo) .
 Dk. Shein ametumia fursa hiyo kupingana na mitazamo ya baadhi ya watu kuwa Vikosi vya SMZ, ikiwemo JKU, KVZ, Mafunzo, KMKM pamoja na Zimamoto zimekuwa zikifanyakazi kwa kuzingatia utashi wao.
Amewataka wananchi wenye matatizo na askari wa vikosi hivyo kufuata miongozo ya kisheria badala ya kujikita katika hisia pekee.
"Kazi zinafanywa kwa kuzingatia Katiba ya Zanzibar na sheria zilizoandikwa bila ya kudhulumu au kudhuru mtu", anasema.
Dk. Shein aliwawahakikishia Wananchi wa Zanzibar kuwa pamoja na mradi huo kugharimu fedha nyingi, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kuutekeleza kwa ufanisi mkubwa ikiwa  haina deni lolote.
Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalum za SMZ Radhia Rashid Haroub  anasema Ujenzi wa Vituo vya Uzamiaji na Uokozi , ni mradi wa miaka minne (4), ulioanza kutekelezwa rasmi katika mwaka wa fedha 2014/2015, ukipangiwa kutumia zaidi ya  shilingi Bilioni 5.9 hadi kukamilika kwake.
Anasema hata hivyo gharama hizo zimeongezeka (hakueleza ongezeko) kutokana na mabadiliko ya thamani ya vifaa vilivyokadiriwa kununuliwa.
Anasema mradi huo ni utekelezaji kwa vitendo wa malengo halisi ya Mapinduzi matukufu ya 1964, sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa CCM ya 2015/2020 katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi pamoja na kuvijengea uwezo vikosi vya Idara maalum za SMZ.
Amebainisha kuwa mradi huo una  maeneo makuu manne (4), ambayo ni Ujenzi wa vituo vya Uzamiaji na Uokozi pamoja na Ununuzi wa Boti za uokozi na vifaa vya uzamiaji.
Maeneo mengine ni Ununuzi wa vifaa vya mawasiliano, pamoja na kuwapatia mafunzo Maofisa, wapinagaji wa kikosi cha KMKM pamoja na wananchi kwa ujumla.
Katibu Mkuu huyo anasema, malengo makuu ya mradi huo ni kujenga vituo sita (6) vya uokozi na uzamiaji nchini kote, na kubainisha kuwa tayari mradi umeshakamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) ambavyo ni Kibweni na Nungwi kwa Unguja, pamoja na Mkoani Kisiwani Pemba.
"Vituo vitatu ambavyo ni Kizimkazi, Wete na Msuka vitajengwa sambamba na ujenzi wa mahanga (makaazi) ya askari kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020", anasema.
Ameongeza kwa kusema kuwa ujenzi wa vituo vilivyokamilika umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 966.8.
Anaeleza kuwa mradi huo umelenga kununua Boti mbili za Uokozi ambazo tayari zimeshanunuliwa, ikiwemo iliyozinduliwa, wakati nyingine iliyobaki ikitarajiwa kuwasili nchini mwishoni mwa mwezi huu.
Akielezea uwezo wa Boti hizo; Radhia anasema, "boti hizi zina uwezo wa kukimbia 'knotical mile 55' kwa saa ikiwa ni sawa na kilomita 99", anaeleza.
Anasema Boti hizo zina vifaa maalum vyenye uwezo wa kuokoa maisha ya hadi watu 400 kwa boti ndogo na watu 600 kwa boti kubwa; kwa wakati mmoja.
Anafafanua kwa kusema kuwa boti ndogo ina uwezo wa kubeba hadi watu 20, wakati ambapo boti kubwa ina uwezo wa kubeba hadi watu 40 na kuwakimbiza kituoni kwa ajili ya kupata huduma.

Anaeleza kuwa boti hizo zimegharimu jumla ya shilingi Bilioni 12.5.
Akigusia kuhusiana na vifaa vya uzamiaji, Radhia amesema  kuna vifaa mbali mbali ambavyo tayari vimenunuliwa, ikiwemo nguo maalum za uzamiaji, mitungi ya gesi, mashine ya kutengenezea gesi pamoja na vifaa vyengine vinavyotumika chini ya bahari wakati wa uokozi.
Anasema vifaa hivyo vimeigharimu Serikali jumla ya shilingi Milioni 500.
Aidha, anasema vifaa mbali mbali vya mawasiliano vilivyogharimu shilingi Milioni 470 vimenunuliwa, ikiwemo Mtambo wa Redio (redio base), Rada ya baharini (marine radar), kompyuta pamoja na vifaa vya GPS.
Anabainisha kuwa kupitia mradi huo, maofisa na wapiganaji 68 wa KMKM wamepatiwa mafunzo yaliogharimu shilingi  Milioni 30, kuhusiana na matumizi ya  vifaa hivyo.
"Pia wananchi 850 wanaofanya shughuli za uvuvi na wasafirishaji wadogo wadogo wa abiria na mizigo katika Mikoa mitano ya Zanzibar wamejengewa uelewa wa kuwepo mradi huu pamoja na kupatiwa mafunzo ya kutumia vifaa vya mawasiliano kwa ajili ya kutoa taarifa pale wanapohitaji msaada wakiwa baharini", anaongeza.
Anasema kuwa tayari miongoni mwa wananchi hao wameanza kuvitumia vituo hivyo pale wanapohitaji msaada.
Katika hatua nyengine, Katibu Mkuu Radhia ameweka wazi mipango ya Wizara ya kuvipatia vituo hivyo 'Drone' moja kati ya tatu zilizonunuliwa kupitia mradi wa Mji salama, ili kuimarisha ulinzi wa baharini kwa njia ya anga.
Aidha, anasema Kikosi cha KMKM kimenunua kifaa maalum (decompression chamber) kitakachotumika kusaidia wahanga watakaoathirika kutokana na mfumo wa kupumua pale wanapopatwa na majanga.
Anasema kuwa upatikanaji wa huduma hiyo utawasaidia sana wahanga kurejea katika hali yao ya kawaida.
Anaeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo, kutaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri wa baharini, katika suala zima la kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao, hususan wale wanaotumia bahari katika shughuli zao za kila siku. 
Katibu Mkuu huyo amechukua ahadi ya kuhakikisha kuwa wapiganaji wa KMKM watavilinda, kuvitunza na kuvitumia vizuri vifaa hivyo, ili  kuifanya sekta ya usafiri baharini kuwa katika hali ya usalama zaidi.
Haji Omar Kheir ni Waziri wa Nchi (OR), Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, anasema uzinduzi wa vituo hivyo unaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha shughuli zote za uokozi zinafanyika kwa weledi wa hali ya juu nakwa njia za kisasa zaidi ili kuleta ufanisi.
Anasema kupitia mradi huo Kikosi cha KMKM kitakuwa na uwezo mkubwa wa kiusalama na kuweza kukabiliana na majanga kwa wakati muafaka.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya uongozi thabiti wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa  kukiwezesha kikosi hicho kwa vifaa na mafunzo kwa watendaji wake.
Salim Hamad Khamis (65) mvuvi kutoka  Makombeni Mkoani ameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazoendelea kuchukuwa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama muda zote wakati wanapokuwa katika shughuli zao za kila siku baharini.
Anasema hatua ya  Serikali kununua boti za uokozi zenye uwezo na kasi kubwa, itawasaidia sana wananchi, ikiwemo wavuvi wadogo wadogo wawapo baharini katika shughuli zao za kila siku.
".........., hakika hili ni jambo la kushukuru sana, kumshukuru Mungu, kumshukuru Rais wetu kwa kuona umuhimu  wa kuwalinda na kuwanusuru na majanga wananchi wake, hasa sisi wavuvi wenye vidau vidogo, muda wote tumashakani, sasa tutakuwa na  amani na kazi zetu", anasema.
Anasema kuwepo kwa boti hizo, sambamba na mafunzo yanayoendelewa kutolewa kwa wananchi katika kukabiliana na majanga wawapo baharini, ni hatua muafaka na dhamira njema ya Serikali kwa wananachi wake katika kukabiliana na majanga.
Siti Awesu Hamad (30) ni maazi wa Makoongwe aliehudhuria kwenye hafla hiyo, anasema uzinduzi wa kituo cha uzamiaji na uokozi ni ukombozi kwa Wazanzibari, hususan wale wanaoendesha maisha yao kwa shughuli za baharini.
Anaiomba Serikali kuviwezesha ipasavyo vikosi vya SMZ ikiwemo KMKM ili viweze kutekeleza vyema majukumu yake, pamoja na kusimamia usalama wa baharini.
Ni dhahiri kuwa uzinduzi wa Kituo cha Uzamiaji na Uokozi Mkoani Pemba, kwa niaba ya vituo vyengine, ni mapinduzi mapya katika kuzikabili changamoto mbali mbali za baharini.
Kuna ukweli usio shaka kuwa sekta ya uvuvi  pamoja na ile ya mawasiliano baharini inabeba kundi kubwa la nguvu kazi ya Taifa pamoja na kuchangia uchumi wa taifa kwa kiwango kikubwa.
Kwa mantiki hiyo ni wazi kuwa hatua ya Serikali ya kuanzisha vituo hivyo, ni uthibitisho wa dhamira njema kwa wananchi wake katika kukabili majanga ambayo yamekuwa yakiongezeka kila kukicha.
Hivyo, ni jukumu la wananchi wote, hususan wale wanaofanya shughuli za baharini kuhamasishana ili kushiriki mafunzo yanayotolewa na watendaji wa vituo hivyo ili kufahamu namna gani wataweza kupata msaada pale wanapopatwa na majanga ya aina mbali mbali.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.