Habari za Punde

Watanzania wametakiwa kulinda amani na utunzaji wa mazingira kwa faida ya wanyamapori na kuongeza mapato ya nchi



Na Ahmed Mahmoud Arusha
Watanzania wametakiwa kulinda amani na kuhakikisha wanapiga Vita suala zima la ujangili ili kuweza kuongeza mapato ya utalii hapa nchini sanjari na kutunza mazingira na uhifadhi ili kuongeza mapato ya nchi.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi wa shirika la hifadhi za taifa (TANAPA) Allan Kijazi kwenye kongamano la kuombea amani nchi yetu sanjari na kutunza mazingira lililofanyika kwenye zawaiya kuu Qadiriya Raziqiya aljailaniya iliyopo Olmatejoo jijini hapa jana.

Amesema kuwa huwezi kujenga misingi ya kiuchumi na uhifadhi bila uwepo wa amani hivyo viongozi wa madhehebu ya dini nchini wanawajibu mkubwa wa kuhamasisha utunzaji wa mazingira na Amani kwani itasaidia kuongeza mapato kwenye sekta ya utalii hapa nchini

"Kwa kuona umuhimu wa kongamano hili ndio maana Kama shirika katika suala zima la kufanya ukijani na utunzaji wa mazingira kwa kupanda Mti utachangia milioni 10 na tutaendelea kila itakapo hitajika Mimi binafsi ntachingia million mbili kuweza kufanikisha kongamano hili"alisema Kijazi.

Aliongeza kuwa wakati nchi yetu kwa sasa inahitaji amani kubwa kwani sekta ya utalii na uhifadhi ndio inategemea uwepo wa amani kwa maendeleo ya taifa letu na viongozi wa madhehebu ya dini wanahitajika Sana kuhimiza amani na utunzaji wa mazingira sanjari na kupiga Vita suala zima la ujangili.

"Uhifadhi na sekta zima ya utalii hapa nchini inategemea uwepo wa amani na utunzaji wa mazingira sanjari na kupiga Vita ujangili hivyo kongamano hili limekuja wakati muafaka ili kuweza kuombea nchi amani hili litasaidia utalii wetu na uhifadhi"alisisitiza Kijazi.

Amesema kuwa juhudi za utunzaji wa mazingira hapa nchini ziende sambamba na Vita ya ujangili na viongozi wa dini wanaowajibu wa kuhamasisha utunzaji wa mazingira na uhifadhi ili kuweza kukuza sekta ya utalii hapa nchini.

Kwa upande wake mwenyekiti wa taifa wa zawiya kuu Qadiriya Raziqiya aljailaniya iliyopo Olmatejoo jijini hapa Sheikh Salim Mbaraka almaarufu Mti Mkavu amewataka watanzania bila kujali itikadi zao kote nchini wanawajibu wa kujenga mazoea ya kuvumiliana na kuheshimiana ili kutunza amani iliyopo sanjari na kuheshimu viongozi walipo madarakani.

Amesema kuwa ushirikiano uliopo kati ya taasisi za kidini hapa nchini uzidi kuimarishwa kwa misingi ya kujenga mshikamano na umoja kwa lengo zima la kudumisha amani hapa nchini.

"Nawasihi Sana watanzania kuhakikisha wanapiga Vita ujangili sanjari na kutunza amani ili isipotee kwa maendeleo ya taifa letu kwa kujenga mazoea ya kuvumiliana na kuheshimiana"alisisitiza sheikh Mti Mkavu.

Amesema kuwa huwezi kujenga tabia ya kuvumiliana na kuheshimiana bila kuwa na amani hivyo ndio maana taasisi yetu ikaona umuhimu wa kongamano hili kuombea amani nchi yetu liende sambamba na utunzaji wa mazingira kwenye mataifa yetu.

Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa mkoa wa zawiya kuu Qadiriya Raziqiya aljailaniya Khalifa Abdi Said amesema kuwa juhudi za utunzaji wa mazingira sanjari na kupiga Vita ujangili ndio nakuitakia Amani nchi yetu ndio kauli mbiu ya kongamano Hilo.

Amesema kuwa kongamano hilo la siku tatu lenye dhumuni la kuombea nchi yetu amani na utunzaji wa mazingira sanjari na kupiga Vita ujangili linashirikisha mataifa matatu kutoka nchi za Kenya Uganda na wenyeji Tanzania .

Amesema kuwa zawiya hiyo imeanza utunzaji wa mazingira kwenye kingo za mto Ngarenaro sanjari na upandaji wa miti lengo likiwa ni kuendelea kuweka Arusha na nchi kwa ujumla kwenye Hali ya kijani.

Akatanabaisha kuwa kongamano hilo limekuwa likifanyika kila mwaka ila la mwaka huu ni la kipekee kutokana na kuzishirikisha mataifa ya nje baada ya zawiya kuvuka.mipaka hivyo kuongeza wigo wake 

"Tumekuwa tukifanya ziara hizi kila mwaka ila ya mwaka huu ni ya kipekee kutokana na kuongeza wigo baada ya zawiya kusambaa Afrika mashariki hivyo hi itasaidia kupambana na.mazingira kwenye nchi zetu baada ya kutoka hapa"alisema Khalifa Abdi.

Kongamano hilo lenye kuombea amani nchi yetu na kupiga Vita ujangili sanjari na kutunza mazingira litadumu kwa siku tatu hivyo kuonyesha umuhimu wa kutunza amani yetu katika ukanda wetu wa jumuiya ya Afrika mashariki nakuongeza wigo wa maendeleo katika nchi zetu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.