Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Afanya Ziara Wilaya ya Mjini Unguja leo, Kutembelea Miradi ya Maendeleo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,akiweka jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Mnara wa Tangi la Maji Safi na Salama eneo la Mnara wa Mbao Kilimani Zanzibar, akiwa katika ziara yake Wilaya ya Mjini Unguja leo. 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein  amewaeleza wananchi wa Mkoa wa Mjini kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha inaukamilisha mradi wa maji safi na salama ili changamoto ya uhaba wa huduma hiyo iwe historia hapa Zanzibar.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatafuta kila njia katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma ya maji safi na salama katika Mji Mkongwe wa Zanzibar pamoja na maeneo ya Nambo ya Zamani.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo huko Saateni katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi Tangi la Maji Saateni ambapo mapema aliweka jiwe la msingi Tangi la Maji Mnara wa Mbao, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya kutembelea Mikoa yote ya Zanzibar atakayoihimisha Februari 25 mwaka huu.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa kila Awamu ya uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilijitahidi katika kutatua tatizo la maji na kila kiongozi alifanya wajibu wake juu ya kuwapatia wananchi huduma hiyo na hakuna aliyedharau.

Aliongeza kuwa katika uongozi wa Awamu ya Saba juhudi hizo ziliendelea na kufanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuanza kutafuta fedha, vifaa pamoja na wajenzi wa miradi na miundombinu ya maji.

Alieleza kuwa mradi huo wa maji ukikamila hali ya maji itakuwa ni bora kwani hizo zote ni juhudi za Serikali katika kuhakikishwa wananchi wa Zanzibar wanapata maji safi na salama.

Alisema kuwa Serikali inakwenda hatua kwa hatua na kuwasisitiza wananchi kuwa wastahamilivu kwani mradi huo utamalizika na utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi.

Rais Dk. Shein alisema kuwa juhudi za makusudi kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB ambapo iliikopesha Zanzibar Dola milioni 21,  Serikali ya Ras al khaimah imechimba visima 23, India imetoa kwa mkopo wa Dola milioni 92 pamoja na msaada kutoka Serikali ya Japan wa Dola milioni 100 kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo ya maji.

“Hakuna dhiki wa dhiki na badala yake baada ya dhiki faraji, hivyo wananchi endeleeni kustahamili Serikali yenu haikupuuzini msinune hakuna mtu anetaka wananchi mpate tabu na vizuri mjue kuwa hakuna mtu anaeweza kutatua tatizo hilo haraka haraka”,alisema Dk. Shein.

Rais Dk. Shein aliwataka wananchi kuachana na mambo mengi yanayosmwa na kunukuu maneno ya Rais Salmin Amour Juma kuwa jambo la muhimu ni kuhakikiisha wanashika mpini yaani wanashika Dola. “watasema mchana na usiku watalala ”,alisisitiza.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa yote yanaofanyika ni miongoni mwa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015-2020 ambayo mpaka hivi sasa tayari imeshatekelezwa kwa kiwango kikubwa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kutunza mazingira kwani miongoni mwa sababu za uhaba wa maji katika Mkoa wa Mjini kunatokana na uharibifu wa mazingira uliofanywa katika vianzio vya maji zikiwemo chemchem.

Nae Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati Salama Aboud Talib alieleza juhudi zinazochukuliwa katika kuhakikisha mradi huo unakamilika huku akitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa kutekeleza Ilani ya CCM ya katika kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Mjini wanapata maji safi na salama.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Zanzibar Mussa Ramadhani Haji alieleza kuwa alieleza kuwa Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Mkoa wa Mjini Magharibi (ZUWSP) unatekelezwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)  na utekelezaji wake ulianza mwaka 2013 na unatarajiwa kumalizika mwezi wa Disemba 2019.

Mradi huo unajumuisha uchimbaji wa visima vipya 6, ukarabati wa visima vikongwe 23, ujenzi wa Matangi 2 yenye ujazo wa lita Milioni mbili 2,000,000 Saateni na Milioni Moja 1,000,000 Mnara wa Mbao, ulazaji wa mabomba makubwa yenye urefu wa kilomita 20 kutoka Bumbwisudi hadi Welezo matangini pamoja na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 60 kutoam Welezo hadi kwa watumiaji.

Aidha, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa Mradi huo hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 23 sawa na TZS Bilioni 37.1   ambapo SMZ imetoa TZS Bilioni 3.8 na TZS Bilioni 33 zitatolewa kwa Mkopo kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB).

Wakati huo huo, Rais Dk. Shein ambaye pia, ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar  alikutana na wanachama na viongozi wa CCM wa Mkoa wa Mjini na kufanya nao mazungumzo katika ukumbi wa CCM Mkoa wa Mjini uliopo Amani ambapo katika mazungumzo yake alisisitiza suala zima la umoja na mshikamano.

Aidha, Rais Dk. Shein amewasisitiza wanaCCM pamoja na viongozi wa Chama hicho kuweka mazingira mazuri ya kushinda uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2020 kwa kufanya maandalizi mazuri.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar imekuwa ikitekeleza mambo yote yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi na yale ambayo hayamo kwenye Ilani hiyo lakini kutokana na umuhimu wake imekwua ikiyatekeleza kwa kiwango cha hali ya juu na kulea mfano ujenzi wa barabara katika eneo la Mwanakwereke, Kibondemzungu pamoja na ujenzi wa mitaro ya maji machafu katika mji wa Zanzibar.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliwataka wanaCCM kuwaepuka waongo ambao wamekuwa wakizusha mambo mbali mbali ambayo hayana msingi ikiwa ni pamoja na kuzua kuwa yeye na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Joseph Magufuli wana mpango wa kufanya kuwepo na Serikali moja tu ambayo ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.