Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza Wakati wa Majumuisho ya Ziara yake Wilaya ya Mjini Unguja leo.12-2-2019.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Wananchi na Viongozi wa Wilaya ya Mjini Unguja wakati wa majumuisho ya ziara yake katika Wilaya ya Mjini yaliofanyika katika ukumbi wa Kariakoo Zanzibar, jioni hii.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza suala zima la maadili kwa viongozi ikiwa ni pamoja na kujua wajibu wao na wanao waongoza.

Rais Dk. Shein aliyasema hayo leo katika Majumuisho ya ziara yake ya Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi yaliyofanyika katika ukumbi wa Kariakoo mjini Zanzibar ambapo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein.

Katika hotuba yake Rais Dk. Shein alieleza kuwa kiongozi anapaswa kuwa na maadili mazuri ili iwe rahisi katika utendaji wake wa kazi hatua ambayo itawasaidia mpaka wale anaowaongoza kutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa taarifa ya Wilaya ya Mjini pamoja na kuwapongeza Mkuu wa Mkoa huo pamoja na Mkuu wa Wilaya wake kwa juhudi wanazozichukuwa katika Wilaya hiyo na kusema kuwa Wilaya hiyo inakwenda vizuri.

Akieleza miongoni mwa changamoto zilizomo katika Wilaya ya Mjini ni pamoja na ongezeko kuwa la watu katika Wilaya hiyo ambapo idadi ya watu wake ni sawa na idadi ya watu wa Zanzibar mnamo mwaka 1964.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza changamoto ya ukosefu wa ajira hapa Zanzibar na kueleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali licha ya wanaohitaji ajira kuwa wengi.

Rais Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa matangi ya maji ambayo hayajawahi kujengwa katika nchi yoyote katika Bara la Afrika yatakuwa ni ya kihistoria kwa Zanzibar kwani yataondosha changamoto ya maji kwani ni mradi wa uhai wa wananchi wa Zanzibar.


Aliwanasihi viongozi wa Wilaya ya Mjini kuendelea kufanya kazi kwa pamoja kwa kushauriana ili wazidi kupata mafanikio katika shughuli zao za kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema kuwa Zanzibar itaendelea kupambana na umasikini wake kwa hali na mali na haitokuwa tayari kuyumbishwa.

Alieleza mafanikio ya ziara zake ikiwemo ile aliyoifanya katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo hivi karibuni ulikuja ujumbe wa Khalifa Fund kutoka Abudhabi ambao umeahidi kutoa fedha za kwa ajili ya vijana ili waweze kujiajiri wenyewe ambapo fedha hizo ziko njiani, na kusisitiza kuwa vijana kamwe hawatotupwa.

Alieleza kuwa kwa upande wa Indonesia tayari washakubaliani na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika zao la mwani na matarajio yake kuwa akina mama wanaolima zao hilo watafaidika kwani  utakuwa na bei nzuri kwani hatua hiyo pia itanyajua sekta ya ajira.

Alieleza jitihada zitafanywa ili kuhakikisha vijana wanapata ajira, na kueleza kuwa  hilo halitofanikiwa ikiwa hakuna maadili, kwani maadili ni suala muhimu.

Aidha, alisisitiza suala zima la kupambana na rushwa na kuwatanabaisha viongozi kuwa wasije kuteleza na kuingia katika balaa hilo.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Rais Dk. Shein alisema kuwa kuna jambo baya sana limeibuka la kughushi mitihani jambo ambalo ni baya sana na kuutaka uongozi wa Wilaya kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kupambana na jambo hilo.

Alisema kuwa tayari ameshaagiza kutafutwa watu ambao wanawaharibia watoto masomo yao na kuutaka uongozi wa Wilaya zote kushirikiana na Wizara hiyo ya Elimu katika kupambana na janga hilo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeahidi kutoa vifaa bure na kueleza kuwa tayari baadhi ya vifaa vimeshaanza kutolewa bure maskulini  yakiwemo mabuku huku akisisitiza kuwa hata huduma za afya zimekuwa zikitolewa bure hapa Zanzibar kwani hayo ndio malengo ya Mapinduzi chini ya uongozi wa Marehemu Mzee Karume.

Alieleza kuwa kuwepo kwa amani na utulivu hapa Zanzibar kumeweza kuwavutia wageni kutoka nchi mbali mbali duniani kuja kuitembelea Zanzibar na kusisitiza haja ya kulindwa na kuenziwa ili Zanzibar izidi kupata mafanikio ikiwemo kuongezeka kwa watalii.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuutaka uongozi wa Wizalaya ya Mjini ambao bado unaendelea kukodi nyumba ya Ofisi kwa ghara za TZS Milioni 4.8 kwa mwezi, kuharakisha kujenga jengo lao ili kuepuka matumizi hayo ya makubwa ya fedha.

Kwa upande wa miradi katika Wilaya ya Mjini, Rais Dk. Shein alisema kuwa tayari miradi 13 imekamilika na miradi 14 imo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na 9 kati ya hiyo bado haijaaza ikiwemo barabara ya Shauri Moyo hadi Mboriborini na kutaka kuhakikisha miradi hiyo inafanyiwa kazi.

Alisema kuwa wakati Serikali ikitekeleza kujenga mtaro mkubwa wa maji ameshtuka na baadhi ya wananchi kutoa lawama zisizo na msingi na kuwataka viongozi wa Mkoa na Wilaya kutoa elimu kwa wananchi juu ya miradi ya maendeleo ili wawache kulaumu.

Alisema kuwa Serikali inafanya kazi kwa ajili ya wananchi hivyo, aliwataka wasiwe mbali na wananchi ili wawape elimu juu ya miradi yao.

 Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Kheir alieleza mikakati iliyowekwa na Serikali katika kuendeleza suala zima la Ugatuzi.

Akitoa neno la shukurani, Mkuu wa Mkoa Mjini Mgharibi Ayoub Mohammed Mahmoud alimuhakikishia Dk. Shein kuwa watakahikisha suala zima la maadili linafayiwa kazi katika Wilaya hiyo kuanzia ngazi zote zikiwemo Shehia, Wilaya hadi Mkoa na kuahidi kutekeleza dhamira hiyo ya Dk. Shein.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema kuwa na wale wote ambao watakwenda kinyume na maadili  taratibu na hatua za kisheria zinafuatwa.

Alieleza mikakati iliyowekwa na Mkoa wake kupitia Wilaya zake ikiwa ni pamoja na kujifunza kwa ajili ya kuendeleza Manispaa zake.

Alieleza kuwa Ofisi yake inadhamiria katika Bajeti ijayo ya mwaka 2019-2020 kama fedha zitakuwepo basi Manispaa zao ziweze kuchangia asilimia 5 badala ya asilimia 2, ambapo katika mgao asilimia 2 zisaidie vijana asilimia 2 zisaidie akina mama na asilimia moja isaidie makundi maalum.

Alisisitiza kuwa mambo yote yaliyokuwa kinyumme na tamaduni za Kizanzibari yatafanyiwa  kazi katika kuyatokomeza na kueleza kuwa wanachukua maelekezo ya kutoa elimu ya miradi na dhamira ya Serikali kwa ajili ya miradi hiyo na kuwaeleza Sera za nchi hii sasa ni maendeleo kwa wananchi.

Ayoub alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuiwezesha kinyenzo Wilaya hiyo katika suala zima la ulinzi wa kisasa, na kueleza haja ya kuenezwa vifaa hivyo katika maeneo mengine ya mjini kwani imethibitika kwamba vifaa hivyo vinasaidia kwa kiasi kikubwa kuwakamata wahalifu.

Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.