Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Azungumza na Wananchi na Kuweka Jiwe la Msingi Kituo Cha Afya Kianga.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi Kituo Cha Afya Kianga kilichojengwa  kwa Mradi wa TASAF na Nguvu za Wananchi wa Shehia ya Kianga, akiwa katika ziara yake Wilaya ya Magharibi A Unguja, kutembelea Miradi ya Maendeleo ya Wilaya hiyo.

Na.Abdi Shamnah -Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi wa shehiya ya Kianga, Wilaya Magharibi 'A'Unguja kukitunza vyema pamoja na kukitumia ipasavyo kituo cha Afya, ili kiweze kuwa endelevu na kuleta tija kwa jamii.
Dk. Shein amesema hayo leo katika hafla ya Uwekaji wa Jiwe la msingi la Kituo cha Afya Kianga, kilichojengwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa mashirikiano na wananchi.
Alisema suala la upatikanaji wa huduma bora za Afya nchini halina mbadala, hivyo kuna haja ya kukitunza kituo hicho na kuhakikisha wananchi wa shehiya hiyo na nyengine jirani wanafika kupata huduma.
Alisema pamoja na wananchi kuendelea na tamaduni za kupata huduma za afya kupitia njia za jadi, kuna umuhimu mkubwa wa kukitumia ipasavyo kituo hicho, ambacho kitaendeshwa kupitia afya ya msingi chini ya mfumo wa Ugatuzi.
"Sisemi yale ya asili msifanye, sijasema hivyo yale fanyeni lakini pia hospitalini mje, sitaki kuondosha imani za watu", alisema.
Aidha Dk. Shein aliiagiza Wizara Afya kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya Magharibi "A" kuhakikisha kituo hicho kinakuwa katika mazingira bora, ikiwa pamoja na kukipatia wataalamu wa kukihudumia.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananachi wa Kianga kwa uamuzi wao uliolenga kupatiwa huduma za afya, ili kuondokana na kadhia ya muda mrefu ya kufuata huduma hizo katika vituo vya afya vilivyopo masafa marefu.
Akigusia historia ya huduma za Afya nchini, Dk. Shein alisema Mapinduzi ya mwaka 1964 yamekuja kuwakomboa Wazanzibari wanyonge kuondokana na kadhia ya kukosa huduma bora za afya.
Alisema kabla ya Mapinduzi, huduma za Afya (kama ilivyo kwa elimu), zilitolewa kwa misingi ya ubaguzi kuambatana na uwezo wa mtu, hivyo Wazanzibari walio wengi walikosa huduma hiyo muhimu.
Katika hatua nyengine Dk. Shein aliwapongeza watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Zanzibar, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais  pamoja na wananchi wote waliofanikisha ujenzi wa kituo hicho.
 Mapema, Waziri wa Nchi, (OR), Tawala la Mikoa na Serikali za Mitaaa na Idara Maalum za SMZ,Mhe.Haji Omar Kheir alipongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli za kuimarisha mfuko huo kifedha kupitia Benki ya Dunia (World Bank).
Alisema ni haki ya wana CCM kuendelea kutembea kifua mbele, kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana katika  utekelezaji wa Ilani ya CCM, kupitia sekta tofauti ikiwemo Afya.
Waziri Kheri, aliahidi kushirikiana kikamilifu na Wizara ya Afya na kuandaa mikakati  ili  kupata wataalamu bora wa kukiendeleza kituo hicho.
Nae, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Mhe.Mihayo Juma Nhunga, alisema kukamilika kwa ujenzi huo kutawaondolea usumbufu wananchi wa Kianga kufuta huduma za Afya katika vituo vya Kizimbani na Bumbwi sudi na Mwera.
Alisema hatua hiyo itafungua milango ya maendeleo kwa wananchi wote wa Jimbo la Mwera.
Aidha, Naibu Katibu Mkuu, (WN) Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Ndg.Abdalla Hassan Witawi, alisema ujenzi wa kituo hicho ulioanza Julai, 2018 umegharimu zaidi ya shilingi Milioni 104 hadi sasa, ukifikia asilimia 85 ya ujenzi wote.
Mitawi alizipongeza Ofisi za Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Unguja na Wilaya Magharibi 'A' pamoja na Kamati ya Uongozi wa Shehiya ya Kianga kwa mashirkiano yao yaliofanikisha vyema ujenzi wa kituo hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.