Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, Aweka Jiwe la Msingi Kituo Cha Kukaushia Dagaa Kihinani Wilaya ya Magharibi A Unguja leo Akiwa Katika Ziara Yake.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuweka jiwe la Msingi la Kituo cha Kukaushia Dagaa cha Ushirika wa Tusiyumbishane Kihanani Unguja, akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ.Mhe. Haji Omar Kheri, wakati akiendelea na ziara yake katika Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo.
Na.Abdi Shamnah. Ikulu Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein aliendelea na ziara yake kwa uzinduzi wa kituo cha kukaushia Dagaa, huko Kihinani.
Akizungumza na wananchi na wajasiriamali baada ya kukaguwa mashine ya kukaushia dagaa, Dk. Shein aliwataka wajasiriamali hao kuendelea na shughuli zao na kuuza bidhaa zilizo bora ndani na nje ya nchi bila ya woga.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na bahari yenye rasilimali kadhaa, hivyo ni vyema ikatumika katika kuwakomboa wananachi kuoka katika lindi la umasikini, akiwashauri kuuza bidhaa hizo hadi Kongo na Malawi ambako soko kubwa hupatikana.
Aliitaka Wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi, kubuni njia bora zaidi ili kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara wa dagaa waweze kutumia mbinu bora za ukaushaji ili waweze kuzalisha bidhaa bora na kukidhi soko la nje ya nchi.
Aidha, Dk. Shein aliwataka wajasiriamali hao kuwa makini katika matumizi ya mashine hiyo wakati wa ukaushaji ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza na kuharibu ubora wa bidhaa zao.
Alisema serikali inaendelea na juhudi za kuimarisha sekta ya uvuvi kwa kununua meli mbili mpya, sambamba na kulifufua shirika la ZAFICO , azma inayokwenda sambamba na ujenzi wa viwanda vya Mwani, kwa mashirkiano na washirika wa maendeleo.
Dk Shein, aliwapongeza wananchi hao kwa utulivu na usikivu wao wa kukubali kuhama katika eneo la Maruhubi walipokuwa wakiendesha shughuli hizo na kuhamia Kihinani.
Mapema, Waziri wa Nchi (OR) Tawala na Mikoa, Serikali za Mitaa na Vikosi vya SMZ, Haji Omar Kheir aliwapongeza wajasiriamali kwa kukubali agizo la Serikali la kuondoka Maruhubi na kuhamia Kihinani, kwa hiari.
Alisema Serikali haina lengo la kuwaonea wananchi wake, akibainisha kuwa utekelezaji huo unakwenda sambamba na Ilani ya CCM katika kuwawezesha wananchi kiuchumi.
"CCM daima itaendelea kuwajali watu wake na kuwa mtetezi wa wanyonge wa nchi hii", alisema.
Alisema imelenga kuliendeleza eneo hilo kwa kufanikisha utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya kisasa, hatua itakayochangia ustawi mkubwa uchumi wa Taifa.
Nae, Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Magharibi 'A' Amou Ali Mussa alisema Bara hizo limetumia zaidi ya Shilingi Milioni 17.1 kwa ajili ya  kulipa fidia wananchi waliokuwa wakilitumia eneo hilo la Kihinani.
Alisema tayari wajasiriamali hao wameanzisha kikundi cha Ushirika ili kuwa na ngvu ya pamoja katika uendelezaji wa biashara zao, ambapo miongoni mwa changamoto zinazokabili ni ukosefu wa barabara za ndani.
Alisema bado Baraza la Manispaa linadaiwa kiasi cha shilingi Milioni 34, kukamilisha deni la fidia za wananchi.
Aidha, alisema kuna changamoto ya ufinyu wa nafasi kwa ajili ya wafanyabiashara, ambapo eneo la eka 1.3 limeazimwa kutoka Chuo cha Mwalimu Nyerere na hivi sasa linahitajika kwa matumizi ya chuo hicho.
Alisema kiasi cha wananchi 1,396 wananufaika kwa kuendesha shughuli za ujasiriamali mahali hapo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.