Habari za Punde

Mwenyekiti wa UWT awataka akinamama Zanzibar kuzidisha mashirikiano

Na Mwashungi Tahir        Maelezo Zanzibar      
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake UWT Taifa Gaudensia Kabaka  amewataka akinamama wa Zanzibar kuzidisha mashirikiyano ili kukikuza Chama cha Mapinduzi pamoja na jumuiya zake kwa lengo la kuleta ushindi ifikapo 2020.
Hayo ameyasema leo huko katika wilaya ya Dimani Magharibi B Tawi la Kiembesamaki  wakati alipokuwa kwenye ziara yake ya kukagua kazi za jumuiya za akinamama  na kutoa shukurani kwa kuchaguliwa pamoja na kupeana mawazo katika uimarishaji wa  Chama na jumuiya zake.
Amesema iwapo  watazidisha mashirikiano katika kuimarisha jumuiya pamoja na chama ushindi utapatikana tena na kwa kishindo kwani akinamama ndio wanaobeba jumuiya na chama cha Mapinduzi kwa kupiga kura nyingi.
“Kinamama tusirudi nyuma tusonge mbele kwa kuimarisha jumuiya zetu pamoja na Chama chetu cha CCM ili tuweze kushinda kwa kishindo ifikapo 2020” ,alisema Mwenyekiti Kabaka.
Amewataka akinamama kuvunja makundi na kuwa kitu kimoja kwani uchaguzi unakaribia , kuweka vikao vya halali katika  chama kwani vikao ndio uhai wa chama na jumuiya zake kwa lengo la kujadili mambo ya maendeleo  na pia kuhimiza  ulipaji wa ada kwa kadi za Chama cha Mapinduzi na Jumuiya zake.
“Makundi yavunjwe karibu uchaguzi tusibaguane sote tuwe kitu kimoja katika kuimarisha chama, walonuna wafunguke  kwni siasa ni demokrasi”alisisitiza mama Kabaka.

Pia amewaomba vikundi vya wajasiriamali waendelee katika kufanya kazi zao na kujipatia riziki za halali na kuendeleza maisha yao na familia zao na kuacha utegemezi kwa akina baba pamoja na kupinga vitendo vya udhalilishaji.
Nae Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Taifa Queen Mlozi amewahimiza akinamama kuwalea vizuri watoto wa kike kwa kuwapatia elimu ili wawe wataalamu wazuri katika Taifa na ndoto zao ziweze kutimia walizojiwekea hapo baadae.
Alihimiza mashirikiano kwa pamoja baba na mama katika kumleya mtoto wa kike asome kwa bidii ili aweze kuwa kiongozi bora kwa jamii na kuondosha ndoa za utotoni kwani zinarudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike.
Kwa upande wa Kaimu Katibu wa wilaya ya DimaniFatma Ramadhani Mandoba akitoa taarifa fupi juu ya wilaya hiyo amesema hali ya siasa iko vizuri , umoja wa wanawake UWT wana mashirikiano mazuri katika utendaji wa kazi zao.
Aidha alisema kwa upande wa mafanikio katika miaka 42 ya chama cha Mapinduzi wameweza kuingiza wanachama wa UWT 500 hiyo ni faraja kubwa katika wilaya hiyo.
Pia alisema uongozi wa UWT Wilaya ya Dimani wanahimiza kwa kila aliyefikia umri wa miaka 18 anapatiwa kitambulisho cha Mzanzibar.
Ziara hiyo inayofanywa Unguja imeanzia katika wilaya ya magharibi B kwa kutembelea katika kanisa la  la mtakatifu yohana Mbweni, Wilaya ya Dimani magharibi B, Zapha plus Welezo  Na kumalizia  Wilaya ya Mfenesini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.