Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk.Ali Mohamed Shein, Azungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia.Ikulu Zanzibar.

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Zambai Mhe. Hassan Simba Yahya alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchini Zambia Mhe. Hassan Simba Yahya alipofika Ikulu Zanzibar kuonana na kufanya mazunguzo na Rais leo.


RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza haja ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia.

Dk. Shein aliyasema hayo leo, Ikulu mjini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia Hassan Simba Yahya ambapo mazungumzo hayo yalijikita zaidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi Hassan Simba kuwa historia iliopo kati ya pande mbili hizo ni vyema  ikaimarishwa kwa kuendeleza sekta za kiuchumi na maendeleo hasa katika kutekeza Sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo azma ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza Sera ya Diplomasia ya uchumi ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uwekezaji hasa katika sekta ya viwanda kwani ndio kiu ya uchumi wa Tanzania hivi sasa.

Alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia zimekuwa zikishirikiana katika nyanja mbali mbali hasa ikizingatiwa kuwa nchi mbili hizo ni wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Bara la Afrika (SADC).

Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa vile Tanzania hivi sasa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, ni vyema mkazo zaidi ukawekwa katika kuhakikisha mashirikiano ya nchi wanachama wa Jumuiyahiyo yanaimarika zaidi kwa azma ya kufikia malengo yaliyowekwa.

Aidha, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umesababisha watu wa pande mbili hizo kuishi kama ndugu hasa kwa kuwepo kwa mradi mkubwa wa usafiri wa Shirika la Reli ya pamoja kati ya Zambia na Tanzania (TAZARA).

Dk. Shein alieleza kuwa  uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zambia na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni njia moja ya kuimarika zaidi kwa mahusiano ya wananchi wa pande mbili hizo hasa ikizingatiwa kuwepo kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kuwepo kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kati ya Tanzania na Zambia itakuwa chachu katikia kuimarisha uhusiano na ushirikiano kwenye sekta ya utalii.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alimtakia kazi njema Balozi huyo na kumueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kumpa mashirikiano makubwa katika kuhakikisha anatekeleza vyema kazi zake sambamba na kuiwakilisha vyema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia.

Akieleza kuhusu mashirikiano katika sekta ya elimu, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya  kuimarisha uhusiano kati ya vyuo vikuu vya nchi hiyo na vile vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vikiwemo vyuo vikuu vya Zanzibar.

Alieleza kuwa katika kuendeleza jambo hilo tayari wapo wanafunzi wanaotoka nchini Zambia ambao wanaosoma katika vyuo vikuu mbali mbali vya hapa Tanzania vikiwemo vyuo vikuu vya Zanzibar hatua ambayo inafaa kuendelezwa kwa kuwahamasisha wanafunzi kutoka pande zote mbili.

Nae Balozi mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Zambia  Hassan Simba Yahya alimueleza Dk. Shein kuwa suala la mashirikiano lina umuhimu mkubwa hivyo aliahidi kulifanyia kazi kwa nguvu zake zote.

Balozi Simba alitumia fursa hiyo kumuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa suala zima la kuendeleza historia ilioyopo katika kukuza uhusiano na ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia ataendelea kulipa kipaumbele katika kutekeleza majukumu yake nchini humo.

Alieleza kuwa historia iliyopo itaendelezwa sambamba na mahusiano mema ya wananchi pamoja na viongozi wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania na Zambia.

Balozi Simba alieleza kuwa utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi ambayo Tanzania kwa hivi sasa imeipa kipaumbele atahakikisha anaifanyia kazi kwa kuitangaza vyema ili kuhakikisha malengo yaliowekwa yanafikiwa.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.