Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein.Aipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania Kwa Ushindi Wao Kuingia Katika Michuano ya Fainali ya Kombe la Mataifa la Afrika AFCON.RAIS  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa ushindi mnono ulioipata dhidi ya Timu ya Taifa ya Uganda.

Dk. Shein alitatoa pongezi hizo baada ya Timu ya Taifa ya Tanzania kushinda mabao matatu kwa bila dhindi ya Timu ya Taifa ya Uganda mechi iliyochezwa katika uwanja wa Taifa Jijini Dar-es-Salaam hapo jana.

Rais Dk. Shein aliipongeza Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kwa kuweza  kufuzu katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya pili baada ya kusubiri kwa miaka 39.

Katika salamu zake hizo za pongezi Rais Dk. Shein aliipongeza Timu hiyo ya Tanzania kwa ushindi wake huo na kueleza kuwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima wamefarajika na ushindi huo ambao utaendelea kuipa hadhi kubwa Tanzania Kitaifa na Kimataifa katika anga za michezo.

Alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania nzima wataendelea kuiunga mkono Timu yao hiyo kutokana na jitihada kubwa inazozichukua katika kuhakikisha inailetea ushindi Tanzania.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwapongeza wananchi wote kwa kuishangiria timu yao hiyo katika mechi yake hiyo iliyocheza hapo jana sambamba na kuiunga mkono katika kuhakikisha inapata ushindi mnono.
Aidha, Dk. Shein amekipongeza Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Kocha  wake Mkuu Mnigeria Emmanuael Amunike pamoja na watendaji na viongozi wote waliofanikisha ushindi huo kwa kuonesha kiwango cha hali ya juu na hatiame kupata ushindi huo mnono uliwapa raha Watanzania wote.  
 Mara ya mwisho timu hiyo maarufu kama (Taifa Stars) kufika katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ilikuwa 1980 ambapo timu hiyo imefuzu katika siku ya mwisho kabisa ya mchuano wa makundi hapo jana Jumaapili baada ya kuifunga Uganda 3-0.

Ushindi huo uliwafanya Star kufikisha alama 8 na kujikatia tiketi ya kwenda Misri baadae mwaka huu.

Katika mchezo mwengine wa kundi  L la (Taifa Stars), Cape Verde walitoka sare tasa na Lesotho, hivyo timu hizo kufikisha alama 5 na 6 mtawalia ambapo kwa matokeo hayo  Star imejiunga na vinara wa kundi hilo Uganda ambao walifuzu awali baada ya kufikisha alama 13.

Star walianza mchezo huo kwa kasi huku wakipata hamasa kutoka kwa mashabiki zaidi ya 60,000 walioujaza uwanja wa Taifa jijini Dar –es Salaam pamoja na mashabiki walioko nje ya uwanja kutoka Tanzania Bara na  Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.