Habari za Punde

Mbegu Aliyoipanda Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani

Na.Othman Khamis. OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mbegu aliyoipanda muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya Mwaka 1964 Marehemu Mzee Abeid Amani Karume ya kuheshimu haki za Binaadamu kwa kufanya Mageuzi makubwa ya Sera ya Magereza hivi sasa mmea wake umechipua vyema na kutoa matunda ya Demokrasia sahihi Nchini.
Alisema Tarehe 12 Januari 1972 Mzee Karume alitoa amri kwa Wafungwa wote waliokuwa kifungoni waachiliwe huru kwa lengo la kuvunjwa kwa Magereza na badala yake kuwekwa Chuo cha Mafunzo ambacho hadi sasa kipo kwa nia ya kumrekebisha tabia Mtu anayefungwa ili atokapo arejee kuwa na tabia inayokubalika katika Jamii.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akilifungua Kongamano la kumuenzi Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Marehemu Mzee Abeid  Amani Karume lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Alisema mageuzi aliyoyafanya Marehemu Mzee Karume yakiwa ya aina yake kufanyika Barani Afrika yamewezesha baadae kuundwa kwa Wizara inayoshughulikia Utawala Bora, Kuwepo kwa Sheria na Sera tofauti zinazolinda haki za Wazee, Wanawake na Watoto.
Balozi Seif alisema kulinda na kupigania Haki za Binaadamu ni suala ambalo Mzee Karume alilisimamia ipasavyo katika misingi ya kutetea wanyonge, aliyependa kusimamia Umoja, Uhuru na Usawa badala ya utengano, ubaguzi na unyanyasaji.
Alisema Falsafa aliyokuwa nayo Mzee Abeid Amani Karume wakati akipigania ukombozi ilikuwa inaelekeza Uhuru na Usawa na Uhuru na Umoja mambo ambayo mara baada ya Mapinduzi aliendelea kuyasimamiwa kwa nguvu zake zote na wakati wote wa uhai wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza wanakongamano hao kwamba mbinu alizokuwa akizitumia Marehemu Mzee Karume zilimsaidia kubadilisha muonekano wa Zanzibar kutoka kwenye umaskini wa kudhulumiwa na kuelekea kwenye maendeleo yakudumu kwa wote.
Alisema ujenzi wa Nyumba za Kisasa za Ghorofa maarufu nyumba za Maendeleo, ugawaji wa Eka Tatu Tatu, huduma za Kijamii za Afya na Elimu, Viwanja vya Michezo, ujenzi wa Bara bara za Kisasa alivisimamia katika azma ya kumuona Mwananchi wa Zanzibar anastawika Kimaendeleo.
Alieleza kwamba katika kipindi chake cha Uongozi Marehemu Mzee Karumne alionekana akitumia muda wake mwingi kutembelea miradi aliyoianzisha ili kuhakikisha kwamba inatekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Alisema Muasisi huyu wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 alikuwa Kiongozi mwenye muono wa mbali asiyeepuka ubinafsi na mchukiaji mkubwa wa rushwa ambapo kichwa chake mara zote kilikuwa na picha ya Zanzibar aitakayo yenye kustawi kwa neema zinazowanufaisha Wananchi wote bila ya kujali Kabila, Rangi, Dini au hitilafu za Kisiasa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kutokana na msimamo wa Mzee Karume, Wananchi hasa Viongozi wanapoamua mambo yenye maslahi mapana na Taifa wasikubali kuyumbishwa hata kama watakabiliwa na upinzani wa ndani au nje ya Taasisi au Taifa.
“ Jee leo sisi kama Viongozi, Watendaji wa Serikali na Sekta Binafsi tukoje? Tuko tayari kumuenzi Mzee Karume kwa fikra na vitendo katika mioyo Yetu? Aliuliza Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Viongozi pamoja na Wananchi wote endapo watafikia hatua ya kuzifuata nyazo za Muasisi huyo wa Mapinduzi ya Zanzibar  watakuwa wamemuenzi kikamilifu.
“ Maneno ya Baraza la Mapinduzi yaliyosisitiza busara na maazimio ya Marehemu Mzee Karume kuwepo na kuendelea kudumishwa milele yakizingatiwa kwa makini pamoja na kufanyiwa kazi yanatosha kubakia kuwa dira itakayotuongoza katika kumuenzi Kiongozi wetu” Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza na Kuwashukuru Waandaaji wa Mkusanyiko huo wakiwemo watoa mada kwa juhudi zao zitakazotoa faida kwa Wanakongamano kujifunza mambo na masuala mengi kutokana na Historia ya Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema Kongamano hilo la kumuenzi Marehemu Mzee Abeid Amani Karume liwe jibu la swali la vipi Jamii inaweza kumuenzi Muasisi huyo wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 ambae pia alikuwa Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akigusia masuala ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar yaliyozaa Muuungano huo yametoa fursa kwa Wazanzibari walio wengi kupanua wigo wa Maisha kwa kuendesha harakati zao za Kimaisha Tanzania Bara.
Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na Tanzania Bra kubarikiwa maeneo mengi ya Ardhi waliyoridhia kuyatumia pamoja na Ndugu zao wa Zanzibar katika uwekezaji wa miradi ya masuala ya Biashara.
Balozi Seif alifahamisha kwamba nusu ya Wazanzibari wanaokadiriwa kufikia zaidi ya Laki Saba hivi sasa wanaendesha Maisha yao upande wa pili wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania bila ya bughudha yoyote.
Mapema Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif  Mohamed alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanzia Mwaka huu imeamua kuziendeleza Kumbukumbu za Muasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar Maerehemu Mzee Abeid Amani Karume katika Juma zima hadi kilele cha siku yenyewe ya Tarehe 7Aprili.
Nd. Shaaban alisema Juma hili la Kumbukumbu ya Mzee Karume lilibeba mambo mbali mbali yenye mnasaba na masuala ya Historia ya Ukombozi wa Visiwa vya Zanzibar nba mtanzao wa baadae wa kustawisha Maisha bora ya Wananchi wake.
Alisema uwepo wa Makongamano yaliyoanzia Kisiwani Pemba na kumalizia Kisiwa cha Unguja yamelenga kutoa Historia halisi ya maisha ya Muasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Mwaka 1964 yaliyokwenda sambamba na vuguvugu la Mapinduzi yenyewe.
Katibu Mkuu Shaaban alifahamisha kwamba wapo baadhi ya Watu kwa makusudi wameamua kuendeleza tabia ya kupotosha Jamii ndani na nje ya Nchi ili kizazi kipya kishindwe kuelewa vyema maamuzi ya Waasisi wa Taifa hili ya kuanzisha vuguvugu la Mapinduzi ya Zanzibar katika kujikomboa kutoka katika makucha ya Kikoloni.
Kongamano hilo la Pili likitanguliwa na lile ya Pemba lilihusisha mada 4 kubwa zilizowasilishwa na Wahadhiri mahiri wa Visiwa vya Zanzibar ambazo ni pamoja na Wasifu wa Sheikh abeid Amani Karume na Mtazamo wa Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume katika kuikomboa Zanzibar.
Mada nyengine ni jitihada za Marehemu Sheikh Abeid Karume baada ya Ukombozi wa Visiwa vya Zanzibar pamoja na Elimu ya Uraia na Uzalendo kwa Vijana juu ya Ukombozi uliofanywa na Waasisi wa ASP chini ya Usimamizi wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.
Tarehe 7 Mwezi wa Aprili ya kila Mwaka imetengwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  kuwa siku maalum ya kumbukumbu ya kuenzi Kifo cha Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, ambae alikuwa Jemedari wa Mapindinduzi Matukufu ya Tarehe 12 Januari  Mwaka 1964 yaliyomng’oa Mkoloni katika Visiwa vya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.