Habari za Punde

Upandaji wa Minazi Kingo za Barabara Ili Zanzibar Irejee Katika Historia Yake ya Uzalishaji wa Zao la Nazi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akipanda Mche wa Mnazi katika Siku ya upandaji Miti Kitaifa katika Shamba la Serikali la Minazi Selemu Wilaya ya Magharibi “A”.
Balozi Seif  akiutilia Maji Maji Mche wa Mnazi mara baada ya kuupanda kwenye Kampeni ya Upandaji Miti Kitaifa huko eneo la Shamba la Serikali Selemu.
Kikundi cha Taifa cha Utamaduni kikitoa burdani ya ngoma ya Kibati katika hafla ya Kitaifa ya Upandaji Miti Kitaifa kwenye Shamba la Serikali Selemu Wilaya ya Magharibi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akihutubia kwenye hafla ya Kitaifa ya Upandaji Miti Kitaifa kwenye Shamba la Serikali Selemu Wilaya ya Magharibi.
Waziri wa Wizara ya Kilimo, Maliasini, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mmanga Mjengo Mjawiri akimkaribisha mgeni rasmi Balozi Seif kuhutubia umma uliohudhuria Kampeni ya upandaji Miti Kitaifa huko Selemu.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasini, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Juma Saadala akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya upandaji Minazi kwenye hafla ya Upandaji Miti Kitaifa Selemu.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Taasisi mbali mbali za Umma, Wananchi pamoja na Wakulima wakifuatilia hafla ya Upandaji Miti Kitaifa huko eneo la Shamba la Serikali Selemu.
Na.Othaman Khamis OMPR.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziagiza Manispaa na Halmashauri za Wilaya  Nchini kuiimarisha Vitalu kwa uzalishaji wa Miche ya Minazi sambamba na kusimamia Kampeni ya upandaji wa Minazi kwenye maeneo ya wazi ikiwemo kingo za bara bara na bustani ili Zanzibar irejee katika historia yake ya uzalishaji wa zao la Nazi.
Alisema Serikali itaendelea kutoa Miche ya Mikarafuu na Minazi bila ya malipo kwa utaratibu maalum ambapo Wananchi watapaswa kuomba kupitia kwa Shehia na Halmashauri husika na baadae maombi yao kupelekwa Wizara ya Kilimo kwa hatua za kupatia Miche hiyo.
Akizungumza  katika Siku ya upandaji Miti Kitaifa katika Shamba la Serikali la Minazi Selemu Wilaya ya Magharibi  “A” Balozi Seif alisema Zao la Nazi Nchini hivi sasa limepungua uzalishaji wake kwa miaka kadhaa za hatimae sasa bidhaa hiyo huagizwa kutoka Nchi jirani kwa baadhi ya wakati.
Alisema hali halisi iliyopo Nchini hivi sasa  inaonyesha mahitaji ya zao na Nazi ni makubwa jambo ambalo kamwe halilingani na kasi ya uzalishaji wa zao hilo muhimu kwa Uchumi wa Taifa.
Balozi Seif alisema kwa mujibu wa Ripoti ya Sensa ya Miti ya Mwaka  2013/ 2014 imekadiriwa uwepo wa Miti ya Minazi ipatayo Milioni 3.4 tofauti ya Minazi Milioni 5.7 iliyowahi kuwepo mnamo Mwaka 1993.
Alisema hali hiyo inatokana na kasi kubwa ya ukataji wa Minazi kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ikiwemo ujenzi wa bara bara, Makaazi, uchongaji wa Vitu vya Samani,  maeneo ya Kilimo pamoja matumizi mabaya ya misumeno ya Moto iliyokwisha pigwa marufu matumizi yake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba hakuna Mwananchi asiyeelewa umuhimu wa Nazi kwa maisha na Uchumi wa Taifa kwa kipindi kirefu kutokana na ilivyokuwa ikizalisha bidhaa za mbata, Mafuta ya Nazi na kazi nyengine zinazotokana na usumba kama vile Mazulia.
Alifahamisha kwamba kutokana na kupungua kwa idadi ya Minazi Nchini hali hiyo imepelekea kupanda kwa bei ya zao hilo pamoja na bidhaa zote zinazotokana na Minazi.
“ Asilimia 95% ya zao la Nazi huuzwa na kutumika katika masoko ya ndani ikiwemo Madafu, makuti, Mafuta ya Nazi, nishati, mbao na Kamba” Alisema Balozi Seif.
Alieleza kwamba hatua za makusudi zinastahiki kuchukuliwa kutokana na faida kubwa ya zao la Nazi ili kuhakikisha hadhi ya zao hilo inaimarika kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Balozi Seif alisema katika kuimarisha zao hilo Serikali imeweka Mkakati maalum ikiwemo Kampeni ya upandaji Minazi Kitaifa, kuandaa Mpango wa Miaka 10 wa kuendeleza Minazi pamoja na kutayarisha Sera na Sheria zinazosimamia Maendeleo ya zao la Nazi Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema inatia moyo kuona uzalishaji wa Miche ya Minazi hivi sasa umeongezeka mara dufu ikilinganishwa na Miaka Mitano iliyopita nyuma.
Aliwakumbusha Wataalamu wa Kilimo kujenga utamaduni wa kuwatembelea Wakulima Mashambani katika utaratibu wa kuwapatia Taaluma bora na sahihi ya upandaji Minazi Kitaalamu zaidi.
Balozi Seif alisema wapo Wakulima wengi Nchini waliojipangia utaratibu wa kupanda Miti ya Minazi kwenye mashamba yao lakini mingi hufifia na mengine kupotea kwa kukosa utaalamu wa uhakika.
Akitoa Taarifa ya Kitaalamu ya upandaji Minazi Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Maryam Juma Saadala alisema Miche Laki 200,000 ya Minazi itakuwa ikipandwa kila Mwaka katika Kampeni endelevu ya upandaji Miti ya Minazi.
Bibi Maryam alisema hatua hiyo inatokana na takwimu za uzalishaji wa Mbata na Mafuta ya Nazi kupungua hadi kufikia Tani 276 Mwaka 2002 kutoka Tani 1,684 za Mbata na Mafuta ya Nazi Mwaka 1984.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo tayari imeshatumia jumla ya Shilingi Milioni Thamanini kwa ajili ya uzalishaji wa Miche ya Minazi ili kufanikisha Kampeni hiyo ya upandaji Minazi Nchini.
Bibi Maryam Juma Saadala alieleza kwamba katika msimu huu wa 2018 – 2019 jumla ya Miche Milioni 4,520,850 tayari imeshaoteshwa katika Vitalu vya Serikali pamoja na Watu Binafsi.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo Zanzibar alizishukuru Halmashauri za Wilayapamoja na Watu Binafsi Nchini kwa kuendeleza Vitalu vya Miti mbali mbali hatua inayoonyesha kuunga mkono jitihada za Serikali za kulirejesha katika haiba yake zao la Nazi Nchini.
Mapema Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mh. Mmanga Mjengo Mjawiri alisema Wizara hiyo imepewa jukumu kubwa la kuwahudumia Wananchi katika Sekta ya Kilimo ambapo Watendaji wake wana dhima ya kujibu Hoja kutokana nachangamoto zinazowakabili Wakulima.
Mh. Mmanga alisema Utaalamu na Ubunifu wa Watendaji wa Sekta ya Kilimo ni suala muhimu linalohitajiwa na Wakulima wakati wote unaopaswa kutolewa kwa haraka katika kuwahudumia Wananchi wote wanaojishughulisha na Sekta hiyo muhimu.
Waziri wa Kilimo aliwataka Wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa Taarifa ya kuwafichua Watu wote wanaohifadhi Misumeno ya Moto Mitaani kwa matumizi mabaya yaliyopigwa marufuku na Serikali.
Alisema bado ipo Misumeno ipatayo Mia 500 ya Moto iliyo mikononi mwa Watu Mitaani ambayo kubakia kwake nje ya Taasisi husika ya Misitu ni hatari yenye kusababisha uadui kwa Taifa.
Ujumbe wa Mwaka huu wa Kampeni ya Upandaji na utunzaji wa Miti Nchini unaeleza “ Tupande na tuitunze Minazi kwa Maendeleo ya Viwanda na Uchumi wa Zanzibar”.
Ujumbe huo umezingatia umuhimu wa Miti kwa vile husaidia kwa kiasi kikubwa kuhifadhi Ardhi na Udongo, vyenzo vya Maji, chemchem, Mito na upatikanaji wa Mvua ambayo ni muhimu sana kwa Kilimo na Ustawi wa Jamii Nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.