Habari za Punde

Micheweni wahamasishwa kusafisha mazingira yanayowazunguka

Na Masanja Mabula-Pemba 25/05/2019.
KAMATI kiongozi za afya za shehia katika wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba zimetakiwa kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kusafisha  mazingira yanayowazunguka ikiwa ni pamoja na kuchimba vyoo na kuvitumia.
Akizindua  kamati Kiongozi  za afya za shehia ya Tumbe , Konde na Chamboni , kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri , Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo Omar Issa Kombo amesema serikali imeunda kamati hizo ni kusaidia kufikisha elimu kwa jamii , na kuwataka kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa lengo la kuleta ufanisi
Amesema moja ya jukumu la Kamati hizo ni kusimamia kushajiisha jamii kutumia njia sahihi kujikinga na maradhi ya mripuko.
Amesema kwamba kipindi hichi ni hatarini hivyo wajumbe wa kamati hizo wanapaswa kupitia kwenye maeneo yao kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira.
‘Ni jukumu la kamati hizi kuhakikisha mazingira yanayowazunguka yanakuwa safi ’alisema.
Mapema afisa uhamasishaji wa afya wilaya hiyo Suleiman Faki Haji ,amesema katika uteuzi wa kamati umezingatia makundi yote ndanai ya jamii.
Ameeleza kuwa kamati hizi zimewajumuisha watu wa  makundi yote ili kurahisisha kufikisha ujumbe wa jamii.
‘Uamuzi wa kufanya uteuzi na kujumuisha makundi yote ndani ya jamii ni kurahisisha jamii kuupata ujumbe kwani kila mmoja atawajibika kulingana na kundi lake, alifahamisha.
 Afisa wa afya wilaya hiyo Ali Rashid amesema wana mpango wa kuunda kamati kishehia .
 Wajumbe wa kamati hizo wameahidi kushirikiana na watendaji wa wizara ya afya kutoa elimu kwa wananchi ili mazingira yanayowazunguka yaendelee kuwa rafiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.