Habari za Punde

Ujumbe wa Benki ya Kiislam ya Amana Tanzania.

Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiislamu ya Amana Dr. Muhsin Salim Masoud Kushoto akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika na Uongozi wake kujitambulisha baada ya kufungua Tawi lao Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kati kati akielezea faraja yake kufuatia uamuzi wa Benki ya Kiislamui ya Amana kufungua Tawi lao Visiwani Zanzibar alipozangunza na Uongozi wa juu wa Benki hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiislamu ya Amana Dr. Muhsin Salim Masoud Kushoto akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi azma ya kuanzisha Tawi lao Visiwani Zanzibar.
Meneja wa Benki ya Amana Tawi la Zanzibar Bwana Nassor Ameir wa Pili kutoka Kulia akitoa ufafanuzi wa mikopo kwa Wanafunzi wanaosoma elimu ya juu mahali popote pale mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifahamishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Kiislamu ya Amana Dr. Muhsin Salim Masoud  taratibu za kutia saini fomu ya kujiunga na Akaunti ya Benki ya Kiislamu ya Amana mara baada ya kuzungumza na Uongozi wa Benki hiyo ulipofika kujitambulisha rasmi.




Na.Othman Khamis OMPR.
Uongozi wa Benki ya Amana ambao tayari umeshafungua Tawi lake Visiwani Zanzibar katika misingi ya Benki ya Kiislamu umejikita kutoa huduma kwa Wananchi mbali mbali ikilenga zaidi makundi mahsusi ya Wanawake na Vijana wenye vipato vya chini.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Dr. Muhsin Salim Masoud alitoa kauli hiyo akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Benki wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ulipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuingia Zanzibar kutoa huduma za Kibenki.
Hata hivyo Dr. Muhsin Salim Masoud alisema Benki hiyo vile vile iko wazi na huru kutoa huduma za Kibenki kwa Wananchi wa Dini na Madhehebu mengine katika masuala mbali mbali ikiwemo mikopo.
Alisema Uongozi wa Benki hiyo umefikia maamuzi ya kusogeza huduma zake Visiwani Zanzibar baada ya utafiti mkubwa iliyofanya na kubainisha uwepo wa umuhimu wa kuongeza huduma za Kibenki kutokana na kukuwa kwa harakati za Kiuchumi zinazotoa fursa kwa Watu kuhitaji kupata huduma hizo.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Benki ya Kiislamu ya Amana alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Tawi la Benki hiyo lililoanzishwa Zanzibar ni la Tisa na kufuatiwa na lile la Kumi liliopo Mkoani Dodoma  ambayo tayari yanafanya kazi Nchini Tanzania.
Dr. Muhsin alielezea faraja yake kutokana na ushirikiano mkubwa waliopata watendaji wa Benki hiyo wakati wa maandalizi ya ufunguzi wa Tawi lao Visiwani Zanzibar jambo ambalo limewarahisishia upatikanaji wa urahisi wa vibali na taratibu zote zinazohusika katika uanzishwaji wa huduma za Kibenki.
Naye Meneja wa Benki ya Amana Tawi la Zanzibar Bwana Nassor Ameir alisema Uongozi wa Benki hiyo tayari umeanzisha program Maalum ya kutoa mikopo kwa Wanafunzi fani mbali mbali wanaohitaji kupata taaluma katika vyuo vyovyote watakavyoamua kusoma iwe ndani au nje ya Nchi.
Meneja Nassor alisema hatua hiyo imezingatiwa na Uongozi huo katika muelekeo wa kuwapunguzia mzigo Wazazi hasa wale wenye mazingira magumu ya uwezo wa kuwasomesha Watoto wao sambamba na kusaidiana na Serikali Kuu katika kukabiliana na uhaba wa mikopo.
Alisema Vijana wengi ndani ya Visiwa vya Zanzibar hivi sasa wamekuwa na muamko mkubwa wa kitaaluma kasi ambayo Serikali, Taasisi na hata Jumuiya za Kiraia zina wajibu wa kuwaunga mkono Vijana hao.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kuongezeka kwa huduma za Kibenki ni jambo linaloendelea kutoa wigo mpana wa upatikanaji wa fursa mbali mbali za Kiuchumi.
Balozi Seif alisema kitendo cha Benki ya Amana kufungua Tawi lake Zanzibar kunamaanisha lengo la Taasisi hiyo ya Kifedha kuungana na Serikali katika kuwakwamua Wananchi na ukali wa Maisha kupitia Sera ya Serikali ya kuviwezesha Vikundi vya Wananchi kuendesha Miradi yao ya kujitegemea.
Alisema Uongozi wa Benki hiyo umeonyesha mwanga wa kuunga mkono dhana nzima ya Uwezeshaji hasa yale Makundi makubwa ya ya Wanawake na Vijana ambayo ndio nguvu kazi kubwa ya Taifa katika kuelekea kwenye maendeleo ya kudumu.
Katika kuunga mkono jitihada za Benki hiyo ya Kiislamu ya Amana kufungua Tawi lake Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif tayari amefungua Akaunti yake ndani ya Benki hiyo katika kuhamasisha Wananchi wengine kuitumia fursa hiyo adhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.