Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, akiondoa kipazia kuashiria kuweka Jiwe la Msingi la Majengo ya Ofisi za SMZ Kisiwani Pemba . Uzinduzi huo umefanyika leo.kulia Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdulwawa.
RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema
kuwa miongoni mwa malengo makuu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuona
kwamba watumishi wa umma wanafanya kazi zao wakiwa katika mazingira yaliyo bora
na salama zaidi.
Dk. Shein aliayasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa
Jengo la Ofisi za Serikali huko Gombani Chake Chake Pemba, Mkoa wa Kusini
Pemba, ambapo viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wananchi na
wafanyakazi walihudhuria.
Rais Dk. Shein alisema kuwa uzinduzi wa jengo hilo ni
miongoni mwa vielelezo muhimu vya utekelezaji wa lengo hilo kwani majengo ya
ofisi ndio mahali pa kufanyia kazi ambapo hutumia muda mwingi ambayo ni
theluthi moja ya siku nzima baada ya kutoka nyumbani.
Alieleza kuwa kuwa na mahala pazuri pa kufanyia kazi kunampelekea
mtendaji afanye kazi kwa furaha, umakini na kujiamini Zaidi na ndio maana
Serikali imeamua kujenga.
Aliongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo ni jitihada za Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia maamuzi ya Baraza la Mapinduzi ambapo hatua
yote hiyo ni kuwawwzesha wafanyakazi katika mazingira mazuri.
Alieleza kuwa ujenzi huo unatokana na baadhi ya ofisi
kuchakaa, nyengine hazina nafasi ya kutosha kwa ajili ya watumishi pamoja na
wananchi wanaofika kwa ajili ya kupatiwa huduma.
Hata hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa baadhi ya Wizara na
Taasisi nyengine za Serikali zililazimika kukodi nyumba kutokana na uhaba wa
majengo halisi ya kiofisi hali ambayo haipendezi hivyo Serikali itaendelea
kujenga majengo ya Ofisi Unguja na Pemba.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali imejenga ofisi hizo
ili kurahisisha utoaji wa huduma hivyo, kila mfanyakazi ahakikishe kwamba
anawajibika ipasavyo kulingana na dhamana na majukumu ya kazi aliyopangiwa.
Hivyo, aliwataka wafanyakazi wahakikishe wanatumia vizuri muda
wa kazi kwa kufanya mambo yanayopaswa kufanywa katika sehemu za kazi.
Alisema kuwa Serikali itaongeza mshahara kwa kima cha chini
na juupale mapato yatakapoongezeka kwa wafanyakazi kuzidi kujituma na kuendelea
kufanya kazi kwa ari, taratibu na nidhamu za kazi.
Alisisitiza wafanyakazi kufanya kazi kwa masaa manane ya
kazi kwa siku kwani hatua hiyo itaongeza ufanisi na kuongeza mapato huku
akisisitiza haja kwa wafanyakazi kutunza siri za kazi kwani nyenzo kubwa katika
Utawala Bora sambamba na kujiepusha na malumbano.
Aliongeza kuwa kuna haja ya kutafuta namna itakayowezesha
kudhibiti matumizi ya simu za mikononi wakati wa saa za kazi kwani kumekuwa na
malalamiko mengi kwa wananchi katika sehemu mbali mbali juu ya suala matumizi
mabaya ya simu.
“Wafanyakazi wanatumia muda mwingi kazini kuchati na
kuperuzi katika mitandao ya kijamii vile vile natoa indhari kwa wale wanaotega
kazi kwamba kuwepo kwa ofisi hizi ndani ya jengo moja kusichukuliwe kuwa ni
ukaribu wa marafiki kuonana kirahisi kwa ajili ya mazungumzo”,alisisitiza Dk.
Shein.
Aidha, Dk. Shein aliwahimiza viongozi na wafanyakazi wote
watakaotumia jengo hilo wahakikishe kwamba wanalitumia vizuri pamoja na vifaa
na miundombinu mengine ili viweze kudumu Zaidi.
Pia, alieleza kuwa ofisi hizo mpya zitaongeza ari na hamasa
ya wafanyakazi ili waweze kufikia malengo yaliyowekwa ya kutoa huduma bora
Zaidi kwa wananchi huku akisisitiza kuwa jengo hilo litasaidia hata zile
taasisi ambazo zimechakaa huku taratibu zikiandaliwa kujenga ofisi nyengine
Zaidi.
“Na zile taasisi ambazo hazina pa kukaa zitaletwa hapa hapa
huku Serikali ikiendelea kujenga majengo mapya”,alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji
wa miradi hiyo mikubwa ya maendeleo ni kielelezo cha juhudi za kuendeleza
fikra, falsafa na malemgo ya Mapinduzi ya mwaka 1964 kwa kuzingatia miongozo ya
viongozi na wazee waliotangulia.
Alisisitiza kwamba Waasisi wa Mapinduzi chini ya Marehemu
Mzee Abeid Amani Karume walihakikisha kwamba panakuwa na uwiano wa kasi ya maendeleo
baina ya Unguja na Pemba.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya
Saba na Awamu zote zilizotangulia zimekuwa zikiyaendeleza haya kwa kasi na ari
ile ile ya Kimapinduzi licha ya kwamba wapo wanayoyabeza.
Alisema kuwa kuimarika kwa uchumi kumeiwezesha Awamu hii
kuyafanya maslahi ya wafanyakazi yawe bora kwa mara nne pamoja na kuubadilisha
mshahara wa kima cha chini kwa asilimia mia moja.
Rais Dk. Shein alisema kuwa mambo yote yanayofanywa ikiwa
ni pamoja na ujenzi wa majengo hayo ni kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar Ibara
ya 10.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni za ndani za Zanzibar
za “Quality Building Contract” iliyojenga ofisi hizo pamoja na Kampuni ya
“ZANCON”iliyokuwa Mshauri elekezi na msimamizi wa ujenzi huo.
Nae Waziri wa Fedha na Mipango Mohamed Ramia Abdiwawa
alieleza kuwa juhudi hizo za ujenzi zinatokana na utekelezaji wa Ilani ya CCM
sambamba na azma ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 na kutoa pongezi kwa
Mawaziri wawili waliomtangulia ambao ni Omar Yussuf Mzee na Dk. Khalid Salim kwaa
kusimamia vyema mchakato wa ujenzi huo.
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa
alisema kuwa ujenzi wa jengo hilo lenye vyumba 145 umegharimu jumla ya TZS
Bilioni 13.6 ambazo ni fedha za mapato ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema kuwa miongoni mwa Wizara ambazo zina ofisi katika
majengo hayo ni sita kwa hivi sasa ambazo ni Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara
ya Katiba na Sheria, Wizara ya Kazi Uwezeshaji Wazee, Wanawake na Watoto, Ofisi
ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na
Nishati na Wizara ya Vijana, Utamaduni na Michezo.
Mapema baada ya kulizindua jingo hilo Rais Dk. Shein
alipata fursa ya kulitembelea jengo hilo katika Ofisi za Wizara zote ndani ya jengo
hilo na kupata maelezo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment