Habari za Punde

HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI IDDI ALIYOITOA KUAKHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA NNE WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI TAREHE 28 JUNI, 2019
Mheshimiwa Spika,
Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, mwingi wa Rehma kwa kutujaalia uhai na afya njema na kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na Nne wa Baraza la Tisa ulioanza tarehe 08 Mei, 2019 hadi leo tarehe 28 Juni, 2019 tunapouahirisha.

Mkutano ambao tumeweza kupokea na kujadili Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2019/2020, na jumla ya Wizara 15 ambazo bajeti zao zimewasilishwa, zimejadiliwa na kupitishwa makadirio yao ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.


Mheshimiwa Spika,
Aidha, Mswada wa Sheria ya Matumizi (Appropriate Bill) na Mswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) iliwasilishwa, kujadiliwa na kupitishwa katika Baraza lako Tukufu.  Kupitishwa kwa Miswada hiyo itaiwezesha Serikali kukamilisha taratibu za kisheria katika matumizi ya fedha pamoja na watendaji kuendelea kusimamia na kutekeleza matumizi hayo ya fedha za Serikali.  Pia, Baraza limepokea taarifa za Serikali zifuatazo:-

  • Taarifa ya Serikali kuhusu ripoti ya kuchunguza  majengo ya Skuli 19 za Sekondari Zanzibar.
  • Kauli ya Serikali juu ya Hoja ya Mjumbe kuhusu maombi ya wananchi wa Jumuiya ya Waendesha Boda Boda Zanzibar juu ya kupatiwa fursa ya kuendelea na kazi ya kusafirisha abiria ili kujipatia kipato.
  • Taarifa ya Serikali juu ya Hoja ya Mjumbe kuhusu maombi ya baadhi ya wananchi wa Unguja na Pemba kuhusu suala la usafiri wa meli baina ya Visiwa vya Unguja na Pemba.  Kauli zote hizo zilijadiliwa na kupitishwa.
  • Baraza pia limepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka wa fedha 2016/2017 ambayo itajadiliwa katika kikao kijacho. 
  • Mswada wa Sheria ya Kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa Pamoja na Mswada wa Sheria ya Utawala wa Baraza la Wawakilishi nayo imesomwa kwa mara ya kwanza.
Shughuli zote tulizojipangia katika Mkutano huu zimekamilika kwa wakati muafaka na kwa mafanikio makubwa.


Mheshimiwa Spika,
Kwa namna ya pekee, natoa pongezi zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wao mahiri na makini katika kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 pamoja na Serikali zetu hasa katika suala zima la kuimarisha maadili, kuondosha rushwa, ufisadi na utekelezaji wa sheria na taratibu za nchi yetu.


Mheshimiwa Spika, Aidha, nakupongeza wewe binafsi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza letu Tukufu, Naibu Spika, Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma Wenyeviti wote wa Baraza pamoja na Katibu wa Baraza na timu yake yote kwa usimamizi mzuri wa shughuli za Baraza letu Tukufu.  Chini ya uongozi wako wa busara na weledi tumeweza kujadiliana kwa uwazi na pale tulipotafautiana busara iliweza kutumika kusawazisha tofauti hizo.  Sina budi pia kuwashukuru na kuwapongeza Wajumbe wote wa Baraza lao Tukufu kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mashirikiano makubwa na kwa kauli moja, na kukifanya kikao hiki kumalizika kwa amani, utulivu na kwa usalama  pamoja na mafanikio makubwa.  Kufanya hivyo, Waheshimiwa Wajumbe niseme kuwa mmejijengea nyinyi wenyewe na Baraza letu Tukufu heshima kubwa mbele ya wananchi.  Ahsanteni sana.


Mheshimiwa Spika, katika Kikao hiki jumla ya maswali ya msingi 157 na maswali ya nyongeza ......... yaliulizwa na yalijibiwa kwa ufasaha na ufafanuzi wa kina na Waheshimiwa Mawaziri husika.  Maswali ambayo hayakuweza kujibiwa kwa sababu yalihitaji taarifa za ziada kama vile takwimu, ahadi zilitolewa maswali hayo kujibiwa kwa maandishi.

Mheshimiwa Spika,
Hivi punde tulikamilisha kazi ya Kikatiba ya kupitisha kwa vishindo bajeti yetu kwa mwaka ujao wa fedha 2019/2020.  Ambapo katika mwelekeo wetu wa bajeti hiyo kiuchumi inakadiriwa kufikia asilimia 7.8, mfumko wa bei unatarajiwa kudhibitiwa kwa kuendelea kuwa na kiwango cha tarakimu moja, mapato ya ndani kuongezeka kwa asilimia 24, kutoka TZS. 790.8 Bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/19 hadi TZS. 859 Bilioni kwa mwaka 2019/2020. Aidha, Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya mishahara kwa wafanyakazi wake wenye uzoefu pamoja na makundi mengine ambayo hayajanufaika na nyongeza za mishahara iliyopita.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi wa Kiongozi wetu mahiri, Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein itasimamia kikamilifu ahadi zake za utekelezaji wa vipaumbele vya Taifa kwa mwaka 2019/2020, ambavyo ni elimu bure hadi Sekondari, matibabu bure pamoja na dawa za lazima, ukamilishaji wa Mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume kwa kutumia fedha zetu wenyewe za ndani, kuanza kwa ujenzi wa bandari mpya ya Mpigaduri na kuanza kwa ujenzi wa hospitali mpya ya rufaa ya Binguni.


Mheshimiwa Spika, Hayawi hayawi, huwa! Na mstahamilivu siku zote hula mbivu, mtakumbuka kuwa tarehe 23 Oktoba, 2018 tulitiliana saini na Kampuni ya Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia ya Ras Al Khaimah (RAK GAS) ya kufanya utafiti juu ya uwepo wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Zanzibar.  Hatua hiyo ilimalizika ikafuata hatua ya kuzichambua data na viashiria vilivyopatikana. Zoezi hili lipo ukingoni kumalizika, na ifikapo mwezi Septemba mwaka huu matokeo ya utafiti huo yatakabidhiwa rasmi Serikalini na baadae kama alivyotoa ahadi Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kuwa matokeo hayo yatatangazwa kwa wananchi hadharani.    Nitoe wito kwa wananchi wote kuendelea kuwa wastahamilivu na wazidishe dua zao ili majibu ya utafiti huo yawe mazuri na Inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu yatakuwa mazuri kama tunavyoyatarajia.  Ameen.


Mheshimiwa Spika, napenda kuwaeleza wananchi kuwa Bandari ya mafuta ya Mangapwani nayo itajengwa katika mwaka mpya wa fedha, kukamilika kwake kutasaidia kuongeza uwezo wa kuipokea shehena kubwa ya mafuta kwa wakati mmoja na kuweza kusambaza mafuta kwa ufanisi ndani na nje ya nchi. Hivyo, tutaweza kuondosha kabisa tatizo la upungufu wa mafuta nchini na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya Serikali maradufu.


Mheshimiwa Spika, Yajayo Yanafurahisha, muda mfupi kutoka sasa meli mpya ya kisasa katika ukanda wetu huu ya kubeba mafuta MT Ukombozi itawasili na kukabidhiwa rasmi Serikalini.  Meli hiyo imenunuliwa kwa kutumia bajeti zetu za ndani.  Kuwasili kwa meli hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kujitosheleza katika usafirishaji wa mafuta na kupelekea kupunguza gharama za usafirishaji wa nishati hiyo.


Mheshimiwa Spika, ujenzi wa shule tatu za ghorofa zitakazokuwa na dakhalia zake pamoja na kuzipatia vifaa vyote vinavyohitajika vikiwemo vya maabara, maktaba na fanicha, zitajengwa mbili Unguja na Pemba moja.  Kwa upande wa Unguja zinatarajiwa kujengwa katika Mkoa wa Mjini Magharibi na Kaskazini Unguja na kwa Pemba itajengwa katika Mkoa wa Kaskazini.  Skuli hizo zitajengwa kupitia mkopo nafuu unaotolewa na BADEA.  Ujenzi huo utafanyika wakati ambapo skuli 9 zile za ghorofa zikiwa mbioni kuanza kuchukua wanafunzi mara tu baada ya kuwekwa fanicha na vifaa vya maabara.  Pia, Vyuo vitatu vya Elimu Mbadala navyo vitaanza kufanya kazi katika mwaka huu wa bajeti vitaanza kufanya kazi, vyuo hivyo ni vile vya Maruhubi, Makunduchi kwa Unguja na Daya kwa Pemba.


Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo yaliyozungumzwa kwa hamasa kubwa katika mkutano huu lilikuwa ni suala zima la ajira kwa vijana wetu.  Tumekusikieni Waheshimiwa, na Serikali imekuwa ikichukua hatua mbali mbali ili kuhakikisha vijana wetu wanakuwa na ajira, tunaujua ukubwa wa tatizo hili ambalo ni tatizo la dunia na sio kwa Zanzibar peke yake au Tanzania.  Hata hivyo, kwa kutambua hilo kupitia mfuko wa vijana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetenga Shilingi Bilioni Nne za Kitanzania kwa ajili ya kuwapatia mikopo ili waweze kujiajiri.  Nitoe wito kwa vijana kujikusanya kutafuta mradi wa kufanya ili kuitumia vizuri fursa hiyo.
Mbali na mfuko huo, Serikali ya Abudhabi kupitia mfuko wa Khalifa (Khalifa Fund) utatoa TZS. Bilioni 23 kwa Zanzibar kwa ajili ya kusaidia tatizo la ajira kwa vijana wetu, kupatikana kwa fedha hizo inatokana na ziara aliyoifanya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika Falme za Kiarabu mwishoni mwa mwaka jana.  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo itaongeza kiasi kama hicho kilichotolewa na Abudhabi Fund ili kusaidia miradi ya vijana.


Aidha, kupitia Mpango wa kunusuru Kaya Masikini chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kipindi cha mwaka 2019/2020 utaendelea na kutekeleza Awamu ya Tatu kwa kuyapa kipaumbele maeneo ya ukuzaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato; kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii; pamoja na utawala bora na uwajibikaji.  Utekelezaji wake utahusisha Shehia zote za Unguja na Pemba.  Awamu hii itatoa msisitizo wa walengwa kufanya kazi zaidi ili kuweza kuongeza kipato chao kwa kujishughulisha na kazi za kiuchumi ili kuondokana na umasikini mapema.


Mheshimiwa Spika, Muungano wetu unaendelea kuimarika ndani ya miaka 55 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali zetu mbili zimekuwa zikiendelea kutatua changamoto zinazojitokeza kupitia mazungumzo baina ya pande mbili.

Mwezi Februari mwaka huu, Kikao cha Pamoja cha SMT na SMZ chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilikutana Dodoma pamoja na mambo mengine kilipitisha utaratibu mpya wa mawasiliano, kwa kuwepo kwa vikao vya Kisekta mara kwa mara pamoja na kuunda Kamati ya Fedha, Uchumi na Biashara na Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria.  Lengo la Kamati hizo ni kuhakikisha kuwa changamoto au kero zinazojitokeza zinatatuliwa kwa haraka bila ya kusubiri Kikao cha Kamati ya Pamoja baina ya SMT na SMZ.


Mheshimiwa Spika, Wiki mbili zilizopita niliongoza timu ya baadhi ya Mawaziri na Watendaji wengine wa Serikali  kwenda Dodoma kukutana na Viongozi Wakuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi wa Tanzania Bara na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano).  Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuwasilisha kwa ndugu zetu hali ya kutoridhishwa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa baadhi ya mambo yanavyotokea.  Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na kukwama kwa miradi mikubwa ya SMZ kunakosababishwa na Sheria za Mikopo, Dhamana na Misaada kama ilivyofanyiwa marekebisho yake ya mwaka 2017, pamoja na masharti mapya ya mikopo kutoka kwa wakopeshaji kama vile EXIM Bank ya China.  Mkutano uliendeshwa vizuri katika hali ya kindugu na kufahamiana, na sote kwa pamoja tumebadilishana mawazo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo.

Nichukue nafasi hii kwa dhati kabisa kuwashukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania kwa jinsi ambavyo walivyotupokea, kutusikiliza na jinsi walivyotuelewa.  Ni matumaini yangu na ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa masuala hayo yatapata ufumbuzi muda mfupi ujao na Muungano wetu utaendelea kuwa imara zaidi.

Mheshimiwa Spika, Msimu huu wa masika nchi yetu ilishuhudia mvua kubwa ambayo ilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu na makaazi ya wananchi.  Jumla ya nyumba 3,837 zimeathirika na mvua, kati ya hizo nyumba 3,037 kutoka Unguja na 800 kutoka Pemba.  Serikali ilichukua hatua ya kugawa vifaa vya kujengea na chakula kwa walioathirika na mvua hizo.  Kwa mara nyengine tena, nawasihi wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi, mabondeni wahame katika maeneo hayo.  Aidha, tuendelee kuwa na utamaduni wa kufuatilia taarifa za kitaalamu zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Kanda ya Zanzibar kupitia vyombo vya habari ili wananchi waweze kunusuru maisha yao na mali zao.  Vile vile, tufuate maelekezo ya kitaalamu yanayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ya kujikinga na maradhi ya mripuko yakiwemo matumbo ya kuharisha.  Miongoni mwa maelekezo yanayotolewa ni pamoja na kuchemsha maji kabla ya kunywa, kusafisha mazingira, kuosha mikono kabla ya kula na mengineyo.  Pia, nawakumbusha wazee na walezi wawe karibu sana na watoto wao ili kuwaepusha kutembelea maeneo hatarishi.Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na hatua za kukamilisha ujenzi wa misingi ya kuondosha maji yanayotuwama sehemu mbali mbali za nchi yetu.  Kukamilika kwa misingi hiyo kutapunguza kwa kiasi kikubwa kutuwama kwa maji barabarani hadi gari kushindwa kupita itakuwa ni historia.  Tayari misingi yenye urefu wa mita 2,485 katika maeneo ya Bubujiko, Kidombo, Toronto, Jambiani Kibigija na barabara ya Uwanja wa Ndege imekamilika na kuanza kazi.


Mheshimiwa Spika, tutambue kuwa ajali za barabarani zinaendelea kuleta madhara makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.  Kwani ajali hizo huondoa maisha ya ndugu zetu ambao ndio tegemeo la familia zetu na ndio nguvu kazi ya Taifa letu.  Pia baadhi yao hupata ulemavu ambao kwa kiasi kikubwa hupunguza uwezo wao wa uzalishaji mali katika kujipatia kipato chao.  Hivyo, nawasihi wasimamizi pamoja na wananchi kuchukua tahadhari wanapoendesha vyombo vya moto wakiwa barabarani.


Mheshimiwa Spika, niruhusu kwa niaba yenu, niwapongeze wasimamizi wa Mradi wa Uendelezaji Huduma Mjini (ZUSP) kwa kusimamia miradi iliyo chini ya mpango huo ikiwemo mradi mkubwa wa kujenga misingi ya maji machafu katika maeneo ya Kijangwani, Kwahani, Kibandamaiti, Sebleni, Mnazimmoja, Kwa mzushi, Karakana, Mtopepo, Darajabovu, Kwamtipura, Mboriborini, Shaurimoyo, Saateni, Mwanakwerekwe, Kwa Mtumwajeni, Nyerere, Kwa Wazee, Sogea, Mikunguni, Kwaalamsha, Mpendae, Jang’ombe, Kilimani, Meya, Urusi na Migombani.
Vile vile, si muda mrefu kutoka sasa miji yetu itaondokana kabisa na kiza totoro, ili kuepukana na wahalifu ambao walikuwa wakinufaika kutokana na kuwepo kwa kiza hicho.


Ninafuraha kuwajulisha wananchi kuwa kazi za kuweka taa katika miji yetu imeanza na taa hizo zitawekwa Unguja na Pemba.  Kwa upande wa Pemba taa za barabarani zitawekwa katika barabara za Mkoani, Chake Chake na mji wa Wete.  Kwa upande wa Unguja taa za barabarani zitawekwa katika barabara za Uwanja wa Ndege, Mnazimmoja, Mwanakwerekwe, Kiembesamaki, Mombasa, Kilimani, Kinazini, Mikunguni na Mwembenjugu.


Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jaa la kisasa huko Kibele unaendelea na tayari umeshafikia asilimia zaidi ya 10, jaa hilo litahusisha eneo la kutenga taka,  ambazo baadhi yake zitatengenezwa mbolea.  Kumalizika kwa jaa hilo la kisasa na la aina yake kwa ukanda wetu wa Afrika, litasaidia jitihada zetu za kukusanya taka na kuzigeuza taka hizo kuwa ni bidhaa ambazo zitakuwa ni kichocheo kingine cha ajira kwa vijana wetu.  Pia tutapunguza gharama kubwa inayotumiwa na Serikali katika kununua mbolea kutoka nje ya nchi.


Mheshimiwa Spika, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 23(4), imeeleza kuwa:-
Kila mzanzibar ana wajibu wa kulinda, kuhifadhi, kudumisha uhuru, mamlaka, ardhi na umoja wa Zanzibar “.

Nawaomba Wajumbe na wananchi wote wa Zanzibar watambuwe kuwa ardhi ni rasilimali muhimu katika maendeleo ya nchi na wananchi wake kiuchumi na kijamii. Hivyo, kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Zanzibar, rasilimali hii bado itaendelea kuwa mali ya Serikali. Wananchi na Taasisi zitapewa ardhi kwa matumizi yao tu na haitoruhusiwa kuuzwa, kurithi, kugaiana au kupeana kwa namna yoyote ile bila ya utaratibu na amri itayotolewa na Serikali kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Spika,  Zanzibar kwa sasa ina Sheria tisa zinazohusiana na matumizi bora na endelevu ya ardhi lakini bado kumejitokeza baadhi ya Viongozi, Watendaji wa Serikali na wananchi kutokuziheshimu Sheria hizo na  kuwa madalali wa kuuza au kuchukuwa ardhi bila kufuata sheria na taratibu zilizopo, hali ambayo inasababisha dhulma na  migogoro mingi katika jamii yetu, hivyo nawaomba watendaji wote waliopewa dhamana ya usimamizi wa sheria za ardhi wawe wazalendo watumie taaluma zao ili kutatua migogoro ya ardhi iliyopo kuanzia ngazi ya Shehia, Wilaya, Mikoa na Taifa  kwa ujumla.  Serikali haitomvumilia na itamchukulia hatua kali mtu yeyote atakaekuwa na tabia ya udalali au kuchukuwa ardhi kwa utashi wake na kwenda kinyume na Sheria za nchi yetu.

Serikali inatambua kuwa kuna baadhi ya wanaojiita wawekezaji wa kizalendo ambao hupewa ardhi na  badala yake huitumia ardhi hiyo kwa kuitia sokoni na kuiuza kwa mamilioni ya dola. Jambo hili halikubaliki na Serikali itawanyang’anya ardhi watu hao endapo watabainika.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbali mbali za kupunguza au kuondosha kabisa migogoro ya ardhi ikiwemo kuimarisha Mahakama za Ardhi nchini, kuendeleza hatua za maandalizi ya upimaji wa miji mipya Unguja na Pemba, kutoa elimu kwa wananchi juu ya utekelezaji wa Sheria na Miongozo inayotolewa juu ya usimamizi wa matumizi mazuri ya ardhi nchini.


Mheshimiwa Spika, naomba kuwaeleza wananchi kuwa, Serikali inaendelea kuhimiza matumizi mazuri ya rasilimali zote nchini ikiwemo mchanga, kokoto na mawe.  Katika utekelezaji wa rasilimali hizo, Serikali imeelekeza utaratibu wa kufuatwa kwa upatikanaji wa mchanga kwa mahitaji ya ujenzi nchini, kwa mujibu wa utaratibu huo mwananchi anaehitaji mchanga anatakiwa kuanzia kwa Sheha ambapo atapewa maelekezo ya ujazaji wa fomu husika hadi kufikia kulipia Benki.  Utaratibu huo wa Serikali unatoa nafasi nzuri na bei muafaka kwa manufaa ya pande zote.  Pamoja na kusisitiza utekelezaji wa agizo hilo la Serikali, nachukua nafasi hii kuvitaka vyombo husika kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaokwenda kinyume bila ya kuwaonea muhali.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wawakilishi kwa namna wanavyoshirikiana na Watendaji na wananchi katika kuendelea kudhibiti mifuko ya plastiki nchini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha usafi wa mazingira. Mafanikio makubwa ya zoezi hilo yameendelea kupatikana kiasi ambacho hata wenzetu Tanzania Bara na wao wameanza zoezi hili rasmi tarehe 01 Juni, 2019.  Tunawapongeza sana!  Nawaomba tuendelee kushirikiana, Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria kwa wale wote watakaokiuka maelekezo ya udhibiti huo ili kuhakikisha mazingira yetu yanaimarika.

Mheshimiwa Spika,
Tatizo la matumizi ya Dawa za Kulevya limeendelea kuathiri sekta mbali mbali za uzalishaji na hivyo kudhoofisha ukuaji wa uchumi na afya za Wazanzibari hasa vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa letu. Serikali kwa kushirikiana na washirika mbali mbali wa ndani na nje ya nchi imefanya jitihada za kukabiliana na tatizo hili ambapo  mwaka 2015 jumla ya kesi 183 sawa na kilo 68.6 za dawa za kulevya ziliripotiwa,  mwaka 2018 kesi 654 sawa na kilo 722.22 za dawa za kulevya zilikamatwa.  Jitihada hizo zinalenga kupunguza madhara na matumizi ya Dawa za Kulevya, pamoja na kudhibiti uingizaji  na usambazaji wa dawa hizo hapa nchini.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kuendeleza Kituo cha Tiba na marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni, kuhakiki vielelezo vya kesi za dawa za kulevya, kuteketeza dawa za kulevya zilizopo katika maeneo ya uhifadhi wa kisheria na kufanya marekebisho ya Sheria ya Dawa za kulevya.


Mheshimiwa Spika, 
Mahakama ni mhimili tunaouamini ambao una Mamlaka ya kutekeleza utoaji wa haki pasina kuingiliwa na mhimili mwengine wowote, tunawaomba watendaji wa muhimili huu kuendelea kutekeleza sheria ipasavyo kwa wale wote watakaokiuka taratibu za sheria wakiwemo wasafirishaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya.  Kwa kufanya hivyo, tutaifanya Zanzibar kuwa huru dhidi ya uingizwaji wa dawa za kulevya na kutumia nguvu kazi yake vizuri kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.


Mheshimiwa Spika, Suala la mgawanyo wa madaraka kati ya mihimili mitatu ya dola, yaani Serikali (Mamlaka ya Utendaji), Baraza la Wawakilishi (Mamlaka ya Kutunga Sheria) na Mahakama (Mamlaka ya kutekeleza utoaji wa haki), imepewa umuhimu mkubwa na kuainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 5A.

Mheshimiwa Spika, Baraza la Wawakilishi ni chombo kitukufu chenye hadhi na heshima ya pekee, kinachofuata Sheria, Kanuni, Miongozo na Maadili kwa Wajumbe na Watendaji wake. Chombo hiki kipo kwa ajili ya kuwakilisha na kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar. Hivyo, ni vyema kwa baadhi yetu Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwacha kuzungumzia maslahi yao binafsi au kuwatetea baadhi ya watu kwa maslahi yao au utashi wao na kusahau wajibu wao waliopaswa kutekeleza katika Majimbo yao waliyochaguliwa.

Mheshimiwa Spika, asilimia kubwa ya Wajumbe wa Baraza lako Tukufu  ni wa Chama cha Mapinduzi (CCM), hivyo, katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 - 2020 ukurasa wa 236 kifungu namba 189 kinasomeka:-

“…..ili Chama cha Mapinduzi kiendelee kukubalika na kuaminiwa na wananchi ni muhimu viongozi wake wawe karibu na wananchi kwa kuwatembelea, kuwasikiliza kero zao na kuzitafutia majawabu......”

Waheshimiwa wenzangu wa Baraza la Wawakilishi, nawaomba sana turudi katika maeneo yetu, ili tukamalizie Utekelezaji wa Ilani yetu ya CCM ya 2015 -2020 pamoja na ahadi nyengine kama tulivyowaahidi wananchi wetu, tukumbuke kuwa kuna msemo wa Kiswahili unaosema kuwa:

“Ada ya Mja hunena Muungwana ni Kitendo”

Ni vyema Wajumbe tuwatendee wananchi wetu matendo mema na mazuri ili na wao wakumbuke fadhila za matendo hayo katika wakati ujao.

Mheshimiwa Spika,
Katika kuharakisha na kuimarisha maendeleo ya Majimbo yetu ya uchaguzi, Serikali imeshatoa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo kwa Majimbo yote 54 kwa Unguja na Pemba. Nawakumbusha Waheshimiwa Wawakilishi wa Majimbo kushirikiana na Kamati zao katika matumizi ya fedha hizo. Vile vile, tunawasisitiza kufanya marejesho kwa wakati ili taratibu za kupata fedha za awamu nyengine ziweze kufanyika mapema iwezekanavyo.


Mheshimiwa Spika, 
Kwa mara nyengine tena, nakupongeza wewe binafsi, na wale wote waliofanikisha Mkutano huu wakiwemo Waandishi wa Habari, Wakalimani wa lugha ya alama na wananchi wote wa Zanzibar kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohammed Shein. Mungu alibariki Baraza letu la Wawakilishi, Mungu aibariki Zanzibar na watu wake, Mungu aibariki Tanzania.


Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako Tukufu liakhirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 18 Septemba, 2019 saa 3.00 barabara za asubuhi panapo majaaliwa.


Mheshimiwa Spika, nomba kutoa hoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.