Habari za Punde

Maadhimisho ya Skauti Miaka 107 Zanzibar.


WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali imetakiwa kuhakikisha kwamba katika mipango na taratibu wanazoziandaa ni vyema wakajipanga vizuri ili uwepo mfumo bora na endelevu wa uratibu na usimamizi wa shughuli za Skauti katika skuli za Zanzibar

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito huo katika maadhimisho ya miaka 107 ya Skauti Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar.

Katika hotuba yake Rais Dk. Shein alisisitiza kuwa ni muhimu uwepo mfumo wa namna moja na unaotambulika rasmi katika kila ngazi inayohusika jambo ambalo litaongeza hamasa na mipango katika kukuza uzalendo, kuamsha ari na kuwakumbusha wananfunzi historia ya nchi yao.

Alieleza kuwa miongoni mwa mambo ambayo yanahitaji kusimamiwa vyema ni lazima kuongezeka kwa heshima, hadhi na thamani za nyimbo za Taifa, Wimbo wa Mashujaa, bendera na nembo za Taifa.

Alisisitiza kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inapaswa kuangalia kuona namna bora ambayo misingi wanayopewa vijana wa Skauti wanakuzwa nayo ili wawe raia wema na wazalendo.

Rais Dk. Shein aliwataka viongozi wa vijana wa Skauti kuwa wamoja na kuepuka vitendo vyovyote vyenye kuashiria ubaguzi kwani wao ni wamoja.

Alieleza kuwa kwa mnasaba huo shughuli za Skauti zina fursa kubwa na nzuri kuendeleza hisia za umoja hasa miongoni mwa vijana ambapo katika hali hiyo vijana hao watakuwa wanapewa urithi bora na kwenda na wakati.

Aidha, Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwaandaa vijana hao ili kuwa wazalendo wa Taifa, akibainisha maendeleo ya nchi na jamii yoyote huletwa na wazalendo.

Alisema uzalendo ndio unaohimiza mtu kufanya bidii, ari, hamasa na kuwa muadilifu katika kazi za halali na hivyo kupata tija na manufaa.

Alisema uzalendo humuongoza mtu kuzilinda na kuzitumia vyema rasilimali za nchi kwa faida ya wananchi, sambamba na kumuepusha kufanya vitendo vya ubadhirifu, rushwa na wizi wa mali ya umma.

Dk. Shein alibainisha kuwa mara baada ya Mapinduzi, Taifa liliweza kupata maendeleo ya haraka ikiwemo uimarishaji wa miundombinu na upatikanaji wa huduma za kijamii, pamoja na wananchi kushiriki kwa moyo katika ujenzi wa nyumba za maendeleo, barabara na vituo vya Afya.

“Kwa bahati mbaya ari na moyo huo umepungua sana hivi sasa,miongoni mwetu, mambo yamebadilika utaratibu wa kujitolea haupewi nafasi kubwa kama zamani”, alisema.

Aliwapongeza vijana wa skauti kwa jinsi walivyo makini na wanaotunza nidhamu, akibainisha kuwa ndio msingi wa mafanikio ya kila kitu.

Alisema mafunzo yanayotokana na shughuli za skauti yanasaidia sana kuwafanya vijana kuwa raia wema wenye kutii sheria na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani.

Alisema vijana wanaopata mafunzo ya skauti huwa wanaandaliwa vyema kuwa walinzi wazuri wa amani.

Dk. Shein alisema amani ni jambo muhimu ambapo limeliwezesha Taifa kupiga hatua za maendeleo katika ukuaji wa uchumi na kuziimarisha huduma mbali mbali , hivyo akawataka wananchi wote kuwa walinzi wa amani.

“Katika kufikia hatua hiyo lazima tuendelee kuwa wamoja na tushikamane ili kila mmoja aone anayo nafasi na wajibu wa kuchangia maendeleo ya nchi na jamii kwa ujumla”, alisema.

Katika hatua nyengine Dk. Shein alisema hivi sasa jamii ya Watanzania imekabiliwa na vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, ajira za watoto, unyanyapaa na hujuma kwa watu wenye ulemavu, hivyo akabainisha umuhimu wa  mafunzo kwa skauti kwani huwaandaa kuweka mbele utu na kupingana na aina zote za ubaguzi.

Akizungumzia kuhusiana na maadhimisho hayo, Dk. Shein alisema yametowa fursa ya kuwakutanisha skauti kutoka maeneo yote ya nchi kwa lengo la kuendeleza umoja na kudumisha mshikamano wa kitaifa.

Alisema mjumuiko huo uliowakutanisha skauti kutoka mikoa 31 ya Tanzania unatowa fursa ya kujifunza mambo mbali mbali muhimu, ikiwemo historia ya nchi, umuhimu wa kuilinda na kudumisha amani pamoja na kuonyesha mapenzi baina ya wananchi.
Aidha, alisema yana akisi dhamira na malengo ya mwanzilishi wa Skauti Duniani Baden Powel alielenga kuwajenga, kuwawezesha na kuwasaidia vijana kuwa wazalendo.

Nae, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma alisema Wizara hiyo kwa kushrikiana an Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ zitaendelea kushirkiana katika kuwaandaa vijana kufanikisha misingi ya kuanzishwa kwa skauti  nchini.

Aidha, Skauti Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania, Mwantum Bakar Mahiza alipongeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa maandalizi mazuri yaliofanikisha vyema maadhimisho hayo.

Alisema maadhimisho hayo yana dhamira ya kuwajenga vijana hao kuwa wazalendo, majasiri pamoja na wenye kujitolea wakizingatia dhana ya uaminifu na uadilifu.

Katika maadhimisho hayo, viongozi mbali mbali wa Kitaifa walihudhuria, akiwemo Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ally Hassan Mwinyi. Rais mstaafu wa SMZ Amani Abeid Karume, Waziri Kiongozi mstaafu Dk. Mohamed Gharibu Bilali an Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.  

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address 2422 Tel.:O777427449. Fax : 024 2231822
E – mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.