Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenmyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Azungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Okan ya Uturuki Ikulu Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Akizungumza na Mwenyekiti wa Kampuni ya Okan ya Uturuki na Balozi wa Uturuki Nchini Tanzania kushoto Ali Davutaglu na Mwenyekiti wa Kampuni ya Okan Mr.Bekir Okan, walipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya uongozi wa Makampuni ya Okan yenye makao makuu yake nchini Uturuki inayokusudia kujenga hospitali ya utibabu wa meno hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Makampuni ya Okan ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Chuo Kikuu cha Okan kiliopo Istanbul nchini Uturuki akiwa amefuatana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Davutaglu.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Uturuki zina historia kubwa hali ambayo imepelekea hadi lugha ya Kiswahili kutohowa baadhi ya maneno kutoka katika lugha ya Kituruki.

Mbali na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar na Uturuli zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu hali ambayo imeimarika kutokana na uongozi thabiti wa pande mbili hizo.

Akieleza kuhusu azma hiyo ya Makampuni ya Okan ya nchini Uturuki kuja kujenga hospitali ya meno pamoja na mradi mwengine wa upanuzi na vifaa kwa ajili ya Hospitali ya MnaziMmoja, Rais Dk. Shein alisema kuwa hilo ni jambo la busara na litasaidia kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaiunga mkono miradi hiyo na iko tayari katika kushirikiana na Makampuni hayo makubwa ya nchini Uturuki katika kuianzisha  miradi hiyo mara tu baada ya kukamilika kwa taratibu na majadiliano baina ya pande mbili hizo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itaunda timu maalum na kukaa pamoja na timu ya Makampuni hayo ya Okan kwa lengo la kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa na linakwenda kwa kasi na kufikia azma iliyokusudiwa.

Aliongeza kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Chuo chake Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ina mpango wa kuanzisha masomo yanayohusiana na kada hiyo ya utibabu wa meno, hivyo itakuwa ni jambo la busara kwa Chuo Kikuu cha Okan kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuanzisha Hospitali hiyo.

Rais Dk. Shein pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga Hospitali katika eneo la Binguni, Wilaya ya Kati, Unguja na kutoa ushauri kwa uongozi huo kuwa ni jambo la busara iwapo ujenzi wa hospitali hiyo utafanyika katika eneo hilo lenye ukubwa za hekta 45 kutokana na nafasi kubwa iliyopo ikilinganisha na eneo la Hospitali ya MnaziMmoja.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliunga mkono azma ya uongozi huo wa Makampuni ya Okan ya kuekeza katika sekta ya utalii hapa nchini na kusema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa sekta alizozijadili katika mazungumzo aliyoyafanya wakati wa ziara yake nchini Uturuki mwaka 2011 alipokutana na Rais wa nchi hiyo wakati huo Rais Abdallah Gul.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shen aliongeza kuwa katika mazungumzo yake na kiongozi huyo walikubaliana kuwepo kwa mashirikiano katika sekta mbali mbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, afya, kilimo,biashara na uwekezaji utalii na nyenginezo ambapo tayari kwa sekta ya afya inaendelezwa na hivi sasa wapo Wazanzibari wanaosomea kada ya afya nchini humo.

Alieleza kuwa ziara yake hiyo aliyoifanya nchini humo kufuatia mwaliko wa Rais Gul pia, imeweza kuzaa matunda kwa upande wa sekta ya usafirishaji kutokana na kutekelezwa kwa ombi lake la Shirika la ndege la Uturuki (Turkish Airlines) kuanza safari zake hapa Zanzibar.

Hata hivyo, Rais Dk Shein alisisitiza haja kwa Kampuni hiyo ambayo pia, inajihusisha na sekta ya utalii katika nchi kadhaa duniani ambapo ina hoteli kubwa ya kisasa katika Mji wa Miami nchini Marekani, kuanzisha safari za ndege kati ya Zanzibar, Uturuki katika mji wa utalii wa Antalya na Miami kwa lengo la kuimarisha sekta ya utalii hapa Zanzibar.

Nae Mwenyekiti huyo wa Makampuni ya Okan, Bekir Okan alimueleza Rais Dk. Shein azma ya Kampuni hiyo kupitia Chuo Kikuu chake cha Okan kiliopo nchini Uturuki ya kuanzisha miradi hiyo mikubwa miwli ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hosptali hiyo ya meno hapa Zanzibar.

Alieleza kuwa Okan iko tayari kuanza kwa miradi hiyo mikubwa hapa Zanzibar baada ya kukamilika kwa taratibu zote za Serikali zikiwemo mazungumzo ya pamoja kati ya timu za wataalamu wa Uturuki na Zanzibar na kuahidi kuanza ujenzi mara tu baada ya mazungumzo.

Kiongozi huyo alitumia fursa hiyo kueleza uzoefu na uwezo wa Kampuni hiyo ya Okan katika masuala mbali mbali ya uwekezaji ikiwemo utalii, usafiri na usafirishaji, ujenzi pamoja na utoaji mafunzo kupitia chuo chake Kikuu cha Okan.

Aidha, alieleza hatua zitakazofuata baada ya kukamilika kwa hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Zanzibar kwenda nchini Uturuki kwa mafunzo zaidi.

Nae Balozi wa Uturuki Ali Davutaglu alimueleza Rais Dk. Shein kuwa kukamilika kwa miradi hiyo hapa Zanzibar kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano na mashirikiano kati ya pande mbili hizo ambayo yana historia kubwa.  
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.