Habari za Punde

Balozi Seif ziarani Pemba akagua ujenzi wa Maabara ya Sayansi Skuli ya Kilindi akutana na kamati za ulinzi na usalama za mikoa miwili

Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Maalim Mohamed Nassor akitoa Taarifa ya ujenzi wa Maabara ya Sayansi Skuli ya Kilindi mbele ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika kukagua Ujenzi huo.
 Balozi Seif akiambatana na Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suleiman Abdullah akiangalia ujenzi wa Maabara ya Sayansi Skuli ya Sekonmdari ya Kilindi Mkoa wa Kusini Pemba.
 Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mh. Hemed Suleiman Abdulla akiishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada inazochukuwa za kusogeza maendeleo ndani ya Mkoa huo.
  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Kilindi na Vitongopji vyake baada ya kulikagua Jengo la Maabara ya Sayansi katika Skuli ya Kijiji hicho.
 Balozi Seif  akizungumza na Viongozi wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa Miwili ya Pemba kwenye Ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo Wawi Chake chake Pemba kujadili zoezi la uhakiki wa kuyatambua mashamba na Eka za Serikali.
Balozi Seif akisisitiza jambo wakati akizungumza na Viongozi wa Kamati za ulinzi na Usalama za Mikoa Miwili ya Kusini na Kaskazini Pemba hapo Ukumbi wa Makonyo Wawi Chake Chakle Pemba.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanza kuonyesha kwa vitendo utekelezaji wa msingi wa uimarishaji wa Miundombinu katika Sekta ya Elimu kwenye Fani ya Sayansi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia yaliyopo Ulimwenguni.
Alisema utekelezaji huo umezingatia muelekeo wake katika Ujenzi wa Majengo 24 ya Maabara ya Sayansi { School Hurb } katika Visiwa vya Unguja na Pemba yatakayojikita na masomo ya Kemia, Fizikia na Biology.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo mwanzoni wa ziara yake ya Siku Nne Kisiwani Pemba kuangalia Miradi ya Maendeleo pamoja na ufuatiliaji wa Mashamba na Eka tatu tatu ambazo bado haliko kwenye Miliki ya Serikali.
Alisema wakati umefika kwa wanafunzi wa Skuli za Sekondari Unguja na Pemba kuchangamkia fursa hiyo ambayo  katika siku za baadae itaweza kuziba pengo la upungufu wa Wataalamu wa Fani ya Sayansi  hapa Nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhika na kiwango kizuri cha Ujenzi  kilichofikiwa na Wahandisi wa Majengo hayo Kampuni ya Kizalendo ya Salim Contructor na kuzitaka Kampuni nyengine zitakazopewa jukumu la ujenzi wa Majengo ya Serikali na Taasisi za Umma kuzingatia ubora wa kiwango kinachokubalika.
Akitoa Taarifa ya Ujenzi wa Maabara ya Sayansi ya Skuli ya Kilindi Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Nd. Mohamed Nassor alisema Maabara hiyo ni miongoni mwa Majengo  24 yanayoendelea kujengwa katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.
Nd. Mohamed alisema Maabara ya Sayansi {Shool Hurb} yameanzishwa kama vituo vya kutoa huduma katika masomo ya Sayansi likiwemo pia somo mama la Kingerezakwa Wanafunzi hasa waliko Vijijini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa fursa hizo.
Akitoa salamu Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alisema Wananchi wa Mkoa huo wanafurahia Maendeleo makubwa yanayopatikana chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein.
Alisema huduma za Maji safi na salama, Umeme Bara bara za Lami pamoja na miundombinu ya Miradi ya Kiuchumi imekuwa ikileta matumaini ya kuongezeka kwa Kipato cha Wnanchi hao jambo ambali limestawisha Maisha yao ya kila siku.
Mh. Hemed alisema Wananchi wana kila sababu ya kujivunia maendeleo hayo makubwa yanayoonekana kila pembe katika dhana nzima ya Utekelezaji wa vitendo wa ahadi zilizotolewa na Serikali ikiwemo kuwasili kwa vifaa vya kutengenezea Miundombinu ya Mawasiliano Kisiwani Pemba.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alikutana na Viongozi wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa Miwili ya Pemba katika Ukumbi wa Mikutano wa Makonyo Wawi Chake Chake Pemba.
Mkutano huo uliohudhuriwa pia na Baadhi ya Mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulijadili na kutafakari hatua zilizochukuliwa na Taasisi mbali mbali Kisiwani Pemba zilizopewa jukumu la kufuatilia na kubaini Mashamba na Eka za Serikali ambazo kwa kipindi kirefu ziko mikononi mwa Watu.
Akitoa Taarifa ya zoezi hilo Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo, Malisili, Mifugo na Uvuvi Pemba Nd. Sihaba Haji Vuai alisema Wizara hiyo imekabidhiwa Madaftari yenye takwimu za Mashamba na Eka za Serikali tokea Mwaka 20113.
Alisema vielelezo vilivyomo ndani ya Mabuku hayo Matatu vimeainisha uwepo wa Mashamba na Eka 2,438 Wilaya ya Mkoani, eka 2,299 Wilaya ya Chake chake na Ekari 2,273 Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Nd. Sihaba alisema Watendaji wa Wizara ya Kilimo ilianza zoezi la kuyafuatilia Mashamba na eka za Serikali katika maeneo mbali mbali kwa kushirikiana na Masheha wa Shehia zilizomo Shamba na Eka hizo.
Alisema zoezi hilo liliweza kubaini uwepo wa Eka 838 Wilaya ya Mkoani, eka 295 Wilaya ya Chake chake, eka 992 Wilaya ya Wete na eka831 katika Wilaya ya Micheweni.
Alifahamisha kwamba mashamba yote ya Serikali yaliyomo ndani ya mikono ya Watu yamekadiriwa kufikia 9,982, ambapo hadi sasa yaliyobainika hadi sasa ni mashamba 6,315 sawa na asilimia 63% ya mashamba yote Kisiwani Pemba.
Afisa mdhamini huyo wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugona Uvuvi Pemba alieleza kwamba uchambuzi wa mashamba na eka hizo umefafanua kwamba Mashamba 2016 yana miti ya Mikarafuu, mashamba 721 miti ya Minazi, 1,884 mazao mchanganyiko, 365 yameachwa muda mrefu, 600 yamegeuzwa kuwa Makaazi na 1200 mashamba yaliyofungishwa Mkataba.
Alisema Mashamba yapatayo Mia 732 yako kwenye utaratibu wa kutaka kugaiwa kwa Wananchi kwa shughuli za kuendeleza Kilimo ili kusaidia kunyanyua kipato chao kitakachokidhi maisha yao.
Nd. Sihaba alisema utayari mdogo wa baadhi ya Viongozi, Taasisi za Umma pamoja na Wananchi ndio unaopelekea baadhi ya Eka walizopewa Wananchi kwa shughuli za Kilimo kugezwa matumizi mengine jambo linalokwenda kinyume na malengo ya utolewaji wa Eka hizo mnamo Mwaka 1964.
Wakichangia  Taarifa hiyo Baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho walisema Viongozi wanaosimamia zoezi hilo lazima wawe tayari kufuatilia  kwa kina mashamba hayo na kuondoa muhali unaopelekea kuzorotesha zoezi hilo muhimu.
Walisema ipo haja ya kufuatilia kwa kina kuanzia ngazi ya Mtaa, shehia hadi Jimbo ili kuibaini Mashamba na Eka ambazo hadi sasa ziko ndani ya mikoni ya baadhi ya Watu.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema zoezi hilo la kubaini mashamba na eka za Serikali zilizo mikononi mwa Watu halina lengo la kuwanyang’anya wale wanaoendelea kuzitumia badhi kinachofanyika ni utambuzi wa kujua mali za Serikali.
Balozi Seif alisema wapo baadhi ya Wananchi katika maeneo tofauti Nchini wanayashughulikia mashamba na Eka za Serikali na unapofika wakati wa mazao wao ndio wanaopewa nafasi ya kwanza kukodi hasa katika upande wa zao la Karafuu.
Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitahadharisha kwamba Serikali haitasita kuchukuwa hatua za kunyang’anya Eka ya Serikali Mtu ye yote atakayebainika kuificha mali ya Serikali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.