Habari za Punde

Shabiki amchinja mchezaji Ndondo Carry Cup

Na Ramadhani Ali/Maelezo     
     
Michuano ya soka Jimbo la Muembe makumbi yaliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo hilo Salum Ussi Pondeza (Amjadi) na kupewa jina la ‘Muembe makumbi Ndondo Carry  Cup’ jana ilipata mshutuko wakati wa pambano kati ya timu ya Chilla ilipokuwa ikivaana na Timber City katika kiwanja cha Muembe makumbi chini ya daraja.
Mshtuko huo ulijiri baada ya Shabiki mmoja anaesadikiwa kuwa wa timu ya Timber City kumfanyia kitendo cha maudhi beki wa Chila Ahmed Abdalla ‘Sheshe’ alieonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa Timber City kurejesha bao ambalo tayari walikuwa wamefungwa.
Kitendo alichofanyiwa Sheshe na shabiki huyo kilimkasirisha na kuamua kumkimbiza na kumshambulia kwa ngumi na ndipo shabiki huyo kuchomoa kisu na kumchoma katika mkono licha ya juhudi  zilizochukuliwa na viongozi wanaosimamia mashindano hayo kumzuia.
Baada ya tukio hilo kijana huyo aliamua kujihami kwa kukimbia akihofia kichapo kutoka kwa wachezaji na washabiki wa timu ya Chilla ambao walionekana kukasirishwa na kitendo hicho kisichokuwa cha kiungwana kwenye viwanja vya michezo.
Baadhi ya wapenzi wa soka waliokuwa wakiangalia pambano hilo walipigwa na mshangao kwa washabiki wa timu kuja kiwanjani wakiwa na silaha na kukosekana walinzi wa usalama wakati ikionekana wazi michuano hiyo inavuta washabiki wengi kutoka maeneo tofauti ambapo mshindi atapata zawadi ya gari aina ya Carry iliyotolewa na mbunge wa jimbo hilo Amjadi.
Wapenzi hao wa soka wamewashauri wasimamizi wa michuano hiyo kwa kushirkiana na Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Muembe makumbi kuanzia sasa kunadaa ulinzi katika viwanja vinavyofanyika mashindano hayo ili kudhibiti vitendo vya uvnjifu wa amani vinavyoweza kutokea.
Katika mtanange huo Chilla iliilaza Timber City bao 1-0 lililofungwa kwa njia ya penelti na Salum Gaucha katika dakika ya 67 baada ya mlinzi mmoja wa kuunawa alipokuwa katika harakati za kuokoa.
KUTOKA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.