Habari za Punde

Wiki ya Viwanda Kufanyika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Na Mwashungi Tahir      Maelezo        30-07-2019.
WAZIRI wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali amewataka Wajasiriamali wa Zanzibar kuitumia fursa ya maonyesho ya SADC ya wiki ya viwanda inayotarajiwa  kufanyika katika ukumbi wa Mwalim Nyerere Dar es  Salaam .
Akizungumza na muandishi wa habari  hizi huko ofisini kwake Migombani  alielezea umuhimu wa kushiriki kwa wawekezaji wa viwanda , wajasiriamali wa Zanzibar na  jinsi watavyojitangaza kupitia mkutano huo ambao utaanza tarehe 4-9 mwezi ujao.
Alisema Wazanzibar wanaweza kushiriki katika wiki ya viwanda kwa kutangaza bidhaa zao ambazo zina kiwango na kujulikana ndani ya  soko kwa kupitia maonesho hayo .
Hivyo alisema Zanzibar tuna fursa nyingi kwa upande wa SADC na kuwataka wafanyabiashara, wajasiriamali kutoa bidhaa zinazokuwa na mvuto ikiwemo mwani, vanilla, mafuta ya karafuu, mafuta ya nazi  na baadhi ya bidhaa nyengine adhimu za Zanzibar.
“Tuacheni woga tutangaze biashara zetu , wajasiriamali waonyeshe mambo ya kizanzibar yenye mvuto yakiwemo ya Utalii, Spice za kila aina tulizonazo hapa Zanzibar”, alifahamisha Waziri Amina.
Akitoa wito kwa wafanyabiashara kutumia fursa ya kufanya mambo mengi katika wiki hiyo ambayo yatasaidia kutangaza  biashara na milango iko wazi ya kuendeleza sekta ya biashara nchini .
Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda  Juma Hassan Reli alisema SADC ni jumuiya ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika ambao umoja wake umeundwa kwa kurahisisha wafanyaji biashara na kuweka vigezo mbali mbali vya kuichumi.
Alisema wafanyaji biashara wawe na  uwiano wa kodi ili kuweza kusababisha umoja wa  soko na uchumi kwa kuweza kubadilishana uzoefu na kuingiza kipato.
Alisema wageni wanaokuja ni viongozi wakuu wakiwemo mawaziri makatibu na marais na hii ni nafasi pekee  ya kujitangaza kupitia wageni hao kwa kununua bidhaa zao.
 Pia alisema kwa upande wa Zanzibar tumepata mabanda kumi kwa lengo la kuonesha bidhaa  mbali mbali zenye kiwango zilizothibitishwa na ZBS hivyo waichangamkie nafasi hiyo ambayo mwaka huu inafanyika Tanzania.
Alisema wageni wataoshiriki tayari wameshaandaliwa mambo yote muhimu ikiwemo usafi kusafishwa sehemu zote ili kunusurika na maradhi mbali mbali na pia wageni hao wanatarajiwa kutembelea hadi Zanzibar kuona vivutio mbali mbali vya utalii.
Vile  vile aliwataka wajasiriamali wajitokeze kwa wingi kupitia chamber commercial kwani faida nyingi zitapatikana ikiwemo fursa ya ajira.
Kwa upande wafanya biashara walisema wamefarijika kufanyika maonesho ya wiki ya viwanda Tanzania kwani wataweza kujitangaza na kupata utaalamu, kubadilishana mawazo  na kujenga uhusiano na wafanyabiashara  na wajasiriamali wenzao kutoka nchi mbai mbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.