RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar iko katika hatua za mwisho za makubaliano ya ujenzi wa
kiwanda kikubwa cha kusarifu mwani kwenye eneo la Chamanangwe, Kisiwani Pemba.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho
ya Nane Nane yaliyofanyika huko Langoni, Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini
Magharibi ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na
Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja
na wananchi wengine.
Rais Dk. Shein alisema kuwa ujenzi wa kiwanda
hicho utafanyika kwa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Kampuni ya OCEAN FRESH pamoja na Kampuni ya KAPA CARAGEENAN NUSANTARA kutoka
nchini Indonesia.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alisema kuwa
kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda hicho cha mwani kutapelekea kufanyika mabadiliko
makubwa ya kilimo cha mwani, uzalishaji wake, bei pamoja na maendeleo yake ya
hapo baadae.
“Mwani ni zao linaloshughulikiwa na wananchi wengi
humu visiwani mwetu hasa kina mama, kwa kuwaunga mkono wananchi hao katika
jitihada zao za kulima na kuuza zao hilo, Serikali imekusudia kuliendeleza zao
la mwani”,alisisitiza Rais Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa azma hiyo ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar ni miongoni mwa ajenda zake kuu ambazo imezipangia Wizara ya Kilimo,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi izitekeleze kwa kushirikiana na Wizara ya Biashara
na Viwanda.
Dk. Shein amekuwa akichukua juhudi za makusudi
katika kuliimarisha zao la mwani ambapo katika ziara yake aliyoifanya mwezi
Agosti mwaka jana 2018 nchini Indonesia alipata fursa ya kutembelea na kukutana
na uongozi wa Kampuni ya mwani ya ‘AGAR
Swallow’ ya nchini Indonesia kwa lengo la kukuza mashirikiano katika
kuliimarisha zao la mwani hapa Zanzibar.
Alieleza kuwa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kushirikiana na Indonesia katika
kuhakikisha zao hilo linaimarika kwani Zanzibar ni miongoni mwa wazalishaji
wakubwa wa zao hilo duniani hivi sasa.
Dk. Shein pia, aliueleza
uongozi huo kuwa azma moja wapo ya kufanya ziara ya kukitembelea kiwanda hicho
ni kujifunza sambamba na kuangalia utaalamu unaofanyika kwa lengo la kupanua
wigo kutoka kwa kampuni hiyo kubwa na yenye uzoefu wa muda mrefu nchini humo.
Nao uongozi wa Kampuni
ya mwani ya ‘AGAR Swallow’ ya nchini Indonesia uliahidi kushirikiana na
Zanzibar katika kuliimarisha zao la mwani ambalo limekuwa ni miongoni mwa zao kuu
la biashara katika visiwa vya Zanzibar wakati ulipofanya mazunguzo na Rais Dk.
Shein katika ofisi za Kampuni hiyo zilizopo mjini Jakarta wakati alipokitembelea
kiwanda hicho.
Katika mazungumzo hayo,
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo Hendrico
Soewardjono alimueleza Rais Dk. Shein azma ya Kampuni hiyo
ya kushirikiana na Zanzibar katika
kuliendeleza na kuliimarisha zao la mwani.
Alieleza kuwa Kampuni
hiyo tayari imepata mafanikio makubwa ambapo aina ya bidhaa yake ya unga wa
mwani ambayo hutengenezewa bidhaa mbali mbali za vyakula na dawa imekuwa na
soko kubwa na bidhaa zake huzisafirisha nchi mbali mbali duniani.
Aliongeza kuwa kutokana
na Zanzibar kuliendeleza zao hilo la mwani na kulimwa kwa wingi Kampuni yake
iko tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo juu
ya uendelezaji wa zao hilo pamoja na
utafutaji wa masoko.
Mkurugenzi Mkuu huyo
alimueleza Dk. Shein kuwa aina ya unga anaotokana na mwani wa aina ya
grasilarias unaotengenezwa kiwandani hapo umekuwa ukitumika sana kwa
kutengenezea bidhaa mbalimbali ambazo zimekuwa maarufu duniani.
Alieleza jinsi
wanavyolisarifu zao la mwani huku akieleza kuwa miongoni mwa bidhaa zinazotengenezewa
unga huo ni vyakula, vipodozi, dawa zikiwemo dawa za meno pamoja na kutengeneza
bidhaa nyengine mbali mbali.
Aidha, kiongozi huyo wa
Kampuni ya AGAR alieleza namna Serikali ya Indonesia kupitia Kampuni yake hiyo
inavyoliendeleza na kulisimamia zao la mwani pamoja na kushirikiana na kampuni
ndogo ndogo zinazofanya biashara ya zao hilo nchcini humo.
Pia, kiongozi huyo
alieleza kuwa kutokana na Kampuni hiyo kupata mafanikio makubwa itakuwa ni
jambo la busara kushirikiana na Zanzibar katika kuliimarisha zao hilo pamoja na
kuja kuonesha uzoefu na mafanikio waliyoyapata kwa lengo la kuwasaidia wakulima
wa mwani wa Zanzibar
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment