Habari za Punde

UHAMIAJI, NIDA Watakiwa Kuhudumia Wananchi.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wananchi waliofika Makao Makuu ya Uhamiaji Visiwani Zanzibar leo  kupata pasi za kusafiria za kielektroniki, wapili kulia ni Kamishna wa Uhamiaji Johari Suluhu.
Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na. Mwandishi Wetu.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni  amewataka  watumishi  wa  Idara  ya Uhamiaji  na Mamlaka ya  Vitambulisho vya Taifa(NIDA) kuwahudumia wananchi walioiweka serikali madarakani ili kuepuka baadhi ya mbinu zinazotumiwa na watu wasio na nia njema kuvuruga amani ya nchi.
Ameyasema hayo Makao Makuu ya Uhamiaji Zanzibar  baada ya kukagua zoezi la utolewaji vitambulisho vya taifa na ubadilishaji wa pasi za zamani za kusafiria baada ya kupokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi waliofika katika ofisi hizo.
“Kuna sauti zinatembea katika mitandao ya kijamii zikieleza ubaguzi unaofanyika katika kutoa pasi na vitambulisho, bado siamini kama kweli watumishi wetu mnafanya hivyo. Muhimu fanyeni kazi kuhudumia wananchi hawa bila kubagua mtu yoyote yule muhimu awe na nyaraka zote muhimu zinazomtambulisha,” alisema Masauni.
“......wananchi hawa wamezichagua serikali hizi mbili lazima tuwahudumie maana ndio waajiri wetu,hatuwezi kuwa tupo katika serikali kisha hatuhudumii wananchi ipasavyo au tunahudumia kwa ubaguzi” aliongeza Masauni.
Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri Masauni wananchi waliofika katika ofisi hizo waliiomba wizara kuongeza idadi ya watumishi hasa katika kipindi hiki cha kukaribia mwisho wa kubadilisha pasi za kusafiria ili kupunguza kupoteza muda mrefu kufuatilia pasi hizo za kusafiria.
“Tangu asubuhi saa mbili tuko hapa na huduma zimekua zikienda taratibu sana,tunaomba kuwepo na uharaka wa kupata huduma hizi,wiki nzima tunakuja hapa lakini utolewaji umekua auridhishi sana,nadhan watumishi waongezwe” alisema Abdallah Kheri Said Mkazi wa Vuga.
Akizungumza katika ziara hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA),Hassan Hassan alisema matarajio mpaka mwisho wa mwaka huu ni kusajili watu Laki Nane Thelathini Sita Elfu huku akiweka wazi changamoto za wingi wa watu wanaofika kwa ajili ya kuchukua vitambulisho ambavyo vimekua vinatumika katika kupata pasi za kusafiria na usajili wa laini za simu.
“Tutaletewa mashine 15 kutoka Tanzania Bara ili tuweze kuhudumia watu wengi kwa wakati mmoja ili kupunguza foleni na kuharakisha utolewaji wa vitambulisho hivyo” alisema Hassan.
Nae Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar Johari Suluhu alitaja changamoto ya kipato  kwa  raia walowezi ambao gharama ya kupata kibali cha kuishi  ambayo ni milioni mbili kuwa ni  kubwa huku wakilalamika vipato vyao vikiwa vidogo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.