Habari za Punde

Balozi Seif akutana na Balozi wa Saudi Arabia nchini

 Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Mohamed Ben Mansour Al- Malek akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofika Nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam kwa mazungumzo.


 Balozi Mohamed Ben Mansour Al- Malek akisisitiza jambo na kumuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  msimamo wa Saudia kuendelea kuiunga Mkono Zanzibar katika harakati za maendeleo.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  akiishukuru Saudia kwa kusaidia miradi ya Jamii yakiwemo masuala ya Majengo ya Ibada.
 Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Mohamed Ben Mansour Al- Malek na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakipongezana baada ya mazungumzo yao wa uhusiano wa Kidiplomasia.
Picha na – OMPR – ZNZ


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Saudi Arabia yenye kuunga mkono harakati za maendeleo ya Zanzibar katika masuala ya Afya na Sekta ya Mawasiliano bado inafursa zaidi ya kuongeza nguvu zake katika sekta nyengine za Maendeleo kwa maustakabala wa kustawisha Maisha ya Wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.
Alisema Saudia Arabia Taifa lilioko Mashariki ya Kati  kupitia Mfuko wa Misaada ya Maendeleo wa Nchi hiyo {Saud Fund} itaendelea kukumbukwa na Wananchi walio wengi kutokana wa kusaidia Sekta ya Mawasiliano katika ufadhili  wa Ujenzi wa Bara bara pamoja na Vifaa kwa ajili ya Hospitali tofauti Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana Mohamed Ben Mansour Al – Malek  Nyumbani kwake Bara bara ya Haile Selassie Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif alisema ipo miradi kadhaa ya Ustawi na Maendeleo akiiainisha iliyopata msukumo kutoka Serikali ya Saudia kuwa ni pamoja na ujenzi wa Bara bara ya Chake Chake Wete na msaada wa Vifaa vya tiba Katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja.
Naye Balozi wa Saudi Arabia Nchini Tanzania Bwana  Mohamed Ben Mansour Al – Malek alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Nchi yake itaendelea kuunga mkono harakati za Maendeleo ya Visiwa vya Zanzibar vilivyojitahidi kuweka Miundombinu imara hasa katika Sekta ya Utalii.
Balozi Mohamed alisema Zanzibar kwa sasa inayonekana kung’ara katika Sekta ya Utalii mbali ya kupokea Wageni kutoka Mataifa ya Ulaya lakini tayari harakati za Watalii wa Mashariki ya kati kuelekeza safari zao Visiwani Zanzibar zinaanza kunukia.
Balozi huyo wa Saudi Arabia Nchini Tanzania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ziara zake Visiwani Zanzibar miaka Miliwi ya hivi karibuni zimemthibitishia kuona Maendeleo makubwa ya Sekta ya Utalii yaliyomuwezesha kuona Hoteli kubwa  zenye hadhi ya kupokea Wageni wa daraja lolote Duniani.
Akizungumzia suala la Ibada ya Hija inayofanyika kila Mwaka Maka Saudi Arabia Balozi wa Nchini Hiyo hapa Tanzania Bwana Mohamed alisema jitihada zitaendelea kufanywa na Uongozi wa Wizara inayosimamia masuala ya Hijja Nchini humo ili kuona Mahujaji wanaotoka Nchini Tanzania wanakamilisha Ibada zao kwa utulivu.
Balozi Mohamed Ben Mansour Al – Malek alisema hitilafu zilizojitokeza katika Miaka ya karibuni ya kuleta mtikisiko kidogo kwa Mahujaji wa Tanzania umepatiwa ufumbuzi na jitihada zimechukuliwa katika kuona utulivu wa Mahujaji wote Duniani unapatikana wakati wa kipindi choche cha Ibada ya Hijja.
Hijja ni nguzo ya Tano na ya Mwisho Miongoni mwa nguzo anazolazimika Muumini wa Dini ya Kiislamu mwenye uwezo kuitekeleza Mara moja kwenye maisha yake huko katika  Ardhi tukufu ya Makka Nchini Saudi Arabia.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.