Habari za Punde

Mafunzo ya kujenga uelewa kwa wasaidizi watoaji huduma za msaada wa kisheria yafanyika


Na Raya Hamad  (WKS)                                                                                     
Imeelezwa kuwa azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma stahiki za msaada wa sheria kutoka kwa wanasheria ambao  wana sifa zinazohitajika kwa  mujibu wa sharia.  

Mkurugenzi wa Idara ya Msaada wa Kisheria  Bi Hanifa Ramadhan Said ameyasema hayo wakati alipokuwa akifunguwa mafunzo ya siku moja ya kujenga  uelewa kwa wasaidizi watoaji huduma za msaada wa kisheria kutoka taasisi mbali mbali za watoa huduma kwenye ukumbi wa mkutano Wizara ya Katiba na Sheria Mazizini.

Bi Hanifa amesema kuwa kila mwananchi anayo haki ya kupata  msaada wa kisheria bila ya ubaguzi kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo inasisitiza kulindwa kwa  haki za binadamu

“Uwepo wa Idara ya Msaada wa Kisheria Zanzibar, kunafungua ukurasa mpya katika kuhakikisha kuanzisha haki na wajibu kwa watoaji wa msaada wa huduma za kisheria, vigezo na viwango pamoja na usimamizi mzima wa huduma za msaada wa kisheria” alisisitiza.

Mkurugenzi Hanifa ameiomba jamii  kuwa tayari kuitumia Idara ya Msaada wa Kisheria  pamoja na wasaidizi wake kwa utaratibu maalum uliowekwa kwani sio watu wote watapewa huduma hio isipokuwa kwa yule asie na uwezo kama sheria na kanuni  zinavyoelekezwa
Aidha amesisitiza kuwa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inatambua na inahakikisha haki na inajumuisha suala la msaada wa kisheria kama msingi wa haki za binadamu kwa watu wote hivyo ni wajibu wa watoaji wa msaada wa kisheria kuifuata miongozo iliyowekwa ili kuweza kuisaidia jamii kupata msaada wa kisheria kwa ufanisi na kwa wakati.
Nao wawezeshaji wa mafunzo hayo na maafisa Sheria  kutoka Idara ya msaada ya kisheria Bw Ali Haji Hassan na Bi Hajar Idrisa Haji wamewataka washiriki hao kufanya tathmini na kuwa waangalifu pale  mdai anapopeleka maombi  yake ikiwemo kutoa vipaumbele  kwa  masuala ya watoto, wazee, watu wenye ulemavu, unyanyasaji wa kijinsia udhalilishaji, migogoro ya ardhi, uriti, huduma za mtoto na masuala ya uvunjifu wa haki za binaadamu.
Ndugu Ali amesema mtoa huduma atahitajika kuweka utaratibu wa tathmini ya huduma anayoitoa kwa ufatiliaji wa mwenendo wa ushauri, mafunzo na taarifa za kila mwezi na kumbukumbu za vikao na kusisitiza kuwa kanuni imeweka wazi juu na kutoa muongozo kwa watoa huduma hao

Aidha katika kuweka usimamizi mzuri, kanuni imeweka wazi kuwa msaidizi wa sheria katika utekelezaji wa majukumu yake atakuwa chini ya uangalizi wa Wakili au Mwanasheria

Bi Hajar amezianisha baadhi ya kazi tofauti zinazofanywa na Idara ya Msaada wa Kisheria ikiwemo kutoa miongozo ya kisera kwa watoaji wa msaada wa kisheria, kusajili watoaji wa msaada wa kisheria, Kumtaka mtoa msaada wa kisheria kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa mtu asiekuwa na uwezo, na kumshauri Waziri kuhusu sera na mambo mengine muhimu yanayohusu kuimarisha utaoaji wa msaada wa kisheria.
Katika kuleta ufanisi na kufanikisha  kazi za utoaji msaada wa huduma za kisheria  kanuni zimeelezea utaratibu maalum kwa watoaji wa msaada huo, ikiwemo taasisi au mtu anayetoa huduma hizo kuhakikishwa uwezo wake wa kufanikisha kazi hiyo, ili kuepuka ubabaishaji wakati wa utoaji wa huduma.
Wawezeshaji hao wamewaomba watoaji wa msaada wa kisheria kuipa mashirikiano ya kutosha Idara ili kuweza kufikia malengo pia kuzisoma na kuzielewa vizuri kanuni kwa lengo la kufikisha elimu kwa walengwa ambao ni wataka huduma wa msaada wa kisheria
Wakitoa michango yao washiriki wa mafunzo hayo wameomba kuwepo kwa mikutano mara mbili kwa mwaka kwa wasaidizi wote wa msaada wa kisheria, aidha wameomba kupatiwa vitambulisho maalum ili watakapokwenda kwa wananchi waweze kuwafahamu kiraisi pamoja na kuwatumia watoa huduma za msaada wa  kisheria kwa wasomi wa vyuo vikuu vilivyopo nchini.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.