Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi akisoma majina ya viongozi mbalimbali walioteuliwa ama waliobadilishwa vituo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam leo Septemba 20, 2019
Picha na Ikulu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amemteua Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha, Lootha Sanare, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kuchukua nafasi ya Dkt. Steven Kebwe ambaye uteuzi wake umeteguliwa.
Akitangaza uteuzi na utenguzi huo leo Septemba 20, 2019 Katibu mkuu kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi, ameeleza kuwa Rais amefanya uteuzi na mabadiliko kadhaa.
Aidha Rais Magufuli amemteua Musa Masele ambaye alikuwa msaidizi wa mkuu wa mkoa wa Geita, kuwa mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Mkoani Morogoro.
Mbali na teuzi hizo pia Rais amefanya mabadiliko ambapo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Charles Kabeho, amehamishiwa wilaya ya Chato na Mkuu wa Wilaya ya Chato Msafiri Mtemi amehamishiwa Wilaya ya Tarime.
Aidha, Rais Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi 12 watakaowakilisha Tanzania nchi mbalimbali, katika uteuzi huo wamo pia Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana na aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Modestus Kipilimba.
No comments:
Post a Comment