Habari za Punde

Ukusanyaji wa Mzuri wa Mapato Unaofanya na ZRB Umeiwezesha Serikali Kupanga na Kutekeleza Mipango ya Maendeleo.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika viwanja vya Bodi ya Mapato Zanzibar, wakati wa hafla ya sherehe za kuadhimisha Miaka 20 tangu kuazishwa kwa ZRB Zanzibar.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ukusanyaji mzuri wa mapato unaofanywa na taasisi za kukusanya kodi umeiwezesha serikali kupunguza utegemezi wa bajeti katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

Dk.Shein amesema hayo katika hafla ya kuadhimisha miaka 20 ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), iliofanyika katika viwanja vya Makao Makuu ya Taasisi hiyo Mazizini Jijini Zanzibar.

Alisema mapato yaliokusanya na taasisi za ZRB na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) katika mwaka 2018/2019 ya shilingi Bilioni 727, yameifanya serikali kupunguza utegemezi wa bajeti kutoka asilimia 30.3 mwaka 2010/2011 hadi kufikia asilimia 5.1 mwaka 2019.

Alisema kiwango hicho kinadhihirisha jinsi Serikali ilivyopindukia malengo yaliyowekwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020, Ibara 68-d, iliyobainisha uwezo wa taasisi hizo kwa kukusanya jumla ya shilingi Bilioni 800 ifikapo mwaka 2020/2021.

“Uwezo wetu umeimarika ambapo mwaka 2018/2019 ZRB pekee ilikusanya wastani wa shilingi Bilioni 36.6 kwa mwezi”, alisema.

Dk. Shein alisema wakati alipoingia madarakani mwaka 2010, mapato yaliokusanywa na ZRB na TRA yalikuwa wastani wa shilingi Bilioni 13.5 kwa mwezi, huku ZRB pekee ikikusanya shilingi Bilioni 8.7 pekee.

Alisema serikali imefanikiwa kutekeleza mikakati mbali mbali ya kuimarisha utendaji na uwezo wa taasisi hiyo katika kukusanya mapato, ambapo katika mwaka 2014/2015 ilikusanya wastani wa shilingi Bilioni 16.17

Rais Dk. Shein alibainisha kuwa kutokana na ukusanyaji huo mzuri wa mapato, Serikali imeweza kuimarisha maslahi ya wafanyakazi mara nne, kutoa pensheni jamii kwa kila mzee aliefikia umri wa miaka 70 nchini pamoja na kuimarisha huduma mbali mbali za kijamii, ikiwemo afya na elimu.

“Tunapoweza kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege na bandari, tunaponunua vifaa vya utibabu na badhi ya huduma nyengine kubwa ikiwemo utoaji wa ruzuku katika pembejeo na zana za kilimo ni uthibitisho wa kuongezeka pato letu nchini”, alisema.

Alisema kurahisisha kazi ya ukusanyaji wa mapato, kuna umuhimu wa kuwaelimisha wananchi kuzifahamu vyema sheria za kodi zilizopo ili waweze kuzifuata kwa ukamilifu.

Alisema ni wajibu wa Bodi ya mapato kuhakikisha inapanga utaratibu maalum wa kuwaelimisha wananchi juu ya sheria za kodi ili waelewe wajibu wao, viwango vinavyopaswa kulipwa, wapi wakalipie na wakati upi.

Aidha, alisema Wizara ya Fedha na Mipango na Bodi zinazoshughulikia ukusanyaji wa kodi unapaswa kuwa na wataalamu waliobobea ili waweze kufanyakazi katika taasisi za Uwekezaji.

Alisema baadhi ya wamiliki wa hoteli hawalipi kodi ipasavyo kwa mujibu wa viwango vinavyopaswa kulipwa na kubainisha kuwa hiyo ni changamoto inayopaswa kushughulikiwa pamoja na wafanyabaishara wanaokodisha nyumba za wageni.

“Tuelekeze juhudi zetu katika matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa katika ukusanyaji na ulipaji kodi”, alisema.

Katika hatua nyengine,  Dk.Shein aliwataka wafanyakazi wa taasisi za kukusanya mapato kuendelea kufanyakazi kwa uadilifu na uzalendo na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha nzuri, sambamba na kutoa huduma kwa kuzingatia wakati wawapo kazini.

Aidha, aliitaka ZRB kuandaa mazingira mazuri pamoja na miundombinu ya kisasa kwa lengo la kurahisisha ukusanyaji na ulipaji wa kodi pamoja na kuhakikisha wafanyakazi wanataaluma za kutosha.

Alibainisha kuwa njia bora zaidi katika kupata ufanisi kazini ni kuhakikisha kuna wakusanyaji kodi waliosomea fani mbali mbali zinazohusu ukusanyaji na ulipaji wa kodi.

Mapema, Waziri wa Fedha na Mipango. Balozi Mohamed Ramia aliwakumbusha wafanyakazi wa ZRB  dhima waliyonayo ya kufanyakazi kwa uangalifu na kuepuka changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika mazingira yao ya kazi.

Alisema kazi ya ukusanyaji wa kodi inahitaji hekima na busara, kwa kutambuwa kuwa wateja wao ni watu wenye tabia tofauti.

Nae, Kamishna Mkuu wa ZRB, Ndg.Joseph Abdalla Meza, alisema kwa nyakati tofauti uongozi wa ZRB umekuwa ukiwakumbusha wafanyakazi umuhimu wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Alisema malengo ya taasisi hiyo hivi sasa ni kujenga jengo jipya la ghorofa nne katika eneo la Gombani kisiwani Pemba ili kuimarisha utendaji.

Aidha, alisema miongoni mwa mikakati na mipango ya taasisi hiyo iliyotekelezwa na kufanikisha makusanyo mazuri ya mapato ni pamoja na kufanya tafiti saba mbali mbali.

Alisema katika kipindi chote tangu taasisi hiyo iundwe, imefanikiwa kujenga mashirikiano na taasisi mbali mbali ikiwemo TRA, mashirika pamoja na Benki, hususun katika suala la kubadilishana uzoefu.

Meza, alisema changamoto kubwa inayolikabili taasisi hiyo ni ile ya baadhi ya wamiliki wa Hoteli kutoainisha viwango halisi vya tozo wanazotoza wageni pamoja na kushindwa kutoa risiti wakati wa mauzo, au kutoa risiti zisizo na uhalisia.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.