Habari za Punde

Dkt.Kijaji Awakalia Kooni Waliochepusha Mabati ya Kijiji Cha Banbare Wilayani Kondoa.

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Bambare  wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani),  alipokuwa anatolea majibu ya baadhi ya changamoto zilizotolewa na wanakijiji hao.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Bambare  wilayani Kondoa, ambapo wananchi hao walimuomba awasaidie mabati ili kuweza kukamilisha ujenzi wa madarasa kijijini hapo.

Na. Mwandishi wetu, Kondoa
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia  ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amemuagiza Afisa Mipango wa Wilaya ya Kondoa Bw. Joshua Mnyangáli kufuatilia yalipopelekwa mabati ya Shule ya Msingi Gayo iliyopo katika Kijiji cha Bambare yaliyotolewa na Mbunge huyo ili kumalizia vyumba vya madarasa ya shule hiyo.

Agizo hilo amelitoa alipofanya ziara katika Kijiji cha Bambare wilayani Kondoa wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ukarabati wa shule, vituo vya afya na miundombinu ya maji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa hajui nini kimetokea hadi shule hiyo haijapelekewa mabati wakati alinunua mabati zaidi ya 1000 na kuagiza yagawanywe idadi sawa kutoka na na uhitaji wa kila shule ili ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilike na wanafunzi waweze kusoma vizuri.

Wananchi wa Kijiji hicho walieleza kuwa kumekuwa na changamoto ya mabati kwa ajili ya umaliziaji wa vyumba vya madarasa ambayo walikuwa wameanza kujenga kwa kutumia nguvu kazi yao.

Dkt. Kijaji alishangazwa na taarifa za ukosefu wa mabati kwa ajili ya kuezeka maboma hayo ya madarasa wakati alikwishatoa mabati na ndio sababu amemwagiza  Afisa Mipango wa Wilaya hiyo kufuatilia yalipo mabati hayo na yapelekwe kijijini hapo ili kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa.

Mbunge huyo alisema kuwa iwapo kutakua na matumizi yasiyofaa ya mabati hayo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kukwamisha juhudi za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Katika kuhakikisha vyumba hivyo vya madarasa vinakamilika kwa haraka nachangia tena shilingi milioni moja ili kuharakisha umaliziaji wa vyumba hivyo vya madarasa uweze kufanyika kwa haraka ili wanafunzi wetu waweze kutumia madarasa hayo”, alisema Dkt. Kijaji.

Aidha Dkt. Kijaji aliuagiza uongozi wa wilaya hiyo hukakikisha wanafuatilia vizuri utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi inayofadhiliwa na Serikali ili kuhakikisha ina kamilika kwa wakati kwa sababu Serikali haianzishi mradi mpya bila kutoa fedha zote za miradi husika.

Kwa upande wake Afisa Mipango wa Wilaya ya Kondoa Vijijini Bw. Joshua Mnyangáli alimuahidi Dkt. Kijaji kutekeleza agizo hilo na kuhakikisha mabati hayo yanafikishwa sehemu husika kama ilivyoelekezwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Kondoa, Dodoma Alhaji Othman Gora akiwasalimia Wananchi wakati wa mkutano wa hadhara kati ya Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji na Wananchi wa Kijiji cha Bambare alipotembea Kijiji hicho. 
Bw. Haji Juma akimuelezea  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango  ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (hayupo pichani), changamoto ya mabati yaliyokwamisha umaliziaji wa madarasa hayo kijijini hapo
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambae pia ni Mbunge wa Kondoa Vijijini Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akiteta jambo na Diwani wa Kata ya Bambare Bw. Adam Iyerya  alipotembea Kijiji hicho.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.