Habari za Punde

Uzinduzi wa kampeni ya chanjo kwa kuimarisha afya za wananchi wafanyika Mkwajuni

 Waziri wa Kazi Uwezeshaji Wazee Wanawake na Watoto Maudline Castico akizungumza na Wananchi katika Uzinduzi wa  Kampeni ya Chanjo ya Kitaifa katika Viwanja vya Skuli ya Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A (kulia) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Halima Maulid na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Vuai Mwinyi .
 Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dr. Fadhil Mohamed akitoa maelezo kuhusu maradhi ya Surua, Polio na Rubella katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo kitaifa katika Viwanja vya Skuli ya Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A.
 Mwakilishi wa Shirika la UNICEF Dk. Maha Damaj akitoa hotuba kwa niaba ya wadau wa maendeleo kwenye uzinduzi wa chanjo ya kitaifa katika  Viwanja vya Skuli ya Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A.
Wananchi wa Wilaya ya Kaskazini A wakifuatilia uzinduzi wa chanjo ya kitaifa katka Viwanja vya Skuli ya Mkwajuni Wilaya ya Kaskazini A.
 Picha na Khadija Khamis -Maelezo Zanzibar .

Na Kijakazi Abdalla            Maelezo         
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  imeamua kufanya kampeni ya chanjo kwa kuimarisha  afya za wananchi ili kutokomeza maradhi yanayowasumbua watoto.
Akizindua kampeni ya chanjo ya surua,rubella na polio katika uwanja wa Skuli ya Mkwajuni, Wilaya ya Kaskazini A Unguja kwa niaba ya Mama Salma Kikwete, Waziri wa Kazi,Uwezeshaji,Wazee, Wanawake na Watoto Maudline Cyrus Castico.
Amesema kuwa kufanikiwa kampeni hiyo ni hatua itakayoweza kupunguza kuenea maradhi hayo na kuyafanya yasiwe tatizo kwa watoto.
Aidha alisema kuwa watoto ambao hawajapatiwa chanjo hizo wananafasi kubwa ya kuambukizwa maradhi hayo na hata kupelekea kupata ulemavu na hata kifo.
Mama Castico alieleza kuwa takwimu za maradhi hayo ulimwenguni imeongezeka kwa kasi ambapo kwa Zanzibar idadi ya watoto wanaogua maradhi hayo imepungua hadi kufikia 28.
Aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina lengo la  kupunguza vifo vya watoto vinavyosababishwa na maradhi hayo kwa thuluthi mbili ifikapo 2022.
Aidha aliwataka wazazi kushiriki kikamilifu katika  kampeni za chanjo katika vituo vilivyopangwa na kuwahakikishia kuwa dawa zinazotolewa kukinga maradhi hayo hazina madhara yoyote na zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani.
Nae Naibu Katibu Mkuu  Wizara ya Afya Halima Maulid amewataka wananchi walipe umuhimu suala la chanjo kwani inasaidia watoto katika ukuaji mzuri wa afya zao.
Aidha alisema kuwa Serikali imekuwa ikichukua jitihada kwa kushirikiana na mashirika ya Umoja wa Mataifa, WHO na UNICEF ili kuwakinga watoto na maradhi mbalimbali  yanayowasumbua afya zao.
Muwakilishi kutoka Shirika la UNICEF Bibi Maha Damaj amesema mpango wa kuwapatia chanjo watoto unalengo la kuwakinga  na athari ya maradhi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.